Xenophobia: Rais Cyril Ramaphosa atuma ujumbe maalum Tanzania kujadili uhalifu dhidi ya wageni Afrika kusini

Chanzo cha picha, AFP
Ujumbe maalum ulioteuliwa na Rais wa Afrika Kusini unazunguka katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Tanzania, kuwasilisha ujumbe kuhusu uwajibikaji wa Afrika kusini kwa uhalifu dhidi ya raia wa kigeni nchini humo.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ametuma ujumbe huo wa ngazi ya juu kama sehemu jitihada ya kuzihakikishia nchi za Afrika usalama wa raia wake baada ya mfululizo wa mashambulizi ya chuki dhidi ya raia wa kigeni.
Wajumbe maalum wanatarajiwa kufika nchini Tanzania, Ghana, Senegal, Zambia na DRC, kuzihakikishia serikali za nchi hizo kuwa raia wao wapo salama.
Tayari rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amekutana na ujumbe huo hapo jana katika ikulu mjini Abuja.

Chanzo cha picha, Presidency Nigeria
Katika mapokezi ya wageni hao kutoka Afrika kusini, Rais Buhari amesema: "Ukirudi katika matukio ya kihistoria, tulijitolea pakubwa kwa ajili ya Afrika kusini kuwa taifa huru... Uongozi wetu uliwajibika kwa azma hiyo. Tulijitolea, jambo ambalo vijana wa leo hawawezi kulitambua."
Ujumbe wake rais Ramaphosa unaoongozwa na aliyekuwa waziri wa nishati Afrika kusini, Jeff Radebe na unawajumuisha pia Balozi Kingsley Mmabolo na Dkt Khulu Mbatha na una jukumu la kuyahakikishia mataifa ya Afrika kuwa Afrika kusini inawajibikia maadili ya Umoja wa Afrika.
"Wajumbe hao maalum wataziarifu serikali za mataifa hayo ya Afrika kuhusu hatua ambazo serikali ya Afrika kusini imechukua kusitisha mashambulio na kuwawajibisha wahusika wa uhalifu huo," taarifa kutoka ofisi ya rais imeeleza.
Rais Cyril Ramaphosa amelaani vurugu hizo na kusema" hakuna maana kwa waafrika kusini kuwavamia wageni"
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Mashambulizi ya biashara zinazomilikiwa na wageni nchini Afrika Kusini zimepokelewa kwa hasira kali na wageni ambao wanahisi wanalengwa na kuonewa.
Baadhi ya serikali za mataifa ya kiafrika zimeeleza hofu juu ya raia wake dhidi ya chuki hiyo na kutoa tahadhari juu ya vurugu hizo.
Takriban wiki moja iliyopita mamia ya watu wameonekana wakikimbia na kupora mali za watu katika eneo lenye shughuli za kibiashara na kuchoma moto maduka yanayoaminiwa kumilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika.
Ghasia hizo zilianzia katika eneo la Jeppestown, lililopo katika wilaya ya kati yenye shughuli za biashara.
Lakini zilisambaa hadi kwenye maeneo mengine kama vile Denver, Malvern, Turffontein, Tembisa na maeneo mengine ya vitongoji vya jiji la Johansburg.
Afrika kusini imeorodheshwa kuwa nchi yenye idadi kubwa ya mauaji duniani.













