Usalama wa DRC uko vipi mwaka mmoja tangu Tshisekedi alipoingia madarakani?

Felix Tshisekedi raisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Felix Tshisekedi raisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Leo ni mwaka mwaka mmoja tangu kwa mara ya kwanza katika historia ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, raisi anayemaliza muda wake kumkabidhi madaraka kwa amani raisi aliyechaguliwa.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi ametimiza mwaka mmoja ofisini lakini ukosefu wa usalama ni moja wapo ya changamoto kubwa anayokabiliana nayo huku akijaribu kumaliza vurugu Mashariki mwa taifa hilo la Afrika ya kati, ambalo pia ni ahadi kuu ya wakati wa kampeni zake za uchaguzi.

Lakini je vikosi vya jeshi la taifa vinavyohusika kikamilifu katika vita dhidi ya kundi la waasi kutoka uganda la Allied Democratic Forces (ADF) huko Beni vimefanikiwa?

''Usalama mashariki ya DRC ni moja ya ahadi na jukumu kubwa la rais Felix Tshisekedi kutokana na makundi ya waasi hasa Lile la ADF kushambulia eneo hilo'', Mwandishi wa BBC, Byobe Malenga anaeleza.

Usalama Kivu Kaskazini

Eneo la Beni limekuwa likishuhudia matukio ya raia kuchinjwa kila uchao. ''Kama nilivyo ahidi wakati wa kuapishwa kwangu ni kwamba udhibiti wa amani katika maeneo ya Beni, Butembo katika mkoa wa kivu ya kaskazini na huko minembwe fizi katika kivu ya kusini dhidi ya makundi ya uasi katika eneo lote la nchi ni moja na itaendelea kuwa jukumu langu la kudumisha usalama katika nchi nzima. '', rais Felix Tshisekedi alisema hivyo wakati wa kampeni.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kuwa rais wa DRC, changamoto ya usalama eneo la mashariki bado ni suala nyeti na limekuwa likikumbwa na msururu wa mauaji ,vita pamoja na utekaji nyara wa mara kwa mara kutoka kwa waasi si tu kundi la MaiMai lakini kubwa ni limekuwa hili la waasi wa ADF.

Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa na operesheni kubwa ya kivita dhidi ya waasi hao wa ADF na hivi karibuni liliteka ngome kuu ya waasi hao ya Madina karibu na mji wa Beni lakini bado kuna changamoto nyingi pamoja na vifo vingi vya wanajeshi.

Mack Azukai msemaji wa jeshi la Beni amesema, ''Tangu tarehe 30 Oktoba mwaka jana, chini ya agizo la amiri jeshi mkuu rais wa nchi, tulianzisha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa ADF katika maeneo ya Beni. Tathimini kamili baada ya operesheni ya kudhibiti eneo la liva na mapobu bado inaendelea na tumedhibiti mji wa Madina ngome kubwa ya ADF ambao ni ushindi mkubwa zaidi ya waasi 40 wamefariki na viongozi wao 5 wameuawa pia tulipoteza askari jeshi zaidi ya 30 na silaha.''

Hata hivyo Azukai amesema operesheni zimekumbana na changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya raia kuunga mkono waasi, ''Katika eneo hilo la Beni wakati tunaanzisha vita dhidi ya waasi kuna changamoto kwani baadhi ya raia wa Maimai wamekuwa wakisaidia adui hadi kujipenyeza kwake. Nachukua fursa hii kutoa wito kwa watu hao raia wa Congo waachane na tabia hiyo na waje kutuunga mkono jeshi lao katika kazi wanayoifanya''.

Muasi wa Mai Mai

Chanzo cha picha, Getty Images

Hali ilivyo na hatma yake

Si tu mkoa wa kivu kaskazini ambao umekuwa na ukosefu wa usalama lakini pia katika mikoa ya Ituri na Kivu ya Kusini pamoja na mkoa wa Tanganyika ambapo kumekuwa na vurugu nyingi huku mashirika ya raia wakilalama kuwa serikali imeshindwa kulinda raia wake.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu na mashirika ya raia wanasema kuwa ikiwa serekali itafanikiwa kutokomeza mashambulizi katika maeneo hayo basi itakuwa ushindi mkubwa kwa Tshisekedi.

''Sisi kama wateteaji wa haki za kibiandamu, tuna majonzi makubwa sana kwasababu ya vifo vinavyotokea katika mji wa Beni, na wakati tunasaidia jeshi letu kupambana na kuvunja ngome zao, sisi tunafurahia zaidi na inaweza kuwa moja ya ushindi wa Rais Tshisekedi katika utawala wake.

''Raia na jeshi washikamane kwasababu wao ndiyo wanaweza kutambua kama adui ameingia sehemu fulani na kutoa siri kwa askari.'' amesema Bi. Batenji, mratibu wa shirika la wanawake la kutetea haki za Kibinadamu FFD.

Mtazamo wa wananchi

Licha ya jeshi kuchukua udhibiti katika maeneo mengi huko Beni dhidi ya waasi wa ADF lakini kwa wengine bado matumaini ya amani inaonekana kuwa madogo katika sehemu kubwa kutokana na wingi wa makundi ya uasi.

''Maoni yangu mimi kama raia wa Congo, vurugu wa usalama ulikuwa mwingi sana sehemu za Beni, Ituri na Butembo. Lakini amepembana na hali hiyo, pili ni elimu ya bure ya shule ya msingi na sekondari.''

''Maoni yangu bado suluhisho halijapatikana kwasababu maeneo mengine kuna fujo,''

''Ni mwaka mmoja na hatuwezi kutathmini kwa kipindi hiki, nchi ilikuwa chini sana.''