Virusi vya corona: Je msaada wa Jack Ma Afrika una umuhimu gani katika kupambana na janga la corona?

Chanzo cha picha, Reuters
Huku mlipuko wa virusi vya corona ukiendelea kuathiri sekta zote duniani, mataifa mengi yameshindwa kupata jibu la kukabiliana na janga hilo.
Kufikia tarehe 6 Mwezi Aprili zaidi ya watu 1,275, 599 walithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo huku takriban 69 499 wakiripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo hatari kote duniani.
Kufkia tarehe 11 mwezi Machi , shirika la afya Duniani WHO lilitangaza rasmi virusi hivyo kuwa janga.
Wakati wa kuzuka kwa mlipuko huo Afrika haikutajwa miongoni mwa bara ambayo ugonjwa huo umeenea , lakini punde si punde mara tu mambo yakaanza kubadilika kwa kasi.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita idadi ya mataifa yalioathirika na virusi hivyo barani Afrika iliongezeka kutoka mataifa 9 hadi 41.
Na huku watu wakiendelea kusafiri, itachukua muda mchache tu kabla ya ugonjwa huo kutangazwa katika mataifa yote 54 katika bara hili.
Hatahivyo cha kutia wasiwasi ni kwamba idadi ya watu katika bara hili mbali na mifumo yake ya kiafya inaliweka tofauti na mabara mengine ambayo yamekabiliwa na virusi hicho vya Covid-19 kufikia sasa
Kwanza hali yake ya kieneo ipo tofauti na ile ya maeneo mengine duniani. Umri wa wastani wa watu wake bilioni 1.3 ni miaka 19.7. Kinyume na ilivyo nchini China ambapo ni miaka 38.4 huku ule wa barani Ulaya ukiwa miaka 43.1.

Suala la pili ni lishe duni, ugonjwa wa seli mundu, malaria, HIV/Aids na Kifua Kikuu.
Suala la jingine ni umasikini mkubwa uliopo miongoni mwa wakaazi wengi wa bara hili.
Ni kutokana na sababu kama hizo ndiposa baadhi ya watu matajiri duniani wamekuwa wakihofia jinsi bara hili lenye umasikini litamudu kukabiliana na mlipuko huo ambao umeyaadhibu baadhi ya mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ikiwemo China na Marekani.
Hofu hiyo imevutia wahisani kama vile mtu tajiri zaidi barani China Jack Ma ambaye amejitolea kwa hali na mali kulisadia bara hili.
Mmiliki huyo wa kampuni ya Alibaba nchini China amesema atalipatia bara hili lenye mataifa 54 Afrika mashine 500 za kuwasaidia wagonjwa kupumua, nguo laki mbili za wauguzi, na barakoa laki mbili , vifaa laki mbili vya kupima joto mbali na glavu lakini tano.
Hatua hiyo inajiri siku chache tu baada ya kuyaahidi matifa ya Afrika kwamba atayafadhili na vifaa vya kupima vurusi vya corona mbali na barakoa, ahadi ambayo alitimiza hivi majuzi.
Katika ahadi hiyo kila taifa lilipokea vifaa 20,000 vya kupima virusi vya corona , barakoa 100.000 na magwanda 10,000 ya madaktari na wauguzi.

Chanzo cha picha, SIMON MAINA
Lakini Je ufadhili huu una maana gani kwa bara Afrika?
1.Vifaa hivyo vitasaidia katika baadhi ya matiafa ya Afrika ambayo hayana uwezo kuanzisha juhudi za kuwapima na kuwaweka karantini raia wake ambao watapatikana na virusi hivyo. Hatua hiyo itasaidia katika kuzuia maambukizi kwa kiwango kikubwa.
2.Vitawasaidia madaktari ambao wengi wao wamekuwa wakiambukizwa virusi hivyo kutokana na ukosefu wa vifaa katika mataifa mengine kujitokeza na kukabiliana na janga hilo moja kwa moja bila hofu ya maambukizi.
3.Vifaa kama vile vya kuwasaidia waathiriwa kupumua ambavyo vimetajwa kuwa bei ghali zaidi vitasaidia kuokoa maisha ya wengi barani Afrika
4.Vilevile hatua hiyo itayapunguzia mzigo mkubwa mataifa ya Afrika ambayo mbali na kwamba mlipuko huo unayaathitiri yanakabiliwa na tatizo jingine la kulipa madeni, kukabiliana na umaskini mbali na magonjwa mengine kama vile malaria na ukimwi.
5.Vilevile vifaa hivyo vitazidi kuimarisha uhusiano kati ya mfanya biashara huyo mkubwa barani Afrika na taifa la China kwa jumla. Hii italikumbusha bara la Afrika kuhusu usaidizi ambao limekuwa likipata kutoka China na watu wake. Hatua hii itayafanya mataifa ya Afrika kuzidi kuelekea China kwa usaidizi badala ya Marekani na Ulaya ambaye amekuwa mshirika wake wa siku nyingi.
John Nkegasong ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa Africa CDC alisema kwamba ufadhili huo ni ishara kubwa ya ushirikiano ambao ulimwengu unahitaji wakati huu muhimu.

Chanzo cha picha, Twitter
''Tunakabiliwa hali ya kibinaadamu, hali ya kiuchumi mbali na ile ya kiusalama katika bara na Afrka CDC inapongeza mpango huo wa wakfu wa Alibaba na Jack Ma''.
Vifaa hivyo vitasambazwa barani Afrika kupitia ushirikiano wa Jack Ma na kampuni ya ndege ya Ethiopia Airlines kupitia waziri mkuu wa taifa hilo Abiy Ahmed.
Jack Ma aliandika katika kurasa wake wa Twitter kuwa mataifa ya Afrika yanaweza kuwa mbele zaidi katika kukabiliana na virusi vya corona.
Alisema kuwa inawezekana watu kujiandaa kukabiliana na corona hatua moja mbele.
Katika barua yake bilionea huyo alisema kuwa haiwezekani kwa jambo hili kupuuzia athari ambayo inaweza kutokea Afrika, katika mataifa ambayo yana watu zaidi ya bilioni 1.3.
Alisema kuwa wataanza kufanya kazi na taasisi za afya mapema iwezekanavyo.
Vipimo milioni 1.1 , vya kupimia corona, mask milioni 6, na vifaa 60,000 vya kujikinga viliwasili katika mji mkuu wa Addis Ababa, Ethiopia.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali ndie alisimamia usambazaji wake katika mataifa ya Afrika.














