George Floyd: Kwanini baadhi ya viongozi wa kidini Washington wamekasirishwa na Trump kutumia Biblia?

Chanzo cha picha, Heidi Thompson
Siku chache baada ya Rais Trump kuonekana amesimama mbele ya kanisa la St John Episcopal akiwa ameshikilia bibilia, zaidi ya viongozi 20 wa makanisa kutoka Washington na maeneo yaliyo karibu wamepinga kile alichokifanya.
Kasisi George C Gilbert Senior ambaye ni mmoja wa viongozi hao, aliuambia umati wa watu uliokuwa umekusanyika hapo, kwamba rais alitumia Bibilia "kama chombo cha kuendeleza ajenda yake binafsi".
Kasisi Gilbert amekuwa padri katika kanisa la Holy Trinity United Baptist mjini Washington DC kwa miaka 35. Akizungumza kwa upole na unyenyekevu alielezea kughadhabishwa kwake na kile alichokitaja kuwa tabia "isiyokubalika"
"Huu ni wakati ambao katika historia ya Marekani tunahisi alichokifanya rais wetu, Donald Trump, ni kejeli," alisema.
"Kusimama mbele ya kanisa akiwa ameshikilia Bibilia mkononi wakati hana mazoea ya kuenda [mara kwa mara] kanisani ni kutokuwa mwaminifu na huo ni udanganyifu.
"Hatuwezi kumruhusu afanye hivyo bila kuwaambia watu - na kumfahamisha yeye pia - kwamba hilo halikubaliki. "
'Magenge yanayozua vurugu'

Chanzo cha picha, AFP
Siku ya Jumatatu, rais Trump alitishia kuwapeleka wanajeshi kukabiliana na "makundi ya watu wanaozua vurugu" ambayo anasema yanahujumu maandamano ya amani ya kupinga mauaji ya George Floyd,46, aliyefariki mikononi mwa polisi.
Muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake, Rais Trump alitembea mwendo mfupi kutoka Ikulu ya Marekani hadi kanisa la St John's Episcopal - linalojulikana kama kanisa la marais - na kuinua Bibilia mbele ya kamera za wanahabari. Kanisa hilo lilichomwa moto wakati wa maandamano ya siku Jumapili.
Lakini Kasisi Gilbert, na viongozi wengine wa kidini waliompinga, wanahisi hatua ya rais kufika kanisani kwa njia hiyo na kuinua Bibilia, haikuwa sawa na "haikubaliki".
"Alifanya hivyo kupiga picha, na huu sio wakati wa kujionesha"

Chanzo cha picha, AFP
Muda mfupi baada ya rais Trump kuzuru kanisani, wanahabari waliripoti kuwa vitoa machozi vilitumika kuwatawanya watu waliokuwa wakiandamana kwa amani mbele ya kanisa.
Waandamanaji hao walijumuisha mapadri kadhaa na waumini wa kanisa hilo kutoka dayosisi zingine za mji huo.
Kasisi Gilbert anahisi ni jukumu la waumini wa kanisa hilo kusimama na viongozi wengine wa kidini kupinga hatua ya rais Trump.
"Kama rais wa Marekani, alistahili kutoa hotuba ya kuwatia moyo wananchi kwa kujaribu kuelewa kilichosababisha hali inayoshuhudiwa nchini [ikizingatiwa kuwa] polisi wamekuwa wakiendelea kuwaumiza Wamarekani kwa kuwaua kiholela vijana wadogo, na kuonesha kuwa ''muda umewadia'' kukomesha uovu huo.
Taifa lililogawanyika
Sio viongozi wote wa kidini nchini Marekani wanakubaliana na hatua hiyo.

"Kwanini rais wa Marekani, kiongozi wa dunia huru, asimshirikishe Mungu katika juhudi za kuleta pamoja taifa lililogawanyika ?" aliuliza Askofu wa kanisa hilo Mariann Budde.
"Alitaka kuonesha na kukumbusha taifa kuwa tunahitaji maombi wakati huu zaidi ya kitu kingine chochote."
Askofu wa kanisa la Epscopal mjini Washington, Mariann Budde anasema alimuona kwenye televisheni mara ya kwanza rais alifika kanisani.
Alisema "hakufika hapo bila kuwazia hatua hiyo, na hakufika hapo kuwatawanya watu [katika eneo hilo] kwa kutumia vitoa machozi ili aweze kupiga picha akiwa ameinua Bibilia."
Maoni yake yalipingwa na Michael Curry, Askofu mwandamizi wa kanisa la Episcopal nchini Marekani US, ambaye alimkosoa Rais kwa kutumia "jengo la kanisa na kuinua Bilibilia kwa maslahi ya kisiasa''.
Rais Trump na kanisa

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Trump hana kanisa maalum analohusishwa nalo lakini uhudhuria ibada ya kanisa mara moja moja kukiwa na hafla maalum.
Amekuwa akitumia ishara na matamshi ya kidini kuwavutia wapiga kura wa Kikristo
Zaidi ya asilimia 75 ya Wainjilisti wazungu walimpigia kura Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kite cha Pew, ikilinganishwa na asilimia tatu tu ya Wamarekani weusi ambao ni wa dhehebu la kiprotestanti.
Kuna baadhi ya wale wanaohisi hali ya Jumatatu ya rais kuzuru kanisa la St John's ni juhudi za rais kuwavutia Wainjilisti wazungu kabla kuelekea uchaguzi mkuu.
Lakini hata wafuasi wa Rais Trump, kama vile mchungaji Burns, wanaounga mkono hatua ya kupiga picha ilikuwa ya kuimarisha msimamo wake wa kisiasa''
"Rais angesifika ikiwa angelitumia nafasi hiyo kuwaomba watu kufanya [maandamano ya amani] na kuwaambia kuwa "Niko na nyinyi, Nitaandamana pamoja na nyinyi, Naelewa kwanini mna ghadhabu."
Hata hivyo Rais Trump ametetea uamuzi weke kwenye Twitter, kwa kuandika: "Mumenielewa vibaya! Ikiwa maandamano ni ya amani, kwanini waandamanaji walichoma Kanisa usiku uliotangulia? Watu walipendezwa na hatua yangu."
Viongozi wengine wa kidini duniani wanasemaje?
Hatua ya Rais Trump kushikilia Bibilia mbele ya kanisa la St John's Episcopal limekosolewa na viongozi tofauti duniani.
Padre Antonio Spadaro, ambaye ametajwa kuwa mwandani wa karibu wa Papa Francis, aliandika katika Twitter "Wale wanaotumia Bibilia kwa maslahi yao ya kidunia nyakati za majanga wanakosea."
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa Cape Town Thabo Makgoba, "Kupiga picha kwa kutumia Bibilia ni kinyume na kile kilichoandikwa ndani yake na maana ya ujumbe uliopo ndani yake, na sote tunajua hilo linamaanisha nini Afrika Kusini."
"Nilizaliwa enzi za ubaguzi wa rangi na kukulia katika mazingira hayo. Ni miaka michache iliyopita ya maisha yangu [ndio nimeishi katika mazingira ya kidemokrasia]," alisema.
Nchini Afrika kusini, dini ilitumiwa kama njia ya kuwabagua kwa misingi ya rangi enzi ya utawala wa kibaguzi.
"Inasikitisha sana wakati wanasiasa wanapotumia kanisa ama kutumia Bibilia kwa maslahi yao binafsi," Askofu huyo Mkuu aliendelea kusema.
Nchini Uingereza, Askofu wa Liverpool, Paul Bayes, aliweka kwenye Twitter picha ya Rais Trump akishikilia Bibilia na kuambatanisha na maneno:
"Hiki ni Kitabu kizuri. Akiashiria maandiko matakatifu kuhusu: 'Upendo wa Mungu .' 'Wapende maadui zako'. Nakuomba awahukumu watu wako kwa haki, Na maskini wako kwa haki. Waokoe na kuwatetea watu masikini #BlackLivesMatter '












