Wanajeshi 300 wa mafunzo watumwa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, huku kukiwa na wasiwasi

Chanzo cha picha, AFP
Umoja wa Mataifa umesema kuwa umefanikiwa kuukomboa mji wa Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambao ulikuwa umetekwa na waasi siku ya Jumanne.
Msemaji wa umoja huo amesema walinda usalama wa Umoja wa mataifa na vikosi vya usalama wa kitaifa vimeudhibiti mji huo baada ya kuwakabili wanamgambo walioamua kutoroka msituni.
Amesema raia waliyokuwa wametoroka mji huo baada ya mapigano kuzuka wameanza kurejea nyumbani.
Jamhuri ya Afrika ya Kati inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu Jumapili hii.
Serikali imemlaumu rais wa zamani François Bozizé, kwa kuunganisha makundi yaliyojihami katika jaribio la kufanya mapinduzi - madai ambayo amekanusha.
Urusi na Rwanda zimepeleka mamia zaidi ya wanajeshi kusaidia serikali, huku waasi wakijaribu kuelekea mji mkuu wa Bangui.
Urusi imetuma askari wa ziada 300 wa mafunzo katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kukabiliana na kile Wizara ya mashauri ya kigeni ya nchi hiyo imesema "kushuka kwa kiwango cha usalama kwa hali ya juu ".
Inasema serikali ya CAR, ambayo inatishiwa na makundi ya waasi kabla ya uchaguzi wa Jumapili wa urais, ilikuwa imeomba usaidizi.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Bogdanov amesema kuwa wanajeshi wa Urusi hawahusiki katika mapigano katika CAR na kwamba watoa wakufunzi wa kijeshi "sio wanajeshi wala kikosi maalumu".

Chanzo cha picha, AFP
Lakini msemaji wa serikali alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema Urusi imetuma "mamia kadhaa ya wanajeshi na silaha nzito " nchini humo kuunga mkono serikali.
Msemaji huyo , Ange Maxime Kazagui, alisema kuwa Urusi ilialikwa kama sehemu ya makubaliano ya ushirikiana, limeripoti shirika la habari la AFP.
Walinzi binafsi wa Urusi wamekuwa wakifanya kazi katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati kutoa ulinzi kwa serikali na kusaidia kulinda mali muhimu za kiuchumi.
Takriban wanajeshi 750 wa Rwanda na maafisa wa polisi wamekuwa wakifanyia kazi nchini humo chini ya kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa kinachojulikana kama Minusca.
Rwanda imepeleka kile inachokiiya "kikosi cha ulinzi " katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati baada ya walinzi wake wa amani kushambuliwa na waasi katika mji mkuu, Bangui.
Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema kwamba nchi yake iliamua kutuma askari katika Jamuhuri ya Afrika ya kati ili kulinda askari wa nchi hiyo waliomo katika kikosi cha umoja wa mataifa ambao wamekuwa wakilengwa na wanamgambo wenye silaha.

Chanzo cha picha, AFP
Rais Faustin Archange Touadéra amesisitiza kuwa uchaguzi wa Jumapili utaendelea kama ulivyopangwa, akisema kuwa uwepo wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa unamaanisha kuwa watu hawana la kuogopa.
Lakini vyama vya kisiasa vya upinzani, kikiwemo cha Bw Mr Bozizé, vimetoa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi "hadi amani na usalama vitakapopatikana ".
Makundi ya waasi yamechukua yakidhibiti wa miji kadhaa iliyopo karibu na mji mkuu Bangui, huku wakikabiliana na vikosi vya usalama na kupora mali, na Umoja wa Mataifa umesema kuwa wanajeshi wake wanafanya hima kuleta amani Bangui.

Chanzo cha picha, AFP
Msemaji wa Bw Bozizé Christian Guenebem alisema : "Tunakanusha kabisa kwamba Bw Bozizé ni chanzo cha kila kitu ."
Wahusika wakuu katika mzozo ni akina nani?
Bw Bozizé, ambaye ni Mkristo, aliingia madarakani baada ya mapinduzi ya mwaka 2003 na akashinda uchaguzi ambao uliangaliwa na watu wengi kama uchaguzi uliotawaliwa na wizi wa kura. Alipinduliwa mwaka 2013 na wanamgambo wa Séléka - muungano wa waasi wa waislamu walio wachache -ambao unamshutumu kuvunja makubaliano ya amani.
Tangu wakati huo nchi hiyo imekumbwa na zozo baina ya vikosi vinavyoitwa Séléka na kinachoitwa "anti-Balaka" ambacho zaidi ni cha Wakristo.
Ni lipi tisho kwa sasa?
Jumapili , makundi mengine matatu makuu ya waasi yalitangaza kuwa wameunda muungano waliouita Patriots for Change (CPC), awakimshutumu Rais Touadéra kwa kujaribu kuiba kura katika uchaguzi ujao.
Katika taarifa yake CPC uliwaalika "makundi yote kujiunga nao " na wakaomba wajumbe wote "kuheshimu maadili ya raia ".
Huku kampeni za uchaguzi zikipamba moto, Facebook ilisema wiki iliyopita kuwa imebaini kampeni za upotoshaji ili kushawishi upigaji kura-uliopangwa na watu binafsi wenye uhusiano na jeshi la Ufaransa na mfanyabiashara maarufu wa Urusi Yevgeniy Prigozhin.
Urusi imetuma "mamia kadhaa ya wanajeshi na silaha nzito " nchini humo kuunga mkono serikali, shirika la habari la AFP limemnukuu msemaji wa serikali ya Jamuhuri ya Afrika ya kati akisema.
Moscow imeimarisha uhusiano wa karibu na Jamuhuri ya Afrika ya kati hivi karibuni . Washauri wa masuala ya kijeshi wa Urusi kwa sasa wako nchini humo kusaidia kutoa mafunzo vikosi vya serikali
Ripoti ya wachunguzi wa Umoaja wa Mataifa, jeshi la Marekani na Waandishi wa habari pia imebaini shughuli za kundi la Wagner Group, ambalo ni kampuni binafsi ya kijeshi inayodaiwa kumilikiwa na mrusi Bw Prigozhin.












