Virusi vya corona: Je ni ipi siri ya bara la Afrika kutoathirika pakubwa na corona?

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu mgonjwa wa kwanza kutangazwa Afrika Februari 14, vyombo vya habari kote duniani, wataalamu, serikali na hata Shirika la Afya Duniani wametabiri kutokea kwa janga katika bara hilo.
Ingawa wataalam wanasema kwamba ni mapema mno kudai kupata ushindi, 'janga hilo linalotarajiwa' limetabiriwa na John Nkengasong, mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika, bado halijatokea.
Huku Ulaya ikishuhudiwa zaidi ya watu milioni 1.5 waliothibitishwa kuathirika na virusi vya corona, Marekani idadi hiyo imepita milioni 1.3 huku Amerika Kusini ikikaribia 250,000, hadi kufikia sasa idadi ya walioambukizwa na virusi vya corona katika bara la Afrika imefikia 5 5, 000.
Idadi ndogo ya wanaokufa ndio jambo linaloshangaza zaidi: Hadi kufikia Mei 8, eneo hilo lilikuwa limesajili zaidi ya vifo 2,000 pekee ikiwa ni idadi ndogo mno ikilinganishwa na mabara mengine au hata ikilinganishwa na mji kama New York, ambako idadi ya waliokufa imefikia 20,000.
Idadi hiyo inatia moyo hasa ukizingatia kwamba Afrika ni ya pili kwa idadi ya watu duniani ambayo ni bilioni 1.2.
Lakini nini kinaweza kuwa siri ya idadi ndogo ya vifo Afrika wakati wa janga la virusi vya corona na kwa nini hata idadi ya wanaothibitishwa kupata ugonjwa wa Covid -19 iko chini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbinu mbalimbali
Nchi za Afrika zilizoathirika zaidi Afrika Kusini ambapo watu 10. 015 wamethibitishwa kuambukizwa, Misri watu 9,400, Morocco watu 6,063 na Algeria ikirekodi watu 5,723 (kufikia Mei 11).
Kwa pamoja, mataifa hayo manne yanasimamia karibu asilimia 50 ya maambukizi yote barani Afrika. Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba hilo linatokana na mfumo mbovu wa afya ambapo ni watu kidogo tu wanaopimwa na kutambuliwa kama wameambukizwa ugonjwa wa covid-19, kwasababu ya ukosefu wa raslimali.
Lakini wengine wametilia maanani mabo mengine kuanzia idadi ya watu kwa jumla hadi wale wanaosafiri kutoka sehemu moja mpaka nyengine.
Anne Soy, naibu mhariri wa BBC Africa anaelezea kwamba kuna mbinu mbalimbali zinazochukuliwa katika kukabiliana na janga la virusi vya corona Afrika, ukizungumzia mataifa 53 barani humo ambayo yamethibitisha kupata maambukizi na kuchukua mikakati mbalimbali
"Kuna nchi ambazo zimechukua hatua za dharura tangu wanzo na kwengine ambapo idadi ya wanaopata maambukizi imeendelea kuongezeka, hata hivyo, kuna nchi ambazo bado hazijakubali kwamba yanayotoea na hazichukui hatua za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo, nchi kama Tanzania," amesema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Tanzania John Magufuli ni miongoni mwa viongozi wachache duniani wanaendelea kuwa na mashaka juu ya virusi hivyo.
Wiki iliyopita, alihoji usahihi wa vipimo vya ugonjwa covid-19 na kumfuta kazi mkuu wa maabara ya taida aliyesimamia vipimo vilivyofanywa akidai kwamba kuna njama fulani.
Awali, Magufuli aliwataka raia wa Tanzanian kuomba kwa minajili ya virusi vya corona na serikali yake haitoi taarifa za kila siku kuhusu hali ya ugonjwa huo ilivyo nchini humo.
Kuchukuliwa kwa hatua kwa muda stahiki
Licha ya matukio kidogo, nchi nyingi za Afrika zimechukua hatua "kwa haraka zaidi kuliko wengine duniani," anasema Soy.
" Wamechukua hatua mapema sana nchi ya kwanza ikiwa Rwanda. Ikaamua kuchukua hatua ya kusalia ndani ikiwa na watu 20 tu waliothibitishwa kuambukizwa. Pia walisitisha ndege zote za kimataifa kutua nchini mwao, " anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Afrika Kusini, nchi ya Afrika ambayo hadi sasa ndio yenye idadi kubwa ya walioambukizwa virusi, tangu Machi 27, imekuwa ikitekeleza moja ya sheria kali ambayo inakataza ndege zote za kimataifa kuingia nchini humo na pia uuzaji wa pombe na sigara umepigwa marufuku.
Kwasababu ya kudorora kwa uchumi wa taifa la Afrika Kusini, nchi hiyo imeanza kulegeza baadhi ya masharti kuanzia wiki jana.
Tajriba ya majanga mengine
Ingawa janga la virusi vya corona ndio janga kubwa la afya kukumba kizazi cha sasa, sio la kwanza. Hasa kwa Afrika bara ambalo limekumbana na majanga mengine kama vile malaria, kifua kikuu, ugonjwa wa kipindupindi, Ukimwi na Ebola.
Magonjwa yote hayo yamesababisha idadi kubwa ya vifo lakini pia wanasayansi wa Afrika na jamii ya kimatibabu wamelazimika kuja na uvumbuzi mpya.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Watu wa Afrika wamezoea katika suala la kuchukua hatua kwa haraka na kutumia wale wanaojitolea. Nafikiri hilo limewezesha kusambaza taarifa kwa haraka ya kuzia ugonjwa huo na kuanza kuufanyia kazi, " Karl Blanchet, mtalaamu wa afya duniani, ameiambia BBC World.
Mlipuko wa hivi karibuni wa janga la Ebola ulikumba Afrika Magharibi kati ya 2014 na 2016 na kusababisha maafa makubwa katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 11,000.
Ingawa WHO imetangaza kutamatisha utoaji wa huduma za dharura za afya katika eneo hilo Machi 2016, mamlaka bado ziko katika hali ya tahadhari katika baadhi ya nchi zilizoathirika zaidi na mlipuko huo.
"Ebola lilikuwa tatizo ambalo liliendelea kushuhudiwa hata kipindi ugonjwa wa Covid-19 unatangazwa kama janga.
Hiyo inamaanisha kwamba baadhi ya nchi za Afrika tayari zilikuwa zimeweka mikakati ya kuchunguza wanaoingia katika nchi zao kupitia viwanja vya ndege,
Maafisa wa afya wa umma na vipimo joto vya mbali yatari walikuwepo katika viwanja vya ndege, "Soy anaelezea.
Mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi pia ulifunza Afrika umuhimu wa kutambua na kubaini waathirika kwa haraka na kutibu wale waliothibitishwa kuabukizwa na pia namna ya kujitenga, kulingana n a mwanahabari huyo wa BBC.
"Kwasababu ya janga hilo, watu waliacha hata kusalimiana kwa mkono Afrika magharibi nan chi ya Kidemokrasia ya Cogo. Pia walihakikisha watu wanakuwa na ufahamu wa ugonjwa huo," ameongeza.
Bara ambalo halitangamano sana kimiji

Chanzo cha picha, Getty Images
Frederique Jacquerioz, mtaalamu wa afya Afrika kutoka timu ya madaktari inayotoa msaada wa kibinadamu kwa nchi za kitropiki katika Chuo Kikuu cha Hospitali huko Geneva, Uswizi, anakadiria kwamba jengine ambalo huenda limechangia Afrika kutoathirika sana na janga la corona ni usafiri wa chini kati ya nchi za bara hilo na pande nyengine ya dunia.
"Mwathirika wa kwanza kuthibitishwa Afrika ilikuwa ni vijana, raia wa Afrika au Ulaya ambao walikuwa wamesafiri nje ya nchi na kurejea Afrika na kuleta virusi hivyo, " daktarin huyo ameiambia BBC Mundo.
Katika dunia hii ya utandawazi, hiyo ilikuwa moja ya sababu iliyochangia usambaaji wa virusi hivyo Ulaya, ambapo makundi ya vijana hutumia muda wao mwingi wa wikendi wakiwa wamesafiri katika miji mingine. Pengine Afrika, usafiri wa miji mbalimbali kati ya nchi sio sana, "aliongeza
Dhana ya kuathirika kwa kiasi kidogo kwasababu ya utandawazi inaungwa mkono na wataalamu wengine.
Blanchet, mkurugenzi wa Cerah, anatoa mfano wan chi tatu ambazo hadi kufikia sasa zimeathirika vibaya na virusi hivyo: Afrika Kusini, Misri na Algeria.
"Ni mataifa ambayo ndege nyingi zenye kuunganisha usafiri wake hadi China hutua katika nchi hizo. Isipokuwa Ethiopia, ambayo ingawa haipo kwenye kundi hilo, ina safari za ndege za moja kwa moja hadi nchi hiyo ya bara la Asia.
Lakini haijaathirika vibaya na janga la virusi vya corona. Hilo bado ni vigumu kuchanganuliwa, "anasema.
Je idadi ya raia waliowengi ina mchango wowote?

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya watu Afrika ni jengine ambalo huenda limesaidia kwa kutokuwa na idadi kubwa ya waliokufa katika eneo hilo: Afrika ni bara ambalo idadi kubwa ya watu ni vijana ikilinganishwa na kwengineko duniani.
Blanchet anaunga mkono hilo na kusema kwa mfano: "umri wastani nchini Kenya ni miaka 19.7, ilihali Ulaya ni miaka 40."
Wakati Anne Soy anatambua kwamba hilo huenda likawa miongoni mwa sababu, anaonya kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha dhana hiyo.
"Huenda ikawa moja ya mambo yanayopendelea Afrika, lakiniw akati huohuo, kuna idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo, wenye mfumo dhaifu wa kinga ikilinganishwa na wengine duniani jambo ambalo linawafanya kuwa katika hatari zaidi.
"Je hilo lina maanisha kwamba huenda idadi kubwa ya watoto Afrika ikaathirika kwa ugonjwa wa Covid-19?"Anauliza.
Hatari iliyopo kwa bara hilo

Chanzo cha picha, Getty Images
Ijumaa, Shirika la Afya Dunian-WHO, limeonya kwamba virusi vya corona huenda vikaathiri Afrika taratibu na kuuwa karibia watu 190, 000 katika kipindi cha miezi 12 ijayo.
Tahadhari hiyo inawadia ikiwa ni mwezi mmoja baada ya shirika hilo kukadiria kuwa mlipuko huo huenda ukaambukiza watu milioni 10 barani humo ndani ya kipindi cha miezi sita.
Utafiti mpya uliochapishwa wiki hii na WHO unatabiri kuwa kati ya watu milioni 29 na 44 huenda wakapata maambukizi mwaka wa kwanza wa janga la Covid-19 ikiwa hatua za kuudhibiti zitashindwa.
Wachambuzi mbalimbali wanasisitiza kwamba athari ya janga la corona kutategemea na hatua zitakazochukuliwa na serikali.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Afrika, Stephen Karingi, ameliambia gazeti la Uingereza la The Guardian itambulike kwamba viongozi wa Afrika wamechukua hatua nyingi kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona.













