Katie alikuwa mraibu wa dawa za kuondoa maumivu tangu akiwa na miaka 16

Maumivu

Chanzo cha picha, Thomas Dowse

Katie 26, anasema: usiku mmoja mwaka jana, nililala kitandani pembeni ya rafiki yangu wa kiume, nikisubiri alale usingizi. Alipolala, nilinyakua begi langu lililoluwa pembeni yake, na kuanza kupekua haraka haraka kwenye makasha matupu ya vidonge nikitafuta kasha jipya ya dawa kali za kuondoa maumivu co-codamol.

Kelele nilizokuwa ninazitoa wakati natafuta dawa zilimuamsha akaniangalia. ''ulimeza dawa kabla ya kulala. Kwa nini unahitaji dawa zaidi'' aliuliza.

''Nina maumivu. Endelea kulala.'' Niligeuka nikiendelea kupekua mkoba.

''Katie, ninaogopa kuna siku utameza dawa nyingi na hautaamka tena.''

Maneno yake yalikuwa kama kofi usoni mwangu.

Yalianza nilipokuwa na miaka 16 nilikimbizwa hospitali madaktari wakidhani nina shida kwenye kidole tumbo (appendicitis). Nilikuwa natazama televisheni, mara, nikahisi maumivu makali upande wa kulia mwa tumbo langu, kama vile nilipigwa teke tumboni.

Nikafanyiwa upasuaji kuondoa appendix lakini ikabainika maumivu hayo makali hayakuwa kwa sababu ya appendicitis. Madaktari wakaona uvimbe kwenye Ovari kisha waliondoa uvimbe huo kwa upasuaji.

Siku iliyofuata, niliandikiwa kutumia vidonge vya co-codamol ambazo niliambiwa kuwa zitaondoa maumivu.

Miaka tisa baadae, maisha yangu yanasonga kwa kutumia vidonge hivyo.

Mamlaka za huduma ya afya nchini Uingereza zinasema inawezekana kuwa mraibu wa co-codamol lakini aghalabu hali hutokea hivyo kama unatumia dawa hizo kwa ushauri wa madaktari.

Baada ya upasuaji, nilijihisi nafuu. Tayari nilishatolewa uvimbe, bila shaka uvimbe uliondoka kwa siku chache .

Baada ya siku chache kupita nilipata tena maumivu, baba akanipeleka hospitali. Niliandikiwa co-codamol zaidi na kisha nikaambia nijitazamie maumivu yangu.

Madaktari kuwapa dawa kali za kuondoa maumivu wagonjwa, kunachangia changamoto za kiafya, katika nchi kama Marekani na Canada, Uingereza na Wales pia zikitajwa na ripoti ya hivi karibuni ya Maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi (OECD). Uingereza sasa ni ya tatu kwa kuwepo kwa matumizi makubwa ya dawa zenye kusababisha uraibu.

Mwaka jana, uchunguzi wa BBC ulibaini kuwa madaktari nchini Uingereza walitoa ruhusa kutumiwa kwa dawa karibu milioni 24 mwaka 2017,ongezeko la milioni 10 tangu mwaka 2007, mamlaka nchini humo zikishutumiwa kuwatengeneza waraibu wa dawa.

Idadi ya vifo na visa vya kunywa dawa zilizozidi kipimo vinaongezeka, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na gazeti la Sunday Times. Uchunguzi umesema kuwa watu watano hufa kila siku nchini Uingereza na Wales kutokana na matumizi ya dawa yaliyokithiri na kusababisha uraibu.

Maumivu

Chanzo cha picha, Thomas Dowse

Mwanzoni nilimeza dozi ya co-codamol. Lakini kabla ya muda mrefu kupita, nikagundua kuwa nimekuwa mraibu wa dawa hizo. Nilikuwa nina hamu ya kumeza dawa zaidi na kila ninapokutana na daktari wangu baada ya mazungumzo humuomba dawa hizo.

Ni vigumu kueleza namna dawa hizo zinavyonifanya nijisikie. Ziliondoa maumivu lakini ilikuwa zaidi ya hicho. Ubongo wangu ulikuwa mzito nilipozitumia dawa hizo, nilikuwa kama nisiyejua nina shida gani nilikuwa kama niliyeharibikiwa.

Baada ya kwenda hospitali, maisha yangu yalijawa na matukio ya kufanya vipimo na upasuaji wakati madaktari walipokuwa wakitafuta kinachonisababishia maumivu. Nilirudishwa nyumbani na kasha la dawa, nilikuwa nikiomba dawa zaidi kila zinapoisha nikidai kuwa nina maumivu.

Nilikuwa najisikia kama nahitaji dawa za kuondoa maumivu ili niweze kuwa vizuri. Kila asubuhi huwa naweka kasha la dawa kwenye mkoba wa shule , kuhakikisha kuwa zinakuwepo wakati wote kama ikitokea nahitaji zaidi.

Nilitegemea dawa kwa sababu nilikuwa nahisi siwezi kufanya vitu vingine . Sikuweza kukaa darasani na kuwa makini na masomo siku nzima kwa sababu ya maumivu, hivyo sikuweza kumaliza elimu ya sekondari. Nilipata kazi ya muda mfupi katika duka la nguo lakini nilishindwa kwa sababu ya kuumwa. Nilishindwa kujua ni nini kilichokuwa kikinisumbua hasa

Picha inayoonyesha mwanamke akiogelea kwenye bahari ya dawa

Chanzo cha picha, Thomas Dowse

Nilikuwa mwenye msongo wa mawazo, niliendelea na dawa za maumivu, nikijua kuwa ndio njia pekee ya kuniondolea maumivu ya mwili, akili, kila kitu. Nikaanza kuongeza idadi ya vidonge haraka haraka kwa majuma machache, nikawa nameza mara mbili na nusu ya dozi niliyopewa na daktari kwa siku. Ilikuwa kama dawa ziko kwa ajili yangu na nilipokuwa kwenye shida nilizitegemea sana.

Mwanamke akivunja dawa

Chanzo cha picha, Thomas Dowse

Wakati mpenzi wangu alipoamka na kunikuta nikitafuta dawa, niligundua kuwa wakati huo aliniona mraibu, nilikuwa mfichaji mzuri sana wa dawa zangu nikijua kuwa hawezi kuziona.

Siku iliyofuata, niliamua kutafuta msaada, daktari wangu alinielekeza kwenye kituo kimoja kinachowasaidia watu kuondokana na uraibu kwa kutumia miongozo na ushauri nasaha.

Mwanzoni nilikuwa na hofu . Nilipokuwa kazini nilikuwa nikiangalia kidonge kimoja mkononi, nikakichukia na kujichukia, nikiwa sitaki kukimeza.

Kujiondoa kwenye hali hiyo ilikuwa vigumu, nilikuwa najihisi mgonjwa sana na mchovu, siku nyingine nilishindwa kutoka kitandani na nilipokuwa kwenye maumivu nilikuwa napambana nisimeze vidonge.

Hatimaye niliimudu vita hiyo mwishoni mwa mwaka, nilikuwa safi, nilikuwa nikipunguza idadi ya vidonge mpaka nikaacha kutumia kabisa.

Siwalaumu madaktari. Ninajua wanafanya jitihada kubwa huku wakiwa na muda mchache na upungufu wa rasilimali. Na wataalamu wanasema kuwa watu wanapokuwa na uraibu hufanya kila mbinu wapate wakitakacho. Ndicho nilichokifanya.

Lakini nafikiri hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha watu wanafahamu madhara ya vidonge kwenye maisha yao, wanaponasa kwenye matumizi ya kupita kiasi. Sikuchagua kuwa mraibu wa dawa za kuondoa maumivu- ilinichukua taratibu mpaka niliposhindwa kuhimili tena.