Coronavirus: Je dunia imepata funzo gani kutokana na mlipuko wa Ebola DRC?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni miezi miwili imepita bila kuripotiwa kwa kisa cha Ebola katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Licha ya kwamba mlipuko huo haukuenea katika mataifa jirani ya Uganda au Kenya katika mataifa mengine ulisababisha hofu duniani na sekta ya afya ya umma.
Lakini tatizo kubwa ni dunia imejifunza vipi kukabiliana na milipuko ya awali ukiwemo ule wa Ebola?

Chanzo cha picha, Alamy
Kulingana na wataalamu mbali mbali wa magonjwa yanayoambukiza walioshughulikia mlipuko wa Ebola DRC yafuatayo ni baadhi ya mafunzo ambayo dunia inapaswa kujifunza ambayo yanaweza kutumiwa katika milipuko mingine kama coronavirus.
Maandalizi ya kijamii
Iwe ni Ebola au milipuko mingine kama coronavirus, mafua , njia pekee iliyothibitishwa ni utaratibu wa shughuli za udhibiti mlipuko kuanzia idara za afya , viongozi waliochaguliwa , mashirika yasiyo ya kiserikali kama madaktari wasio na mpaka na Shirika la Afya Duniani
Maandalizi ya kukabili mlipuko yanapaswa kuanza katika ngazi za utawala: ''Utafiti wetu umeonyesha kuwa kuhusishwa kwa viongozi wa kijamii ,watoaji wa huduma za afya, watoaji tiba za kitamaduni na wagonjwa ni muhimu katika kujenga imani miongoni mwa jamii juu ya udhibiti wa mlipuko.
Hii inakuwa na ufanisi wa kweli hususan katika maeneo yenye watu ambao hawana elimu.
Kuwasiliana na waliokutana na wagonjwa wa awali, kuwafuatilia na kuwapatia chanjo watu wanaoishi katika maeneo maskini, mizozo na ukosefu wa usalama'', anasema Philip A.
Lederer ni Profesa katika Chuo Kikuu cha Boston chuo cha Udaktari na magonjwa yanayoambukiza ambaye pia ni Daktari katika Kituo cha tiba cha Boston.

Chanzo cha picha, AFP
Uongozi wa nchi
Uongozi wa DRC unawajibu wa kuwekeza katika hospitali na vituo vya afya katika nchi husika ili kuviwezesh akudhibiti maambukizi ya virusi kama Ebola na coronavirus.
Ni muhimu kuelewa kuwa hatuwezi kuzuwia utangamano baina ya binadamu na wanyama kwa hivyo huenda tusiweze kuzuwia maambukizi kama Ebola, coronavirus na mengine yanayotoka kwa wanyama lakini la muhimu ni kuhakikisha huduma za afya zinawafikia walengwa salama na hilo linapaswa kuwa jukumu la serikali, kulingana na baadhi ya wataalamu wa magonjwa ya maambukizi
Katika uongozi wa dunia
Katika ngazi ya Dunia WHO imejifunza na imefanya kazi nzuri chini ya uongozi wa Mkurugenzi wake Mkuu Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Shirika hilo limeongoza kwa haraka na mapema juhudi za kutoa ushauri na njia za udhibiti wa kusambaa kwa maambukizi ya coronavirus.
Hali kadhalika limeongoza katika kutoa muongozo na ufuatiliaji wa juhudui za kupata chanjo ya Coronavirus.
''Swali kubwa ni lini dunia itawekeza sio tu katika watu na matibabu , bali katika kuwezesha vifaa vya tiba vinawafikia walengwa, anasema Philip A. Leader'', na kuongeza kuwa kuingia na kutoka maeneo ya vijijini kusambaza huduma za afya linapaswa kuwa jambo rahisi
Mafunzo au semina kwa watoaji huduma za afya
Wataalamu wa magonjwa ya milipuko wanapaswa kuwezeshwa kutoa huduma za mlipuko na pia vituo vianzishwe katika maeneo mbali mbali hususan Afrika juu ya huduma za milipuko.
Wataalamu wa magonjwa haya wanahitajika kufanya kazi kwa ushirikiano na nchi nyingine jirani, mawasiliano, usalama, kuimarishwa kwa maabara na utambuzi wa tamaduni husika ili kuweza kuwasiliana nazo kuhusu milipuko.
Hali ilivyo kwa sasa kuhusu coronavirus DRC
Kitongoji kimoja katika mji mkuu Kinshasa, kitakua katika amri ya kutotoka nje kwa muda wa wiki mbili kuanzia Jumatatu.
Eneo la Gombe linaonekana kama ndio kitovu cha taifa cha coronavirus na ndiko wengi wa watu wanaotoka nje ya nchi wanaishi.
Ni wafanyakazi wa afya pekee watakaoruhusiwa kutembea.
Makampuni muhimu ya serikali na baadhi ya bidhaa binafsi pia zitaruhusiwa kuendelea wakati wa amri ya kutotoka nje. Gavana wa Kinshasa Gentini Ngobila alitoa tangazo hilo Alhamisi jioni.
Wiki iliopita , alisitisha uamuzi wake wa kuliweka jiji la Kinshasa chini ya amri ya kutotoka nje kabisa kwa wakazi wake kwa kuhofia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.
Wengi wa wakazi wa mji huo mkuu wanahisi kuwa amri ya kutotoka nje katika manispaa moja kati ya 24 za mji huo haina ufanisi katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona.
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeripoti visa 134 vya corona hadi leo, pamoja na vifo 13.













