Rachel Wambui: Afanikiwa kukabiliana na uraibu wa pombe wa miaka 10

Chanzo cha picha, Rachel Wambui
Rachel alianza kutumia pombe akiwa na umri wa miaka 17 baada ya kumaliza masomo yake ya shule ya upili. Alianza kunywa pombe kama njia ya kujipatia raha pamoja na marafiki zake.
Kulingana na Rachel amesema siku yake ya kwanza ya kunywa pombe ndipo alipojihisi 'ametulia' na tangu siku hiyo akaanza kutumia pombe kama suluhu ya shida zake zote alizokuwa nazo.
Baada ya muda alianza kutumia kwa kiwango kikubwa cha pombe na bila kufahamu alikuwa na uraibu.
Rachel alitumia vileo kwa muda wa miaka kumi licha ya kwamba alikuwa na ndoto maishani na ahadi ya kuwa na maisha bora.Lakini ndoto hiyo ilikatika kwa muda wa miaka 10.
Rachel akizungumza na kipindi cha afya cha BBC amekiri uraibu wa pombe ni kitu kigumu kukabili lakini usaidizi alioupata kutoka kwa watu wengi hasa jamaa zake wa karibu ulimsaidia.
Kulingana na Rachel amesema mara nyingi alihisi kwamba watu waliomzunguka walikuwa hawamuelewi.Lakini siku moja familia yake iliamua kumzungumzia kuhusiana na hali yake na kumsihi ajiunge na sehemu ya watu walio na uraibu hupata usaidizi.
Rachel amesema alibaguliwa kwani jamii ilimtizama kama mwanamke aliyekosa nidhamu au hata maadili mema.
Kwa miaka hiyo kumi alipoteza kazi tofauti alizoandikwa kwani hakuwa na nia yoyote maishani wakati huo.
''Nilikuwa naamka na sikuwa najisikia kwenda kazi, matajiri wangu walinisaidia lakini sikuona umuhimu wowote wakati huo na hata Uhusiano na watu wanaokupenda uliharibika,'' Rachel amesema
Rachel alipofika umri wa miaka 27 aliamua kuweka chupa za pombe kando na kujitafuta tena maishani.
''sasa mimi ni mtu mwengine mpya nimeanza maisha upya ,''

Chanzo cha picha, Rachel Wambui
Rachel amesema safari yake ya miaka saba bila kutumia pombe haijakuwa rahisi kwani lazima kila siku aamke na akumbuke bado anaweza kurudia pombe wakati wowote ule.
Kwa hivi sasa anahisi furaha maishani.
Rachel ametoa wasio kwa mtu yeyote mwenye uraibu wa pombe kwamba uraibu huo una suluhisho.
Njia za kukabiliana na uraibu wa pombe
- Kujikubali
- Ushauri nasaha
- Kuzungukwa na watu wanaokukubali
Watu wenye uraibu wa pombe wanastahili kupendwa na kukubalika katika jamii lakini ni jukumu la mwenye uraibu kujikubali na kukubali usaidizi.













