Ajali Morogoro: Je waathirika wa mkasa wa lori Tanzania ni akina nani?

- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
Ajali ya kasa wa Lori la mafuta lililopuka na kusababisha vifo na majeruhi nchini Tanzania imeacha kumbukumbu ambazo hazita sahaulika kwa ndugu jamaa na marafikiwa wa waathiriwa wa mkasa huo.
Idadi ya Watu waliokufa kutokana mkasa wa moto uliotokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro, Mashariki mwa Tanzania Jumamosi ni watu zaidi ya 71 na 60 kati yao tayari wamezikwa katika eneo la makaburi.

Miongoni mwa waaathiriwa walikuwa ni vijana, wakiwemo madereva wa pikipiki au bodaboda ambao walikimbilia kuchota mafuta wakati lori la mafuta lilipoanguka na baadae mafuta kuwakaa moto.

Walioathirika waliwa ni watu wa aina gani?
Magreti Saimon Emmanuel amempoteza mtoto wake wa kiume Shukuru katika mkasa huo: ''Nimempoteza mwanangu Shukuru, alikuwa ni dereva wa bodaboda...tunasikitika sana kwasababu ya kumpoteza mtoto wetu...ameacha mke mmoja na mtoto mmoja tunaomba serikali itusaidie''. Amesema Bi Magreti mwenye uso uliojaa huzuni ameiambia BBC.
Miongoni mwa walionusurika na mkasa wa mlipuko wa Lori, ni Batholomeo .Anasema ajali ilikuwa mbaya na imemuathiri kiakili:
''Ajali ni mbaya na wengi waliokufa ni vijana, wanawake sio wengi sana...wengi ni wanaume...yaani nguvu kazi... Halafu ni kama lika langu... Mimi nimeumia hapa kwenye goti, lakini kwa sasa nasikia afadhali ''

''Yaani hapa maisha hayajarudi kama mwanzo...ni simanzi, yaani kila mtu akipita hapa haamini...yaani ajali imetokea hapa...mimi. Usiku wala sikulala ...Nina marafiki zangu hapa walikuwa wanaishi sehemu ya Msamvu..., sikulala ...Nilikuwa yaani kama naweweseka hivi, mimi mwenyewe yaani katika kichwa nasikia siko vizuri.'' Anakumbuka Bathomeo ambaye anasema ni vigumu kusahau aliyoyashuhudia katika mkasa huo.
Ni vigumu kwa baadhi kuamini kuwa hawatawaona tena wapendwa wao kutokana na mkasa wa Jumamosi na kwa sasa kumbukumbu ya wapendwa wao iliyosalia ni eneo la mkasa. Wandishi wa BBC walioshuhudia eneo la ajali baada ya tukio Jumatatu walishuhudia makundi ya watu waliokuja kutafakari mkasa huo kwenye eneo tukio.

Bi Beatrice Makoe anafanyakazi karibu na eneo ulipotokea mkasa wa moto anasema mambo yamebadilika baada ya mkasa.'' maisha yamekuwa magumu, tulishazowea purukushani za wat, mtaa umepoa, sehemu zote za biashara zimefungwa, kila nyumba ni msiba. Kwa kiasi kikubwa Wengi waliokufa ni mabodaboda na hao mabodaboda huwa tunawatumia wanatuletea wateja dukani kwetu ...Kwa kweli inauma kiukweli'', amesema Beatrice ambaye anasema anaogopa kupita eneo la tukio la mkasa.

Shughuli ya kuchimba makaburi imeendelea Jumatatu, huku ndugu na jamaa wa waathiriwa wakifika makaburini walau kuweka shada za maua kuwaenzi wapendwa wao. Orodha rasmi ya watu waliojeruhiwa kwenye mkasa imetolewa, na kinachobaini kwenye orodha hii, wengi wa waathiriwa ni wanaume, na vijana waliokuwa wakijaribu kutafuta riziki ya maisha kutokana na mafuta yaliyokuwa yakitiririka kwenye tenki ya lori lilioanguka na kusababisha mkasa mkubwa.

Miili ya watu 60 wa kwanza imezikwa kwenye vilima vya Kola mjini Morogoro
Waziri mkuu wa Kassim Majaliwa ameagiza mnara ujengwe kwenye eneo la makaburi hayo, kama ishara ya kumbukumbu ya vifo vya Watanzania waliokufa kwenye mkasa huo.
Kutokana na mkasa huu mkubwa pia rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo kuwakumbuka waathiriwa wa mkasa wa Morogoro.
Hata hivyo kwa wakazi wa eneo la Msamvu, hususan ndugu jamaa na marafiki wa waathiriwa mkasa huu utasalia kuwa kumbukumbu wanayoishi nayo akilini kila siku maishani mwao.














