Peter Mutharika: Mahakama yafutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi

Rais Peter Muthatrika

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais Peter Muthatrika wa Malawi wakati wa uchaguzi wa 2019

Mahakama ya kikatiba imefutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi Peter Mutharika uliofanyika mwezi Mei 2019, Kulingana na mtandao wa gazeti la kibinafsi la Nyasa Times.

''Tumegundua kwamba kulikuwa na makosa mengi katika uchaguzi huo hali ya kwamba maadili ya matokeo hayo yaliingiliwa'', mahakama hiyo yenye majaji watatu ilisema.

Mahakama ilitangaza kwamba matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa na makosa na kwamba hayakustahili na wakati huohuo ikakubaliana na walalamishi kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu mkubwa, ulisema mtandao huo.

Katika uchaguzi huo wa mwezi Mei mwaka 2019 , Mutharika alitangazwa kuwa mshindi akiwa na asilimia 38 ya kura zote zilizopigwa, Lazarus Chakwera alikuwa wa pili na asilimia 35 naye aliyekuwa wakati mmoja makamu wa rais Saulos Chilima akiwa wa tatu na asilimia 20 ya kura zilizopigwa.

Chakwera na Chilima waliwasilisha kesi dhidi ya uchaguzi wa Mutharika na kuongoza maandamano ya kutaka maafisa wa tume ya uchaguzi nchini humo kujiuzulu.

Runinga ya taifa haikurusha matangazo ya moja kwa moja ya mambo yaliokuwa yakiendelea katika mahakama hiyo.

Uchaguzi mpya utafanyika katika kipindi cha siku 150, mahakama hiyo ilisema katika uamuzi wake, ikisisitiza mwishowe kwamba inatumai uamuzi huo hautaliharibu taifa hilo.

Katika kesi yao Chakwera na Chilima walipinga matokeo ya uchaguzi huo wakisema makosa yaliofanyika yaliathiri zaidi ya kura milioni 1.4 kati ya kura milioni 5.1 zilizopigwa.

Hatahivyo uamuzi huo wa siku ya Jumatatu unaweza kupingwa katika mahakama ya kilele.

Lazarus Chakwera (kushoto) na Saulos Chilima (kati) walikuwa wakichuana na rais Mutharika (kulia)

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Lazarus Chakwera (kushoto) na Saulos Chilima (kati) walikuwa wakichuana na rais Mutharika (kulia)

Kulingana na The New York Times mawakili waliokuwa wakimwakilisha rais walikataa kujibu maswali na kuondoka kwa haraka katika eneo la mahakama hiyo.

Mwanasheria mkuu , aliyekuwa akiwakilisha tume ya uchaguzi alisema kwamba watalazimika kutafuta ushauri kuhusu hatua watakazochukua.

Hali ya usalama iliimarishwa na raia kote nchini walikuwa wakifuatilia kwa hamu yaliokuwa yakiendelea katika Mahakama.

Majaji hao wa mahakama ya kikatiba walisema kwamba matokeo hayo yalionyesha kwamba hakuna aliyechaguliwa kwa wingi wa kura kulingana na katiba ya taifa hilo, ikiangazia ufafanuzi wa wingi wa kura na anayeongoza kwa kura.

Mahakama hiyo ililiagiza bunge kufanya kikao baada ya kipindi cha siku 21 ili kutoa sheria mpya itakayoongoza uchaguzi mpya.

Taifa la Malawi sasa ni la pili katika eneo la jangwa la sahara barani Afrika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais.

Mwaka 2017 mahakama ya kilele nchini Kenya ililishangaza taifa hilo baada ya kufutilia mbali uchagiuzi wa urais ikidai udanganyifu.

Rais Uhuru Kenyatta hatahivyo alishinda uchaguzi huo kwa urahisi baada ya kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga kususia uchaguzi wa marudio.

Tunazidi kukupasha.....