Uchaguzi Tanzania 2020: Upi mustakabali wa Chadema, ACT pamoja na Membe?

Hatua yoyote itakayochukuliwa na Bernard Membe, kabla ya siku ya kupiga kura haitakuwa na athari kubwa kwa chama
Maelezo ya picha, Hatua yoyote itakayochukuliwa na Bernard Membe, kabla ya siku ya kupiga kura haitakuwa na athari kubwa kwa chama
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Baada ya vumbi la Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu kutulia, kuna chama kimoja cha siasa kina uhakika wa kuwa chama kitakachokuwa kimefanya vizuri kuliko vingine vyote; chama hicho ni ACT Wazalendo.B

Hatua yoyote itakayochukuliwa na mgombea Urais wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu, Bernard Membe, kabla ya siku ya kupiga kura haitakuwa na athari kubwa kwa chama hicho.

ACT kimeingia katika uchaguzi huu kutoka katika ule wa mwaka 2015 kikiwa na mbunge mmoja tu; Zitto Kabwe, ambaye pia ndiye Kiongozi wa Chama hicho na halmashauri moja ya Kigoma Ujiji.

Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad, walitangaza kumuunga mkono Tundu Lissu.
Maelezo ya picha, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad, walitangaza kumuunga mkono Tundu Lissu.

Kwa vyovyote vile, mara baada ya uchaguzi huu, ACT inaweza kupata wabunge zaidi ya 20 na kuna uwezekano kikawa chama cha upinzani chenye wabunge wengi katika Bunge la Tanzania mara baada ya uchaguzi huu kwa sababu ya wingi wa wabunge itakaoweza kuwapata visiwani Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania Bara.

Hata hivyo, katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi huu, chama hicho kimeingia katika sintofahamu kufuatia hatua ya viongozi wake wa juu; Zitto na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad, kutangaza kumuunga mkono mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Pamoja na viongozi wa juu wa ACT Wazalendo kutangaza kumuunga mkono Lissu, Membe amezungumza na wana habari Oktoba 19 mwaka huu na kutangaza kwamba yeye bado ni mgombea halali wa chama hicho kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Bernard Membe (kushoto) Hakufurahishwa na namna viongozi wa juu wa chama hicho walivyoshughulika na suala la kumuunga mkono Lissu.
Maelezo ya picha, Bernard Membe (kushoto) Hakufurahishwa na namna viongozi wa juu wa chama hicho walivyoshughulika na suala la kumuunga mkono Lissu.

Katika mazungumzo niliyofanya na watu wa karibu na Membe pamoja na viongozi wa ngazi ya taifa wa ACT, nimefahamu kwamba mwanadiplomasia huyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwa miaka nane wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, hajafurahishwa na namna viongozi wa juu wa chama hicho walivyoshughulika na suala la kumuunga mkono Lissu.

" BM (Membe) hajafurahishwa kabisa na namna viongozi wa chama walivyoshughulika na hili suala la kumuunga mkono Lissu. Yeye hana tatizo na kumuunga mkono Lissu lakini hajafurahishwa na namna viongozi wenzake katika chama walivyolifanya jambo hili," ameaniambia mmoja wa watu wa karibu na Membe aiyezungumza nami kwa masharti ya kutotajwa jina lake.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, watu wengi walitaraji kwamba angetangaza kumuunga mkono Lissu lakini kwa sababu viongozi wa chama chake wameshafanya hivyo lakini yeye akasema kwamba anabaki kuwa mgombea wa chama chake.

Inawezekana Membe amekwepa mtego wa ACT Wazalendo 'kushughulikiwa' na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo tayari imetangaza kwamba ni makosa kwa chama cha siasa kutangaza ushirikiano na chama kingine nje ya muda uliokubaliwa na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kwa kuzungumza kama alivyozungumza, Membe amekisaidia chama chake kuwa salama kwa Msajili katika wakati huu ambapo chama chake kinaelekea kupata mafanikio makubwa -vyovyote vile itakavyokuwa iwe atangaze kumuunga mkono Lissu au la, lakini pia hajasema jambo baya dhidi ya Lissu na hivyo uhusiano baina ya vyama hivi vikubwa vya upinzani nchini unabaki kuwa mzuri.

Hata hivyo, kuna mambo ya kutazama kiundani kutokana na mkutano wa jana wa Membe.

Hatma ya kisiasa ya Membe

Katika maisha yake ya kisiasa, Membe hajawahi kuwa mwanasiasa kipenzi cha watu. Hii ni kwa sababu ya asili ya kazi zake za utumishi wa umma alizowahi kuzifanya huku nyuma. Miaka yake takribani 20 ya kwanza ya utumishi wake aliitumia kama kachero; kazi ambayo mara nyingi hufanywa mbali na macho ya watu.

Mbunge huyu wa zamani wa Jimbo la Mtama, alijulikana zaidi wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje -nafasi ambayo kwa bahati mbaya huwa na majukumu mengi zaidi ya kusafiri nje ya nchi na hakupata fursa ya kufanya kazi zinazoonekana au kugusa maisha ya Watanzania.

Kwa haiba, Membe ni kama ilivyokuwa kwa Rais wa Awamu ya Tatu ya Tanzania, hayati Benjamin Mkapa, ambaye historia yake katika utumishi wa umma ilikuwa ya shughuli za kiserikali zaidi; lakini yeye alipata bahati ya kupigiwa debe na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati alipotaka kuwa Rais.

Jakaya Kikwete pia alipata Urais akitoka kuwa Waziri wa Mambo ya Nje lakini kuna tofauti kubwa ya haiba baina yao. Jakaya ni mtu wa watu kiasi kwamba Watanzania walikuwa wanajua hata anashabikia timu gani ya mpira wakati akiwa waziri - haijulikani Membe anashabikia timu gani hadi sasa, lakini pia kupitia marafiki zake waliojulikana kwa jina la "Mtandao" walifanya kazi kubwa ya kumfanya aonekana anafaa kuwa Rais miaka mingi kabla hajatangaza nia.

Kwa hiyo, kisiasa, mafanikio ya mtu wa aina ya Membe yanategemea vitu vikubwa viwili; Mosi, kiongozi mwingine kipenzi cha watu wa kutangaza kumuunga mkono na kumpigia debe kwa Watanzania, pili mtandao mpana wa marafiki wa kufanya kazi ya chini kwa chini kumuuza.

Mara baada ya Maalim Seif kutangaza kumuunga mkono Lissu, Membe alisisitiza kuwa yeye ndiye mgombea halali wa ACT.
Maelezo ya picha, Mara baada ya Maalim Seif kutangaza kumuunga mkono Lissu, Membe alisisitiza kuwa yeye ndiye mgombea halali wa ACT.

Kwa bahati mbaya, mwaka huu, mazingira haya mawili hayapo kwa Membe. Wakati anajiunga na ACT Wazalendo, upinzani haukuwa na uhakika wa kurejea kwa Lissu kugombea Urais. Kama hali ingebaki kuwa vile na labda kama Lissu angetangaza kumuunga mkono Membe, angeweza kuwa na nafasi nzuri ya kushindana na mgombea wa CCM, Rais John Magufuli. Angekuwa anatembea juu ya nyota wa wapinzani na mfumo wa upinzani ungembeba.

Ndani ya chama chake cha ACT, Membe bado ni mpya na hana wafuasi wa kutosha.

Bado chama hicho kina nguzo mbili za mamlaka; Zitto na Maalim Seif na Membe hawezi kushinda vita yoyote ya ndani ya chama endapo ataamua kufuata njia hiyo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Membe alizungumzia kuhusu "kufunga bao katika dakika ya 89" ya mchezo. Namna pekee ya kufunga bao hilo ni kuonekana katika mkutano wa kufunga kampeni wa Lissu uliopangwa kufanyika Dar es Salaam na kuwaambia Watanzania kuwa "Wanajua wanachotakiwa kufanya".

Kupanda kwake jukwaani kwenye mkutano wa Lissu kutaonyesha ishara kwamba naye anamuunga mgombea huyo ambaye viongozi wake tayari wametangaza kuwa watampigia kura. Pasipo kusema waziwazi kuwa naye anamuunga mkono - jambo linaloweza kukipa shida chama chake mbele ya Msajili, ujumbe kwa umma utakuwa umefika.

Kwa mchezo ulivyo sasa, Membe hawezi kwenda kinyume cha chama chake. Kama atafanya vinginevyo, atachukiwa na viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani. Ili kuwa mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika nchini, ni muhimu kwa Membe kwenda pamoja na wimbi hili la matamanio ya wafuasi wa vyama vya upinzani.

ACT inatokaje hapa ilipo sasa

ACT, kupitia kwa Kabwe, ilifanya jitihada za zaidi ya miaka miwili kumtongoza Membe ajiunge na chama hicho. Watu wengi wanafahamu chama kikubwa cha upinzani hapa nchini ni Chadema lakini Mbunge wa Kigoma Mjini alifanikiwa kufanya ushawishi Membe akatua ACT.

Ujio wa Membe ulifuatia ujio wa Maalim Seif na wenzake na umebadili kabisa ramani ya kisiasa ya Tanzania na mwonekana wa jumla wa ACT Wazalendo. Mara baada ya uchaguzi huu, ACT inaweza kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na ikawa ama chama tawala Zanzibar au chama kilicho katika Seikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa vyovyote vile, ACT Wazalendo itakuwa sehemu ya serikali kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Katika muktadha huo, ni muhimu kwa viongozi wa chama hicho kuwa na watu kama Membe ambao wamewahi kuwa serikalini na wana ushawishi mkubwa katika duru za kidiplomasia. Ingawa Zanzibar si dola, kuwa na mtu kama Membe akiwa mshauri wa masuala ya Diplomasia wa Maalim Seif ni jambo la faida.

Hata hivyo, sintofahamu ya siku za karibuni na malalamiko ya watu wa karibu na Membe yanaonyesha kuna tabia ya kufanya mambo pasipo kushirikishana au kushauriana waliyonayo baadhi ya viongozi wa ACT Wazalendo.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video, Bernard Membe alikuwa na matumaini ya kusafishwa baada ya kufukuzwa uanachama

Jambo hili la Membe lingeweza kusababisha mgogoro ndani ya chama ambao haungekuwa na sababu. Kilichotakiwa kuufanyika ni kumshawishi Membe akubali kuwa chama chao kina nafasi zaidi kikimuunga mkono Lissu na pengine kingempa yeye nafasi ya kuwa wa kwanza kutangaza kumsapoti mgombea huyo wa Chadema kwa namna ambayo ingemjengea heshima.

Kuelekea uchaguzi ujao wa mwaka 2025, ACT inatakiwa kuwa makini katika kushirikishana mambo makubwa, kuweka mfumo imara wa mawasiliano ambao hautoa ndimi mbili katika jambo moja. Hili linaweza kuwapa imani watu wengine wa aina ya Membe kujiunga na chama chao pasipo kuhofiwa kuvunjiwa heshima zao.

Kura za Wapinzani

Kwa vyovyote vile, hata kama ACT Wazalendo ingefanya kampeni kiasi gani, kura za Membe zisingeweza kuzidi zile za Lissu. Kwa hiyo, hatua ya viongozi wa ACT kutangaza kumuunga mkono mgombea wa Chadema itahamisha tu kura zao kwenda kwa Lissu.

Kura zingekuwa nyingi zaidi endapo uamuzi wa kumuunga mkono Lissu ungefanywa mapema kabla jina la Membe haljaingizwa katika karatasi za kupigia kura. Hata hivyo, kutetea wapinzani, kulikuwa na mazingira fulanifulani yaliyofanya kumuunga mkono Lissu mapema kuwa vigumu.

Hatua ya ACT Wazalendo kumuunga mkono Lissu inatengeneza nguzo ya ushirikiano imara wa vyama hivi viwili katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Kama wapinzani wakifanikiwa kupata viti vya kutosha bungeni na wakaweza kuunda Kambi ya Upinzani yenye nguvu na hoja nzito na huku ikitengeneza msingi imara wa ushirikiano na muungano ifikapo miaka mitano ijayo, wanaweza kuvuna wafuasi wengi zaidi uchaguzi ujao.

Itakuwa vigumu sana kwa upinzani kushinda katika uchaguzi dhidi ya Rais aliye madarakani, lakini ushirikiano huu unajenga hamu ya kuwa imara zaidi kwenye uchaguzi ujao dhidi ya mgombea mpya wa chama tawala ambaye hatakuwa Rais aliye madarakani.