Cabo Delgado: Uhusiano uliopo kati ya mali asili,uasi na mapigano nchini Msumbiji

Chanzo cha picha, Getty Images
Uasi unaoendelezwa na kundi moja la kiislamu katika kona ya juu ya taia la Msumbiji umegeuka na kuwa vita vya wazi ambavyo vimesababisha mauaji ,watu kukatwa vichwa na kutekwa kwa miji kadhaa katika wiki za hivi karibuni katika Mkoa wa Cabo Delgado.
Eneo la kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na machafuko hayo tangu mwaka wa 2017. Wanamgambo wanaohusishwa na kundi hilo.
Islamic State (IS) wamehusika na mzozo katika eneo hilo lenye Waislamu wengi. Mapigano hayo yamesaabisha mauaji ya watu 2500 ilhali 700,000 wameachwa bila makaazi.
Wanamgambo walifanya mashambulizi ya kushtukiza katika Mji wa Palma mapema wiki jana kwa kushambulia Maduka ,benki na kambi za jeshi. Mamia ya watu walitoroka mashambulio hayo kwa kukimbilia vichakani na vijiji vilivyo karibu.Takriban wafanyikazi 180 wa kigeni na wa kampuni moja ya gesi walikimbilia usalama wao katika hoteli ya Amarula Palma.
Wapiganaji hao wana uhusiano upi na kundi la Islamic State?
IS limedai kuwajibikia msururu wa mashambulizi ya hivi karibuni nchini Msumbiji ambayo ina asilimia 18 ya Waislamu na inaonekana kuendeleza shughuli zake katika eneo hilo kama sehemu ya 'oparesheni zake' ambazo inazidi kuzisambaza katika maeneo mengi ya bara la Afrika.
Dhana ya kuwepo kwa harakati za kijihadi zinazolenga kusambaza itikadi kali za kidini imepewa uhalisia na hatua ya wanamgambo wenyewe kutanagaza hadharani uaminifu kwa kundi la Islamic State mwaka jana.
Uhusiano huo unazinufaisha pande zote.
Je wenyeji wanabaguliwa?
Waangalizi wanasema kuibuka kwa uasi nchini Msumbiji ni sawia kabisa na kuchipuka kwa kundi la Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria ambapo kundi hilo linatumia lalama za wenyeji kuendeleza mashambulizi dhidi ya mamlaka na mashirika ya kigeni katika eneo hilo na kuzihangaisha jamii katika eneo hilo. Maelfu ya vijana ambao wamechoshwa na utawala fisadi pia wameahidiwa nafasi za kazi kwa kujiunga na kundi hilo .
Serikali kuwaajiri mamluki
Ijapokuwa serikali ya Msumbiji iko kimya kuhusu kukubali uwepo wao, makandarasi wa jeshi la kibinafsi wamekuwa wakifanya kazi katika mkoa huo pamoja na vikosi vyake vya usalama.

Hapo awali mnamo 2019, mamluki wa Urusi kutoka kikundi cha Wagner walikuwa wakiendesha shughuli katika eneo hilo
Hivi majuzi, Kikundi cha Ushauri cha Dyck chenye makao yake Afrika Kusini DAG) kiliaminika kualikwa na serikali ya Msumbiji kuisaidia kupambana na waasi.
Ripoti ya hivi karibuni ya Amnesty International juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa huko Cabo Delgado ilihusisha kundi hili pamoja na vikosi vya serikali, na wanamgambo katika mauaji ya kiholela ya raia.
DAG inasema inachunguza madai yaliyotolewa dhidi yake
Kuna wasiwasi kwamba mzozo huo, iwapo hautashughulikiwa vizuri unaweza kuenea katika nchi jirani ya Tanzania, na labda hata hadi Afrika Kusini.
Kampuni za kimataifa za gesi - zilizo tayari kuwekeza mabilioni katika uwanja wa gesi wa pwani uliyogunduliwa pwani ya Cabo Delgado - sasa zinaogopa , haswa kwa sababu ya ukosefu wa usalama, lakini pia kwa sababu ya kushuka kwa bei ya gesi.
Waangalizi wengi na wachambuzi wanaamini kuwa, kimsingi, suluhisho la mzozo liko katika kuhakikisha pana utawala bora, uwazi, kushughulikia kero za uchumi na kijamii, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa haki ya kumiliki ardhi, kazi, na sehemu ya mapato yoyote ya gesi.
"Unaposikia tuhuma hizi za majeruhi ya raia zinazohusisha wakandarasi wa jeshi la kibinafsi, inaiweka serikali katika picha mbaya," anasema Emilia Columbo, mshirika mwandamizi katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa cha Washington.
Kuna wasiwasi pia juu ya ufanisi wa wakandarasi hawa wa kibinafsi.
Kaimu mratibu wa kukabiliana na ugaidi wa Marekani John Godfrey amesema kuhusika kwa mamluki "hakujasaidia" serikali ya Msumbiji katika kukabiliana na tishio linalowakabili kutoka kwa wanamgambo.
Chimbuko la mzozo ni nini?
Cabo Delgado ni mkoa ulio na umaskini mkubwa na kuna malalamiko juu ya upatikanaji wa ardhi na ajira.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini umuhimu wa Cabo Delgado kwa serikali, na sababu zaidi ya malalamiko ya ndani, iko katika akiba tajiri ya gesi asilia inayochimbwa hivi sasa pwani mwa eneo hilo kwa kushirikiana na kampuni za nishati za kimataifa.
Inaonekana kwamba wanamgambo hao wamepata mafanikio makubwa katika kupata makurutu kutoka kwa mkoa huo na zaidi.
Acled imerekodi zaidi ya visa 570 vya vurugu kutoka Januari hadi Disemba mwaka wa 2020 katika jimbo hilo.
Hizi ni pamoja na mauaji, kukatwa vichwa na utekaji nyara, na vifo kutoka kwa mashambulio yaliyofanywa na vikundi vyote vilivyohusika katika mzozo kuongezeka sana mwaka jana.
Tukio la kutisha zaidi lilikuwa la watu 50 kukatwa vichwa katika uwanja wa michezo katika kipindi cha wikendi.
Makundi ya haki za binadamu yameripoti uharibifu mkubwa wa majengo kote kaskazini mwa Msumbiji na wanamgambo. Ukosefu wa utulivu umesababisha idadi kubwa ya watu kutoroka makazi yao katika maeneo ambayo mzozo umezuka.
Karibu watu 670,000 walikuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Cabo Delgado, Niassa na Nampula mwishoni mwa mwaka 2020, kulingana na Ofisi ya UN ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu.













