Gazeti Tanzania Daima lapigwa marufuku kuchapishwa na kusambazwa ndani na nje ya Tanzania

Chanzo cha picha, TANZANIA DAIMA
Idara ya habari nchini Tanzania, imepiga marufuku gazeti la Tanzania Daima kuchapishwa na kusambazwa popote nchini au nje ya nchi kufuatia uamuzi wa kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo la kila siku.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Uamuzi unatokana na 'kukithiri na kujirudia' kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi na maadili ya uandishi wa habari.
''Juhudi za kuwaonya, kuwaelekeza na kuwakumbusha wa gazeti wahariri wa gazeti hilo kufuata masharti ya leseni waliyopewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa zimeshindwa kuzaa matunda kutokana na ukaidi, ubishi, dharau kwa mamlaka za nchi na wakati fulani nia ovu ya dhahiri.'' Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Barua hiyo imeeleza kuwa kwa sababu hizo kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya mwaka 2016, Mkurugenzi wa Idara ya Habari amefuta leseni ya gazeti hilo ikiwa ni baada ya kulionya gazeti hilo kwa zaidi ya mara 10 huku gazeti lenyewe likilazimika kuomba radhi mara mbili kwa uvunjifu wa maadili ya kitaaluma na sheria za nchi ikiwemo kuchapisha habari za uongo, uchochezi na uzandiki.
Kwa mujibu wa Sheria, wachapishaji wa gazeti hilo wanayo fursa ya kuomba tena leseni kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari ili kuruhusiwa kurejea kuchapisha na kusambaza watakapoona wamejitafakari na kuwa tayari kufuata taratibu.
''Kwa mujibu wa kifungu cha 10 (1) cha sheria ya hudumaza habari Na 12, 2016, kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana na habari ndani ya siku 30 iwapo hawajaridhika na uamuzi huu.'' ilieleza taarifa hiyo, iliyotiwa saini na bwana Patrick Kipangula kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari.
Serikali imevipongeza vyombo vingine vya habari vinavyoendelea kutii sheria na kufuata misingi ya taaluma na kusema kuwa haitasita kuchukua hatua kali wakati wowote kwa watakaokiuka taratibu za kisheria na misingi ya taaluma muhimu ya habari.








