Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aandaa chakula, kuchangisha fedha za miradi

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anatarajiwa kuandaa chakula kwa ajili ya kuchangisha fedha, kuweza kusaidia kupata dola bilioni moja kwa ajili ya miradi ya miundombinu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa.

Maafisa nchini humo wanasema tiketi kwa ajili ya chakula hicho zitauzwa zaidi ya dola za Marekani 175,000 kwa mtu mmoja. Lakini taarifa zaidi hazikuwekwa wazi.

Chakula hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu vitega uchumi vya kigeni katika nchi hiyo ya Afrika inayokuwa haraka kiuchumi.

Tangu alipoingia madaraka mwaka jana, Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini humo.

Waandishi wa Habari wanasema Ethiopia imeamua kuchangisha fedha yenyewe kuliko kutegemea zaidi misaada ya kigeni. Tukio kama hilo limepangwa pia kwa ajili ya kuchangia uwekezaji wa kiuchumi na misaada ya kibinadamu.

Waziri mkuuu wa Ethiopia aliuza saa yake kwa kiasi cha dola za Marekani 175,000 kwa ajili ya kuchangia mradi wa Miundo mbinu wa Ambo, ambapo jumla ya dola za Kimarekani milioni 14 zilipatikana katika uchangishaji huo.

Wanawake wa Ethiopia na Eritrea

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanawake wa Ethiopia na Eritrea

Waziri mkuu Abiy Ahmed aliingia madarakani baada ya miaka mitatu ya maandamano yaliyokuwa yakifanywa na watu wa kabila la Oromo, ambao walikuwa wakidai kumalizwa, kwa kile walichokielezea kama kutengwa kwao kisiasa na kiuchumi.

Toka kuapishwa kwake, tayari ameleta mabadiliko mengi nchini humo, ikiwemo pia kuleta amani na nchi jirani Eritrea.