Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Ukimbizi' wa Lissu, Lema na siasa mpya za Tanzania

- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
KAMA mfuatiliaji wa siasa za Tanzania katika kipindi cha miaka 10 hadi 20 iliyopita akiulizwa ataje wanasiasa watano jasiri na waliopitia magumu katika safari yao ya kisiasa hapa nchini; majina mawili hayatakosekana katika orodha yake.
Kwanza litakuja jina la Tundu Lissu na la mwenzake Godbless Lema halitakuwa mbali naye.
Hawa ni wanasiasa wawili ambao wamewahi kuwa wabunge wa Bunge la Tanzania na viongozi wa ngazi za juu wa upinzani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Hadi sasa, Lissu aliyekuwa mgombea urais waChadema katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika mwezi uliopita, ndiye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini wakati Lema ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Lissu, tangu wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, amewahi kupigwa mabomu ya machozi, kufunguliwa kesi za kutosha mahakamani, kulala mahabusu na mwaka 2017 alinusurika kifo baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa mjini Dodoma.
Kama kuna mtu ambaye maisha yake ya sasa yanasadifu kisa cha Lazaro wa kwenye Biblia, basi mtu huyo ni Tundu Lissu. Ni miujiza tu ya Mwenyezi Mungu kwamba yu hai kiasi kwamba aliwania urais mwaka huu.
Lema naye amepitia machungu mengi ikiwamo kufungwa jela katika Gereza la Kisongo kwa takribani miezi mitano, kufukuzwa bungeni, kushitakiwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya kisiasa na changamoto nyingine mbalimbali za wanasiasa mashuhuri wa upinzani hapa nchini.
Kama unataka mifano ya wanasiasa jasiri Tanzania, wawili hao wana rekodi nawameweka viwango vyao. Hata hivyo, katika kipindi cha wiki moja iliyopita; wawili hao wametangaza kwamba maisha yao yako hatarini na wanahofia uhai wao kiasi cha kukimbilia katika nchi za kigeni kuomba kulindwa.
Kwa tafsiri ya sheria za kimataifa, maana yake ni kwamba wanasiasa hawa wameomba hifadhi ya kisiasa katika nchi za ughaibuni; Lissu akitangaza kuishi katika makazi ya Balozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam na Lema akikimbilia Kenya na kudai kwamba Tanzania sasa imegeuka kuwa "Persecution Paradise" (Pepo ya Watesi).
Kama Lissu na Lema ambao kwa muda mrefu walikuwa kama alama ya ujasiri na mapambano dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wameamua kuondoka Tanzania kwa kuhofia uhai wao, nini sasa kinaendelea katika siasa za Tanzania?
Swali hili litajibiwa mwishoni mwa uchambuzi huu lakini kwanza ni muhimu kufahamu nini hasa kilichofanywa na wanasiasa hawa mashuhuri wa Tanzania.
Tamko la Haki za Binadamu na Mkataba wa Wakimbizi
Desemba 10, mwaka 1948, wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) walipitisha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) ambalo liliweka msingi wa masuala ya haki za binadamu.
Mojawapo ya masuala ya haki za binadamu yaliyofanyiwa kazi lilihusu mambo ya wakimbizi ambapo wanachama walikubaliana kwamba itakuwa marufuku kuzuia mtu anayeomba hifadhi nchini kwako kwa kuhofia uhai wake au mateso katika nchi anayotoka.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ndilo hasa lilipewa kazi ya kuhudumia watu wa namna hii na ndiyo sababu taarifa kutoka Kenya alikokwenda Lema zilieleza kwamba jambo lake lilikuwa linafanyiwa kazi na shirika hilo.
Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951 na sheria iliyokazia mkataba huo ya mwaka 1967, ndivyo hasa zinazoipa UNHCR kutimiza majukumu yake kisheria.
Kwa sababu hiyo, kilichofanywa na Lema na Lissu kuomba hifadhi walipoomba, hakijavunja sheria yoyote. Kama wanadamu wanaolindwa na UDHR na Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951, wana haki - kama ilivyo kwa watu wengine wote duniani, kwenda kuomba hifadhi katika nchi nyingine kama wanaona kwamba maisha yao yatakuwa hatarini endapo watabaki katika nchi yao ya asili.
Ni mkataba huo na sheria nyingine za kimataifa ndizo zilizofanya Tanzania ipokee mamilioni ya wakimbizi kutoka katika Nchi za Maziwa Makuu zilizokuwa katika vita za wenyewe kwenye miaka ya nyuma.
Mshtuko kwa wafuasi wa upinzani
Hatua ya vinara wawili wa upinzani kuomba hifadhi katika nchi za kigeni imepokewa kwa mshtuko mkubwa na jamii ya Watanzania.
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992, Tanzania haijawahi kuwa na mwanasiasa mashuhuri aliyeomba hifadhi nje ya nchi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, kulitokea mauaji Zanzibar yaliyosababisha baadhi ya wananchi wa visiwa hivyo kukimbilia Kenya na kwingineko kuomba hifadhi. Hata hivyo, wakati huo, hakuna mbunge au kiongozi mkubwa aliyeomba hifadhi.
Inabidi kurudi nyuma miaka takribani 50 iliyopita, wakati wa utawala wa chama cha TANU, chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ndipo wanasiasa maarufu kama Oscar Salathiel Kambona, walikimbia kwenda uhamishoni nchini Uingereza kwa sababu za kisiasa kama ilivyo sasa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam, Abbas Mwalimu, alisema kwamba anaamini kwamba wanasiasa hao wawili walikuwa na sababu ya kufanya walivyofanya kwa vile hakuna mwanasiasa anapenda kuacha nchi yake kwenda ughaibuni.
" Kwanza tukubaliane kwamba walichofanya kiko ndani ya uwezo wao kisheria. Kama mtu anaona maisha yake au familia yake yako hatarini, ana haki ya kwenda kuomba hifadhi kokote.
"Hata hivyo, jambo moja ambalo linanitatiza hadi sasa ni kwamba kwanini wanasiasa hawa hawakuondoka kabla au baada ya uchaguzi na badala yake waondoke sasa? Mimi nadhani walikuwa tishio zaidi wakati wakiwa wanawania madaraka na wagombea wa CCM lakini sasa wameshindwa uchaguzi wanaogopa nini?"alisema Mwalimu.
Lissu na Lema, kwa nyakati tofauti wameeleza kwamba hofu yao imetokana na vitisho walivyopewa na watu kupitia simu zao za mkononi au wasamaria waliowaeleza kwamba kuna njama ovu zinapangwa dhidi yao.
Athari za hatua za kina Lissu
Kwa mujibu wa mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, itakuwa vigumu sana kuendesha siasa za upinzani nchini Tanzania wakati vinara wa upinzani wakiwa nje ya nchi. Ametumia mifano ya ndani na nje ya nchi; Kambona kwa ndani na Leopoldo Lopez wa Venezuala kimataifa.
" Kwa Afrika, ni vigumu sana kwa chama cha upinzani kushinda endapo viongozi wake wakubwa watakuwa nje ya nchi. Namna pekee ya kuwatia nguvu wanachama na wafuasi ni kupambana ukiwa ndani ya nchi. Tumeona mfano wa Kambona kwa Tanzania na Lopez kule Venezuela.
" Wapinzani walikuwa wanakaribia kumwondoa Rais Nicholas Maduro wa Venezuela. Lakini mwaka 2014, kiongozi waupinzani, Lopez, akakimbilia kwenye ubalozi wa Hispania na sasa ameenda Hispania. Tangu aondoke, kammaliza nguvu mwenzake Juan Guaido na upinzani kwa ujumla.
" Mimi naamini huu ulikuwa wakati mzuri kwa viongozi wa upinzani kukaa chini na kuumiza kichwa nini kinaweza kufanyika ili kuiondoa CCM madarakani. Kama wanataka kuungana, wanahitaji kuungana kwenye malengo na si kwenye kutafuta mgombea mmoja, "alisema mhadhiri huyo.
Katika duru za kimataifa, habari za kina Lissu zimeandikwa na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya kimataifa; jambo linaloweza kuchafua taswira ya Tanzania kama mojawapo ya mataifa yenye kuheshimu demokrasia na utawala wa sheria.
Tayari, mabalozi wa mataifa makubwa kama Marekani na Japan, tayari wametoa msimamo wao kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliomalizika wiki jana na kueleza kuhusu kasoro zilizokuwepo.
Jeshi la Polisi Tanzania kupitia kwa Mkuu wake, IGP Simon Sirro, limesema hadi sasa jeshi lake halijapokea malalamiko kutoka kwa mmoja wa wanasiasa hao au wote wawili kuhusu kutishiwa maisha.
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas pia amekanusha taarifa za wanasiasa hao kutishwa na kuiambia BBC kuwa wanachokifanya ni "mchezo wa kisiasa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa kidemokrasia."
Wakati serikali ikitoa taarifa hizo, kuna taarifa kwamba Lissu na Lema ni baadhi tu ya wanasiasa na wanaharakati ambao wana mpango wa kuondoka nchini haraka iwezekanavyo kuepuka kukamatwa au kufunguliwa mashitaka yasiyodhaminika.
Katika baadhi ya mitandao ya kijamii, yapo majina ya wanaharakati na wanahabari yanayosambazwa ikielezwa kwamba wahusika wako mbioni kukamatwa na vyombo vya dola.
Mambo haya yamezua taharuki nasintofahamu kubwa miongoni mwa wafuasi wa kambi ya upinzani hapa nchini.
Siku chache zijazo, zitatoa mwanga wa ni watu au viongozi wa aina gani wanaweza kufuata nyayo za akina Lissu na kwenda kuomba hifadhi katika mataifa ya kigeni.
Kama hatimaye karibu viongozi wote mashuhuri wa upinzani wataamua kuondoka kwa kuhofia maisha yao, ni wazi kwamba kutaibuka kundi lingine la viongozi wa Chadema na upinzani kwa ujumla ambao itabidi waendeleze mapambano kutoka ughaibuni.
Kama suala hili litaishia kwa Lissu na Lema peke yao kuondoka, ina maana jambo hili litakuwa habari ya muda mfupi na kupita - kabla Watanzania hawajahamisha akili zao katika tukio lingine kubwa linalofuata.
Siku chache zijazo, zitatuambia nini utakuwa mwelekeo wa siasa za upinzani katika kipindi cha angalau miaka mitano ijayo.












