Ubalozi wa Marekani waeleza kusikitishwa kwa kukamatwa kwa wapinzani na kufungiwa gazeti Tanzania

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tamko la kusikitishwa na walichokiita hatua za serikali ya Tanzania kuminya demokrasia.
Hatua hizo kwa mujibu wa tamko lililotolewa na ubalozi wa Marekani leo Alhamisi ni pamoja na kuwakamata viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wakiwa katika vikao vyao vya ndani na kufuta leseni ya gazeti la "chama cha siasa cha upinzani."
"Hatua hizi ni mwendelezo wa mlolongo wa matukio ya kusikitisha ya vitisho kwa wanachama wa vyama vya upinzani, asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza ni mambo yaliyojumuishwa na yanayolindwa na Katiba ya Tanzania na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu," imeeleza sehemu ya tamko la ubalozi.
Ubalozi huo pia imeeleza kuwa unafahari kusaidia na kuunga mkono uhuru wa kujieleza na ushiriki jumuishi wa kisiasa kwa namna zote.
Tamko hilo limetoka wiki hii ambapo matukio matatu ya namna tajwa kutokea ambayo nikufutiwa leseni kwa gazeti la Tanzania Daima, kukamatwa kwa viongozi wa chama cha upinzani ACT Wazalendo na pia wafanyakazi wa kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Kufutiwa leseni Tanzania Daima
Jumanne wiki hii serikali ya Tanzania ilipiga marufuku gazeti la Tanzania Daima kuchapishwa na kusambazwa popote nchini au nje ya nchi kufuatia uamuzi wa kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo la kila siku.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya nchi hiyo, hatua hiyo ni matokeo ya 'kukithiri na kujirudia' kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi na maadili ya uandishi wa habari.
''Juhudi za kuwaonya, kuwaelekeza na kuwakumbusha wa gazeti wahariri wa gazeti hilo kufuata masharti ya leseni waliyopewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa zimeshindwa kuzaa matunda kutokana na ukaidi, ubishi, dharau kwa mamlaka za nchi na wakati fulani nia ovu ya dhahiri.'' Ilieleza sehemu ya taarifa ya serikali.

Chanzo cha picha, TANZANIA DAIMA
Mwaka 2017, gazeti hilo lilifungiwa kwa siku 90.
Kwa mujibu wa Sheria, wachapishaji wa gazeti hilo wanayo fursa ya kuomba tena leseni kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari ili kuruhusiwa kurejea kuchapisha na kusambaza watakapoona wamejitafakari na kuwa tayari kufuata taratibu.
Kukamatwa kwa Zitto Kabwe na viongozi wa ACT
Jumanne ya wiki hii pia, Kiongozi wa chama cha upinzani ACT Zitto Kabwe na wenzake saba walikamatwa katika mkutano wao wa ndani Kulwa, kusini mwa Tanzania.
Awali viongozi hao walikamatwa kwa tuhuma za kuandamana bila kibali wakiwa wanaelekea kwenye mkutano huo.
Hata hivyo, tuhuma dhidi yao zimebadilika na sasa ni kutishia uvunjifu wa amani. Wote waliachiwa jana Jumatano baada ya kulala korokoroni, na watatakiwa kuripoti tena polisi Julai mosi.

Toka mwaka 2016, vyama vya upinzani nchini humo vimepigwa marufuku kufanya mikutano ya hadhara pamoja na maandamano.
Tukio la kukamatwa kwa viongozi wa ACT limeongeza wasiwasi endapo wapinzani watapewa fursa na uhuru sawa wa kuwafikia wananchi wakati Tanzania ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.














