Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gerard Fernandez: Mtawa 'anayewapeleka' wafungwa kunyongwa
Mwaka 1981 mtawa wa kanisa Katoliki kutoka Singapore alianza kuandika barua kwa wafungwa wenzake wa kike waliohukumiwa kifo, mawasiliano ambayo yaliendelea kwa miaka saba.
Mtawa huyo alikuwa Gerard Fernandez na mfungwa Tan Mui Choo,ambaye ni mwanafunzi wake wa zamani ambaye alihukumiwa kifo kwa kuhusika na mauaji ya kikatili ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini.
Alimfahamu kama Catherine, kama "msichana mzuri na muadilifu" ambaye anatoka katika familia ya kidini na pia alisomea shule ya kikatoliki.
Tan, pamoja na mume wake Adrian Lim na hawara wake Hoe Kah Hong, walitekeleza mauaji ya kikatili dhidi ya watoto wawili.
"Alifanya makosa makubwa," alisema kwa utaratibu mtawa huyo mpole ambaye, sasa ana mika 81. "Nilisikitika sana niliposikia habari hizo kwa mara ya kwanza lakini nilijua lazima nikutane naye."
Kwa miaka kadhaa mtawa Gerard alimtembelea Tan gerezani, na wakati mwingine kuomba na wafungwa usiku kucha. Mchakato ambao anasema uliwaimarisha kiroho na kuelewa kiundani umuhimu wa kutubu dhambi.
"Nilikuwa hapo kumsaidia Catherine naye alijua kuwa naweza kusema ," alisema. "Nadhani hilo lilimfanya ajinasue kutoka katika jela ya mawazo."
Mtawa huyo alikuwa hapo hadi mwisho wa Novemba 25 mwaka 1988 - asubuhi ya kunyongwa kwa Tan.
"Kila mmoja ni muhimu kuliko kitu kibaya alichokifanya ,"mtawa alisema. "Haijalishi mtu amefanya dhambi gani, kila mmoja ana haki ya kufa kwa heshima."
Asubuhi yake ya mwisho, Tan alivalia nguo ya rangi ya samawati na viatu vilivyofanana na nguo yake. "Alikuwa mtulivu,"mtawa Gerard anakumbuka. Wanawake hao wawili walishikana mikono kwa mara ya mwisho kabla ya kutembea hadi eneo la kunyongwa .
Aliimba wimbo unaopendwa na Tan 'How Great Thou Art' alipoingia katika chumba cha kunyongwa.
"Nilimsikia akipanda ngazi na pia nilisikia wakati kamba zilipovutwa akinyongwa. Mlango ulifunguka na hapo nikajua kuwa Catherine ameenda."
Jela hilo lenye ulinzi mkali linapatikana eneo la kaskazini mashariki mwa Singapore mwendo mfupi kutoka uwanja wake mashuhuri wa ndege duniani.
Linatumiwa kuwazuilia wahalifu sugu nchini humo na wale waliohukumiwa kunyongwa.
Tan Mui Choo alikuwa mmoja wa wafungwa 18 ambao Sister Gerard Fernandez alitembea nao hadi katika eneo la kunyongwa.
"Hukumu ya kifo sio kitu ambacho mtu anakubali kwa urahisi," alisema.
"Inachukua muda kwa mtu kukubali hatma yao na kiuahakika ni hatua ya kuumiza sana."
Mtawa Gerard aliendelea kufanya kazi na wafungwa kwa miaka 40. Anaamini ni sehemu ya wito.
"Wafungwa waliohukumiwa kifo wanahitaji msaada wa kiakili, kihisia na kiroho," alisema.
"Nilitaka kuwasaidia ili wapate kuelewa kwamba kusamehe kunaponya, na kwamba baada ya hapo wataenda mahali pazuri."
'Nikimuona Mungu nitamuelezea juu yako'
Miaka mingi baadae mfungwa mmoja alimwambia mtawa Gerard baada ya kumuona kutoka kwenye seli yake. "Alisema uwepo wangu unamfariji,"anakumbuka.
Aliomba kumuona siku aliyokuwa ananyongwa.
Sister Gerard anachukulia wito wake kama "nafasi ya kipekee" yakutembea na mfungwa aliyehukumiwa kifo.
"Hatua ya mtu kukuelezea hisia zake za mwisho akiwa na huzuni na kuniruhusu kuwanae dakika za mwisho maishani mwake ni upendo na uaminifu wa hali ya juu," alisema.
Anakumbuka maneno yake ya mwisho: "Naenda kukutana na Mungu asubuhi na nikimuona, nitamwambia kila kitu juu yako."
Idara ya magereza nchini Singapore, ambayo inaendesha magereza 14 na vituo vya kurekebishia tabia, imesema ushauri ni "sehemu muhimu katika mchakato wa kuwarekebisha tabia wafungwa ili waweze kujumuika tena na jamii baada ya kumaliza vifungo vyao".
"Mtawa Gerard Fernandez amefanya kazi [na sisi] ya kujitolea kwa miaka 40," Msemaji aliiambia BBC. "Kujitolea kwake na bidii yake kumetugusa, na wengine wengi wanaojitolewa kusaidia wafungwa na familia zao."
Kwa wengi, hali ingelikuwa tofauti kabisa bila uwepo wa mtawa Gerard.
Mama wa mlanguzi wa dawa za kulevya ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema mtawa huyoalibadilisha maisha ya mtoto.
"Mtawa Gerard hamhukumu mtu wala kuchoshwa naye," alisema, akiongeza kuwa aliona mabadiliko makubwa katika mtazamo wa mwanawe. "alijikubali na kugeukia sala ya toba''.
Hukumu ya kifo inasalia kuwa suala lenye utata nchini Singapore.
Taifa hilo tajiri lililopo katika eneo la kusin mashariki mwa bara Asia linajivunia kuwa na viwango vya chini vya uhalifu .
Licha ya serikali kuidhinisha mabadiliko katikasheria ya hukumu ya kifo mwaka 2012 takwimu rasmi za magereza zinaonesha kuwa watu 13 waliuawa mwaka 2018-idadi ambayo ni ya juu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Kura ya maoni ya umma kuhusu hukumu hiyo pia zinaonesha watu wanaunga mkono kikamilifu sheria hiyo kali.
Shirika la kutetea haki la Human Rights Watch linapinga vikali hukumu ya kifo.
"Ni katili sana na inakiuka haki za kimataifa za binadamu," naibu mkurugenzi wa shirika hilo wa bara Asia, Phil Robertson alisema.