Tanzania: 'Tunapolinda mipaka yetu tusitafsiriwe kama tunawazuia wakimbizi'

Chanzo cha picha, Wizara ya mambo ya ndani Tanzania
- Author, Munira Hussein
- Nafasi, BBC Swahili
Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania George Simbachewene amesema kuwa Ripoti ya Umoja wa mataifa juu ya Tanzania kurudisha wakimbizi wa msumbuji haina uhalisia wowote.
Katika mahojiano na BBC Simbachawene amesisitiza kuwa Tanzania inalinda mipaka yake na kujilinda dhidi ya magaidi ambao wakati mwingine wanaweza kujichanganya na wakimbizi kisha kuingia nchini.
''Hakuna uhalisia wowote wa ripoti hii Je unawezaje kuwajua wanapotaka kuvuka kuja upande wa pili, je unawezaje kuwajua kama humo hakuna magaidi, sisi tunaogopa hawa magaidi, tunalinda mipaka yetu na tunapolinda tusitafsiriwe kama tunawazuia wakimbizi'' anasema Waziri Simbachawene.
Wiki iliyopita Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika Wakimbizi (UNHCR) lilisema limepokea ripoti kuwa wakimbizi wa Msumbiji wapatao 600 waliokimbilia Tanzania wametakiwa kurejea kwao.
"UNHCR ina wasiwasi juu ya familia zilizozuiwa makazi au kulazimishwa kurudi kwao na Tanzania," taarifa imeeleza.
Hata hivyo Waziri Simbachewene amesisitiza kuwa wakimbizi hao wanaweza kuhifadhiwa na Msumbiji yenyewe kwakua sehemu yenye machafuko ni wilaya moja hivyo hakuna haja ya Tanzania kuwa suluhisho.
'Serikali ya Msumbiji itajihidi kushughulika nao, eneo lenye machafuko ni wilaya moja tu, hivyo wawapeleke sehemu ambayo haina machafuko, ni wilaya moja tu, nyingine zote kuko salama inakuaje suluhisho iwe Tanzania?. Anasema Waziri Simbachawene.
Kumekuwa na ghasia nchini Msumbiji katika mji wenye utajiri wa gesi, Cabo Delgado tangu mwaka 2017.

Chanzo cha picha, AFP
Kutokana na machafuko hayo kuna wakimbizi ambao wamekwama msituni wakiwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula na maji, baadhi walikimbilia kusini na wengine kaskazini katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Shambulio la mwezi Machi lililotokea Palma limelazimisha watu wapatao 10,000 kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa UNHCR.
Maelfu ya watu wamekimbilia msituni wakati wanamgambo wa kiislamu walipoanza kushambulia, ambapo wanamgambo hao wanaripotiwa walikuwa wakiwachinja wananchi.
Watu kadhaa wameuawa , wakiwemo raia wawili wa kigeni ingawa hakuna taarifa rasmi kuhusu idadi ya vifo vilivyotokea.
Wasiwasi wa usalama baada ya shambulio hilo umefanya kampuni kubwa ya kifaransa ya mafuta Total kuondoka katika eneo hilo ambalo walikuwa wamewekeza mabilioni ya fedha katika mradi wa gesi huko Afungi peninsula, kilomita chache kutoka Palma.
UN pia imelazimika kusitisha operesheni zake za ndege kutoka Afungi, na kusababisha maelfu ya watu kuwa na sintofahamu.
Taasisi ya majanga nchini Msumbiji imesema kuwa watu wapata 30,000 wanahitaji kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Unaweza pia kusoma:
Wafanyakazi wa mashirika ya msaada na wamishionari kwa sasa wanawasaidia mamia ya wakimbizi waliokimbia makazi yao katika mji wa Pemba.
Wengi wa wakimbizi wanasaidiwa na ndugu na marafiki, UNHCR imesema.
Mapigano hayo yamesababisha watu zaidi ya 2,600 kuuawa, huku nusu yao wakiwa raia na watu wapatao 700,000 kukimbia makazi yao.












