Kuvunja unyanyapaa dhidi ya wanaume wanaojihusisha na ulezi wa watoto

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Marta Moreiras na wanaume aliowapiga picha - baba wanaoonekana wakibeba watoto wao mgongoni - walishangazwa kwa namna watu walivyowaangalia wakipigwa picha katika mitaa ya mji mkuu wa Senegal Dakar.
"Watu walikuwa wanapiga makofi - mara nyingine ilikuwa vigumu kuzipiga picha kwasababu kulikuwa na umati mkubwa wa watu waliokusanyika kututazama - mpiga picha huyo raia wa uhispania ameieleza BBC.
"Wanawake wote walikuwa wanasema: 'He, hebu nipe tano, ninakwenda kumuita mumewangu - hili ni jambo ambalo hatulioni kila siku."
Na ndio sababu kwanini Moreiras alianzisha mradi huu, ambao umeorodheshwa katika tuzo ya mwaka huu ya mashindano ya upigaji picha za kitaalamu - Sony World Photography Awards
Fikra hiyo ilimjia alipokuwa akitazama picha za zamani, nchini Senegal za tangu 2008.
"Niligundua kwamba nina picha nyingi za akina mama wakiwa wamewabeba watoto wao mgongoni, na ndio nikawaza, kwanini sina picha za wanaume wanoafanya hivyo?"

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Alipoanza kuwapigia rafiki zake wa kiume nchin iSenegal walio na watoto, baadhi yao walisema wako radhi kuwabeba watoto wao mgongoni lakini wanapokuwa nyumbani pekee - na sio nje hadharani.
"Kuna mgawanyiko mkubwa hapa wa nafasi za umma na za faragha - na ni jambo kubwa watu kuzingatia wengine wanavyowafikiria," anasema Moreiras.

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Licha ya hayo, utafiti wake umedhiirisha kwamba wanaume wana jukumu kubw akatika ulezi wa watoto, sio tu kwasbabau Dakar ni mji wenye gharama kubwa na mara nyingi wazazi wote huwa wanafanya kazi.
"Hilo linawafanya wagawanye majukumu.
"Na nilipowauliza wanaume iwapo wanasaidia katika masomo ya watoto wao na iwapo walisaidia katika majukumu ya nyumbani baadhi walijibu: 'Ndio, nalazimika kufanya hivyo, mkewangu anafanya kazi pia hawezi kufanya majukumu yote.'
"Lakini kila unapoona picha ya mtoto kwa mara nyingi haonekani akiwa na babake, akicheza naye akimpeleka shuleni au akimuosha," anasema.

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Hivi ndivyo alivyowashawishi watu aliowahoji ili awapige picha.
"Niliwaambia: 'haya basi ili kudhihirisha kwa uwazi zaidi jukumu la baba - nataka nikupige picha wewe na mwanayo.'"

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Walipolikubali hilo, aliwaambia angependa wambebe mtoto mgongoni badala ya mikononi, hili nalo pia wakaliridhia , walisita tu pale alipowataka watoke nje ili awapige picha hio hadharani .
"Hatufanyi hivyo, hatutoki hadharani tukiwa tumewabeba mtoto mgongoni," ndilo lililokuwa jibu la jumla - lakini msisitizo wa Moreiras uliishia kwa ufanisi.
"Kulikuwa na msisimko mkubwa hadharani, jambo lililowafanya niliokuwa ninawapiga picha kutulia zaidi."

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Picha hizo alizozipiga katika kipindi cha baina ya miezi miwili na mitatu zilionyeshwa hadharani mnamo Mei mwaka jana katika maonyesho ya sanaa Afrika ya Dak'Art, nchini humo.
Na zilizua mjadala bila shaka alipoamua kuzionyesha katika les parcours sportifs - eneo la wazi katika sehemu ya mbele ya ufuo wa bahari - linalojaa watu wanaokwenda kufanya mazoezi.

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
"99% ya watu wanaokwenda katika eneo hilo ni wanaume, wanaoonyesha misuli na ujasiri wa kuwa mwanamume,"anasema.
Lakini baadih ni walio katika umri wa kuwa baba - umati stahiki wa kulengwa kwa ujumbe huo anasema Moreiras.
Picha moja mahsusi iliwagusa wengi kutokana kwamba ilikuwa ni picha ya msanii maarufu Badou, anayejulikana kwa majigambo na kujivuna kwingi kiume.

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
" Ni kioo cha jamii, na kila mtu anamtambua. Ni muhimu katika mradi huu kwamba wamejumuishwa watu mashuhuri kwa mfano mwema na kufungua majadiliano katika kusaidia kutambua kwamba hakuna tatizo lolote na mwanamume kumbeba mtoto mgongoni au kusaidia na ulezi wa watoto hadharani," anasema mpiga picha huyo.
Kuna watu maarufu waliokataa ombi lake alipoafuata kutokana na kuhofia namna jamii itakavyowachukulia.
Kwa Moreiras, ambaye picha zake nane zimeorodheshwa katika tuzo ya picha duniani World Photography Awards, 'huu ni mradi usiokuwa na mwisho'.
"Bado ninashughulika nao - Ninafurahia kuwa na wanaume wengi watakaojitolea kwasababu naamini kumaliza unyanyapaa huu wa akina mama pekee kuhusishwa na jukumu la ulezi wa watoto, tunahitaji angalau kuona taswira inayotoshana kwa upande wa wanaume na jukumu hilo."

Chanzo cha picha, Marta Moreiras
Picha za Marta Moreiras.
Washindi wa tuzo ya 2019 Sony World Photography Awards watatngazwa 17 Aprili 2019. PIcha zote zitakazoorodheshwa kaika orodha ya mwisho zitaonyeshwa Somerset House mjini London kuanzia 18 Aprili hadi 6 Mei 2019.












