Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Rais Magufuli amtaka CAG Kichere kutii mihimili mingine
Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemtaka CAG mpya Charles Kichere kutojifanya mhimili, badala yake awe mtiifu kwa mihimili anapoagizwa kutekeleza majukumu.
Bwana Kichere na watumishi wengine walioteuliwa mwishoni mwa juma lililopita wameapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kichere anachukua nafasi ya Profesa Mussa Assad ambaye ameitumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano.
Kabla ya wadhifa huu mpya, Kichere alikuwa katibu tawala wa Mkoa wa Njombe.
Akizungumza baada ya kumuapisha, Raisi Magufuli amesema ofisi ya CAG si safi kama inavyofikiriwa.
''Usije ukaenda huko ukajifanya wewe ni mhimili, mihimili ni mitatu tu, na umeiona hapa, mahakama, kuna bunge na sisi wengine wa serikali na katika kiapo chako nilikuwa nakisikiliza nafasi yako ni mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa hiyo mwenye serikali yupo, kafanye kazi zako vizuri za ukaguzi, unapopewa maagizo na mihimili mingine kama bunge katekeleze, usibishane nao ukipewa maagizo na mhimili kama mahakama katekeleze, wewe ni mtumishi''. Alisema Raisi Magufuli.
Profesa Assad amesema nini?
Kuhusu jambo hili amesema ni vyema watu wengine wakilifafanua jambo hili watu wengine kuhusu hatua hiyo kisheria kuliko kulieleza yeye mwenyewe kwa kuwa linamuhusu moja kwa moja.
Bwana Assad amesema anatarajia leo kupatiwa barua yake rasmi kwa kuwa uteuzi ulifanyika mwishoni mwa juma na haikua wakati wa kazi, hivyo wataichanganua na
Kuhusu namna alivyopokea uamuzi huu ameiambia BBC kuwa alitegemea uwezekano wa kuwepo kwa uamuzi wa Dokta Magufuli.
''Jambo hili si la kisiasa ni jambo la kisheria, lakini nasema riziki anayo mwenyewe Mwenyezi Mungu na kwake haiishi kwa hiyo sikupata wasiwasi, kuna vitu chungumzima vya kufanya Inshallaah Mungu atatufanyia na kila kitu kitakwenda vizuri.'' alisema Profesa Assad.
Charles Kichere ni nani?
Alisomea elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na chuo kikuu cha Tumaini, mjini Dar Es Salaam.
Kichere aliwahi kuwa naibu kamishna mkuu wa TRA.
Mnamo tarehe 25 Machi mwaka 2017, aliteuliwa na rais Magufuli kuwa kamishna mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).
Aliipokea nafasi hiyo kutoka kwa Alphayo Kidata ambaye aliteuliwa wakati huo kuwa katibu mkuu ikulu Tanzania.
Charles Kichere alihudumu kama kamishna wa TRA kuanzia Machi 2017 hadi Juni mwaka huu 2019, wakati aliondoshwa katika mamlaka hiyo ya TRA, katika mageuzi ya rais Magufuli aliyotoa ikulu mjini Dar es Salaam kupitia taarifa rasmi ya mkurugenzi wa mawasiliano ya rais.
Kichere aliteuliwa badala yake kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Yuko kwenye bodi ya Benki ya CRDB Tanzania.
Zamani alikuwa mkaguzi mkuu wa shirika la Kitaifa la barabara, mweka hazina na pia mkaguzi mkuu wa hesabu katika kampuni ya majani chai ya Unilever nchini Kenya na Tanzania.
Siku ya Jumamosi taarifa kutoka Ikulu ya Tanzania na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Ikulu ya rais, ilisema kuwa walioteuliwa ni Mathias Kabunduguru ambaye sasa ndiye mtendaji mkuu wa mahakama ya Tanzania, akichukua nafasi ya Hussein Katanga aliyeteuliwa kuwa balozi.
Wengine walioteuliwa ni Godfrey Mweli kuwa naibu katibu mkuu Tamisemi anayeshughulikia elimu.
Kabla ya uteuzi huo Mweli alihudumu kama mkurugenzi wa mipango katika wizara ya katiba na Sheria.
Hashim Abdallah Komba naye ameteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Nachingwea. Kabla ya Uteuzi huo Komba Komba alikuwa akihudumu kama katibu tawala mkoa wa Iringa.
Anachukua nafasi ilioachwa na Rukia Muwango ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Vilevile kiongozi huyo wa taifa amemteua Hassan Abbas Rungwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nachingwea. Anachukua mahala pake bakari Mohammed Bakari ambaye ameondolewa na huenda akapatiwa kazi nyingine.