Waandishi Uganda wakamatwa kwa kupinga ukatili wa jeshi la polisi

Muda wa kusoma: Dakika 2

Waandishi wa habari wa Uganda wanashikiliwa na polisi kwa kuandamana kulaani unyanyasaji wanaofanyiwa na maafisa wa usalama.

Waandishi hao kutoka chama cha waandishi wa habari wa Uganda (UJA) wamesambaratishwa na polisi walipokuwa njiani kuelekea kwenye makao makuu ya jeshi la polisi nchini Uganda eneo la Naguru mjini Kampala kuelezea kero zao.

Kwasasa wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha kati katika mji mkuu Kampala.

Walikuwa wakiandamana kuuomba uongozi wa jeshi la polisi la Uganda kuwazuia maafisa wao tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili waandishi wa habari kokote wanakotumwa kukusanya habari za matukio ya ghasia na maandamano.

Walitaka pia askari polisi binafsi waliohusika katika ukatili dhidi yao wafunguliwe mashtaka kwa ukatili walioufanya na walipe gharama zote zilizotumiwa na waandishi wa habari waliojeruhiwa na vitendea kazi vyao walivyoharibu.

Unaweza pia kusoma:

Rais wa Muungano wa waandishi wa habari nchini humo Bwana Bashir Kazibwe ni mmoja wa waandishi wa habari ambao wamekamatwa na polisi.

Awali Bwana Kazibwe aliiambia BBC kuwa hatua ya maandamano ya waandishi wa habari imechukuliwa baada ya ukatili wa maafisa wa usalama dhidi yao kuonekana kukithiri.

''Hatua hii imechukuliwa baada ya wandishi habari kupigwa wakifanya kazi zao za kuripoti wakati wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere walipofanya maandamano ya kupinga nyongeza ya karo ya asilimia 15%.

Hii si mara ya kwanza wandishi habari kupigwa na walinda usalama, anasema mwandishi huyu wa habari ambaye hakutaka jina lake litajwe.

''Katika kipindi cha wiki mbili ambapo ghasia za wanafunzi zimedumu, wandishi habari walinyanyaswa kwa namna mbalimbali. Baadhi walikamatwa na kulazimishwa kufuta picha na video walizorekodi. Vitendo hivyo ndivyo wanahabari wanaelezea kuwa ni hila za polisi kuwakosesha kufanya kazi yao ya kupasha jamii habari kuhusu uhalisi wa mambo'', amesema.

Wiki iliyopita, waandishi wa habari kadhaa waliokuwa wakifuatilia taarifa ya maandamano ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini humo walilazwa hospitalini baada ya kupigwa kikatili na maafisa wa Uganda.