'Vituo vya biashara ya Cocaine vimeundwa Ulaya, taasisi ya kupambana na dawa na uraibu wa dawa imeeleza

Chanzo cha picha, Reuters
Wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina ya cocaine wameunda ''vituo vya huduma kwa wateja'' barani Ulaya kwa ajili ya kufikisha dawa hizo kwa wateja kwa njia ya haraka na wepesi zaidi, Shirika la kupambana na dawa za kulevya na uraibu wa madawa la Umoja wa Ulaya limeeleza.
Wasambazaji hutumia smartphones katika mtandao wao wa biashara hiyo,limeongeza shirika hilo.
Utafiti huo umeonekana kwenye ripoti ya mwaka ya taasisi ya ufuatiliaji wa madawa na uraibu wa madawa (EMCDDA).
Pia imeonya kuwa mamlaka za nchi za Umoja wa Ulaya zinakamata viwango vikubwa vya cocaine.
Katika matumizi ya teknolojia ya digitali, ripoti imesema ''njia za usambazaji zinazitumika na wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni za ''ubunifu wa hali ya juu''
''Kuna ushahidi kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii, tovuti za kibiashara na mitandao ya kompyuta inayotumika kufanya biashara haramu inasaidia makundi madogo na mtu mmoja mmoja kujiingiza kwenye biashara hiyo'', taasisi hiyo imeeleza na kuongeza kuwa wauzaji hushindana kwa kutoa huduma za ziada zaidi ya usambazaji wa bidhaa yenyewe.

Chanzo cha picha, Getty Images
Neno lililojitokeza kwenye ripoti hii kitaalamu linaitwa "Uberisation". Yaani inaeleza namna magenge ya wafanyabiashara wa cocaine walivyotumia fursa za smartphone, app za kutuma ujumbe,na satellite kama zinavyofanya kampuni nyingine zinazofanya biashara halali.
Hali hii inafanya mitandao ya biashara hii kufanya kazi kwa haraka hivyo inakuwa vigumu kuibaini na kuiharibu,hasa kama bidhaa hizo huagizwa kwa kutumia vituo vyao vya huduma katika nchi nyingine.
Katika kutilia mkazo jambo hili, upatikanaji wa cocaine kwa wingi umeelezwa ni kutokana na ongezeko la kilimo cha mmea wa coca.Imekua ikipatikana kwa wingi kwa takriban miaka 20 hali inayofanya kushamiri kwa masoko huku wafanyabiashara nao wakitafuta njia za ubunifu kuwapiku washindani wao.
Kamishna wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya,Dimitris Avramopoulos,amesema ''ripoti imeonyesha kuwa madawa ya kulevya ni tishio kwa jamii zetu hivyo tunahitaji kwa pamoja kupata njia ya kupambana na hali hiyo lani pia kutazama kazi ya digitali katika soko la dawa hizi''.
Kwa mujibu wa EMCDDA, cocaine ''hutumika zaidi katika nchi za EU''kuwa na watumiaji milioni 2.6 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 34 mwaka jana.













