George Floyd: Ulimwengu unavyofuatilia matukio nchini Marekani

Chanzo cha picha, AFP
Mataifa duniani yamekuwa yakifuatilia kwa mshangao matukio yanayoendelea nchini Marekani kufuatia maandamano ya ghasia yaliochochewa na - kifo cha George Floyd, mtu mweusi aliyefariki baada ya polisi mweupe kumzuilia chini kwa kutumia goti lake kwenye shingo hadi akashindwa kupumua.
Maandamano hayo yalioandaliwa kupinga dhulma zinazotekelezwa na polisi dhidi ya Wamarekani weusi yamechukuwa mkondo wa kibaguzi huku vurugu zikishuhudiwa katika miji tofauti ya Marekani.
Picha za maandamano hayo na magari yaliochomwa moto zinaendelea kugonga vichwa vya habari duniani huku taarifa kuhusu janga la corona zikichukua nafasi ya pili.
Kifo cha Floyd Mei 25 mjini Minneapolis ni cha hivi punde katika msururu wa mauaji ya Wamarekani weusi mikononi mwa polisi wa Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mataifa yanasema nini kuhusu maandamano hayo?
Ulaya
Vyombo vya habari duniani vimekuwa vikiangazia maaandamano ya Marekani kwa karibu.
Kurasa za kwanza za magazeti na vitengo vya uhariri wa magazeti kutoka nchini Ufaransa hadi Mexico mpaka China zimesheheni taarifa za kifo cha Floyd, maandamano ya vurugu yaliofuatia, jinsi walinda usalama walivyokabiliana na waandamanaji, na matamshi ya rais Donald Trump yalivyochochea maandamano hayo zaidi.
Maandamano ya barabarani na katika balozi tofauti za Marekani pia yamefanyika nchini Canada,Uingereza, Ujerumani na mataifa mengine nje ya Ulaya kuunga mkono wandamanaji wa Marekani wanaolalamikia ukosefu wa usawa katika jamii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji wa Tume ya Ulaya aliwasilisha kwa vyombo vya habari taarifa isiyokuwa ya kawaida kuhusu masuala ya Marekani, akiashiria kuwa maafisa mjini Brussels wanatumai kuwa "matakwa yote" yalitolewa na waandamanaji "yatapewa kipaumbele na kusuluhishwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na haji za binadamu"
Taarifa hiyo ilifuatiliwa na nyingine siku ya Ijumaa kutoka kwa Mkuu wa Tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Muhamat, ambaye alilaani mauaji ya George Floyd na kuongeza kuwa kitendo hicho ni "muendelezo wa visa vya ubaguzi dhidi ya Wamarekani weusi ambao pia ni raia wa nchi hiyo.
China
Maafisa nchini China kupitia kituo cha kituo cha habari cha kitaifa wamelaani utawala wa Trump kwa kuendeleza ubaguzi wa rangi na kushindwa kukabiliana na ghasia zinazoendelea ambazo pia zimekumbwa na visa vya uhalifu na uvunjaji wa sheria katika miji kadhaa.
Washingnton iliwahi kuikosoa China kuhusiana na jinsi ilivyokabiliana na maandamano makubwa ya Hong Kong yaliyokumbwa na vurugu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Chama tawala cha Kikomunisti cha China kilianzisha sheria ya usalama ya kitaifa yenye utata kwa Hong Kong, hatua ambayo ilionekana kama uminywaji wa uhuru.
Iran
Serikali ya Iran imekosoa jinsi utawala wa Marekani na mamlaka za usalama zinavyoshughulikia maandamano yanayoendelea nchini humo kufuatia kifo cha George Floyd, kwa mujibu wa tarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Iran, IRNA.
Siku ya Jumanne kiongozi wa mahakama, Hojjatoleslam Raeesi, alisema "Viongozi wa Marekani wanastahili kushitakiwa katika mahakama ya kimataifa kwa mauaji ya kiholela na ubaguzi wa rangi."
Msemaji wa serikali ya Iran Abbas Mousavi kwa upande wake alitoa ''wito''kwa Marekani kukomesha visa vya ukandamizaji dhidi ya watu wake na kuwpatia nafasi ya kupumua'' Washington iliwahi kuikosoa Iran kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuvunja maandamano ya kupinga serikali mwisho wa mwaka 2019.

Chanzo cha picha, Reuters
Iran imekuwa chini ya shinikizo za kiuchumi tangu Marekani ilipoiwekea upya vikwazo 2018 kwa kukiuka mkataba wa nyuklia.












