Je maslahi ya raia ni kipa umbele kwa wabunge Kenya?

Bunge la Kenya

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Maelezo ya picha, Bunge la Kenya
    • Author, Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi

Swali ambalo limejaa vinywani mwa Wakenya wengi kwa sasa ni: Je, Bunge la Kenya limeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo?

Swali hili linatokana na visa vya hivi karibuni ambapo wabunge wa Kenya wamejipata wakilaumiwa kwa jinsi wamekuwa wakishughulikia majukumu yao rasmi bungeni.

Katika kisa cha hivi karibuni zaidi, wabunge walilaumiwa na Wakenya kwa kutoshughulikia swala la gharama ya maisha na ushuru wa dhamana kupanda, jambo lililosababisha kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli pamoja na bei ya bidhaa nyingine muhimu kwa maisha ya Mkenya wa Kawaida.

Itakumbukwa kwamba, baada ya bunge la Kenya kupitisha mswaada wa kodi ya ushuru unaotozwa bidhaa za mafuta ya petroli na kuhairisha utekelezwaji wake, Rais Uhuru Kenyatta alijivuta kutia saini na kuiirudisha sheria hiyo bungeni pamoja na mapendekezo yake.

Ili kuyakataa mapendekezo haya, iliwahitaji wabunge theluthi mbili ya bunge la kitaifa kuyapinga mapendekezo hayo ili kuhakikisha kutotekelezwa kwa sheria hii.

Hata hivyo, badala ya kuishughulikia sheria hiyo ili kuhakikisha kuwa bei ya mafuta ya petroli na bidhaa nyingine hazijapanda, wabunge walianza mbwembwe na nyimbo bungeni hali iliyochangia mtafaruku na kushindwa kwa juhudi zao na kupita kwa sheria hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta amependekeza kupunguza hadi 8% tozo la kodi kwa mafuta

Chanzo cha picha, POOL/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta alipendekeza kupunguza hadi 8% tozo la kodi kwa mafuta

Kutokana na hali hii, hadhi ya bunge la Kenya imekuwa ikishuka miongoni mwa macho na fikra za Wakenya wengi.

Kwa muda sasa, kumekuwa na shutuma kuwa wabunge hufikiria na kujihusisha na maslahi yao tu na kutaka kujiongezea mishahara na marupurupu badala ya kulenga kutunga sheria na sera za kuwajali walio wengi nchini Kenya.

Kumekuwepo na visa vingi katika siku za hivi karibuni ambapo bunge la Kenya limejipata likilaumiwa kuhusiana na kutoyashughulikia maslahi ya Wakenya katika kazi yao bungeni.

Baadhi ya wabunge walidaiwa kupokea hongo ya shilingi 10,000 (za Kenya) ili kusaidia katika kuhakikisha kuwa ripoti ya kamati ya bunge kuhusu kilimo iliyotayarishwa kuhusu sukari ambayo haikuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Waandamanaji walisimama nje ya bunge na mabango wakilalamika kuhusu sheria hiyo ya kodi
Maelezo ya picha, Waandamanaji walisimama nje ya bunge na mabango wakilalamika kuhusu sheria hiyo ya kodi

Baada ya ripoti hiyo kushindwa bungeni, kulikuwepo na shutuma zilizoelekezewa wabunge kwa kula mlungula ili kuhakikisha kuwa ripoti hiyo ambayo ilikuwa inawalaumu maafisa wakuu serikalini na mawaziri kwa kuingizwa kwa sukari isiyofaa nchini Kenya.

Baadhi ya wabunge walijitokeza wazi na kutangaza kuwa walikuwa wamewaona wabunge wakihongwa ili kuipinga na kuiangusha ripoti hiyo.

Pamoja na haya yote, kile ambacho ni bayana miongoni mwa Wakenya wengi ni kuwa bunge la sasa nchini Kenya linagubikwa na ukosefu wa uaminifu na hili linaonekana kuchangia kuwepo chuki dhidi ya bunge.

Hali hii ya chuki dhidi ya wakuu fulani serikali na baadhi ya taasisi nchini Kenya inatokana na visa ya ufisadi vinavyoendelea kufichuliwa na gharama ya maisha ambayo inaendelea kupanda kila kukicha.

Itakumbukwa kwamba Rais Kenyatta alianzisha mpango wa kupigana dhidi ya ufisadi jambo ambalo limechangia wakuu wengi wa taasisi za serikali kufikishwa mahakamani.

Wandamanaji wanaopinga ufisadi serikalini wakiwa katika jiji kuu la Kenya Nairobi
Maelezo ya picha, Wandamanaji wanaopinga ufisadi serikalini wakiwa katika jiji kuu la Kenya Nairobi

Kutokana na visa hivi vya bunge la Kenya kutowachukulia hatua wakuu serikalini ambao wametajwa kwenye kashfa mbali mbali na kutochukua hatua ya kuwatetea Wakenya walio wengi, ni dhahiri shairi sasa kuwa bunge la Kenya limeshindwa kudhibiti na kuisimamia serikali na jukumu lake la kutunga sheria na sera ambazo zinaangazia hali ya Wakenya.

Majukumu ya bunge katika katiba Kenya:

  • Kulingana na katiba ya Kenya, bunge lina majukumu kadhaa.
  • Bunge "linawakilisha matamanio ya Wakenya, na kuchukua jukumu hilo la uhuru kwa niaba ya Wakenya", kwa mfano.
  • Bunge la kitaifa "linajadili na kuamua kuhusiana na masuala yanayowahusu watu."
  • Linatunga sheria (wakati mwingine jukumu hilo linagawanya na bunge la seneti).
  • Bunge pia lina jukumu la kuamua jinsi fedha zinavyogawanywa baina na kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti, linaidhinisha fedha za kutumiwa na serikali ya kitaifa na taasisi nyingine za serikali, kupitia kwa bajeti, linasimamia taasisi za serikali na jinsi fedha za serikali zinavyotumika.

Kwa muda sasa, kumekuwepo na tetesi nchini Kenya kuwa baadhi ya wabunge "hununuliwa" ili kuuliza maswali fulani bungeni, kuunga mkono au kupinga hoja.

Tofauti na nchi nyingine ambako mipango ya kisiri hufanyika kila mara kuwafumania na kuwanasa wabunge wakipokea hongo, hakuna mbunge yeyote nchini Kenya ambaye amewahi kufumaniwa kuhusiana na ufisadi.

Haya yote yakifanyika, kinaya ni kuwa wabunge wenyewe wamekubali waziwazi kuwa wamekuwa wakipokea hongo, hata chooni!

Itakumbukwa kuwa katika miaka ya 90, nchini Uingereza, wabunge wawili wa chama cha Conservative waliadhibiwa eti kwa sababu ya kuuliza maswali bungeni mwao kwa niaba ya wafanyabiashara matajiri wawili.

Kesi hiyo, na nyingine ambazo zilitokea baadaye, zilishughulikiwa bungeni na wabunge wenyewe kutoruhusiwa kuhudhuria bunge kwa muda mfupi. Aidha, kumekuwepo na visa vya ukosefu wa maadili miongoni mwa wabunge nchini Marekani katika bunge la Congress.

bei ya mafuta kenya

Je Wabunge hulipwa kuuliza maswali bungeni?

Nchini Kenya, mashirika mengi yasiyo ya kiserikali na wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusiana na na shutuma za wabunge kuuliza maswali bungeni kwa malipo.

Ripoti ya Transparency International (TI), kwa mfano, ilidai kuwa watu na mashirika fulani waliwalipa wabunge kuuliza maswali bungeni na kuleta hoja kisiasa na wakiwa na malengo ya kiuchumi.

Ripoti hiyo pia ilieleza kuhusu ukosefu wa maadili wakati wa kuwachuja maafisa wakuu katika kamati za bunge; kwamba baadhi ya wanakamati hulipwa kuwaunga mkono au kuwapinga maafisa ambao majina yao yamependekezwa na serikali.

Pia, kumekuwepo na shutuma kuwa wabunge wengi nchini Kenya wanafikiria kuwa jukumu lao kuu ni kusimamia hazina ya maeneo bunge yaani CDF.

Hata hivyo, hili haliwezi kuwa hivyo kwa sababu wao ni wanasiasa na jukumu kama hilo ni wafanyikazi wa umma kama katiba ya Kenya inavyoeleza.

Wakenya wengi wanatarajia kuwa badala ya kushughulikia mambo yasiyo na umuhimu kwa taifa, wabunge wangekuwa wanajadili maswala kama sekta ya kilimo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakenya wengi wanatarajia kuwa badala ya kushughulikia mambo yasiyo na umuhimu kwa taifa, wabunge wangekuwa wanajadili maswala kama sekta ya kilimo

Ni nini kimewakumba wabunge nchini Kenya?

Mijadala bungeni haielekezwi na misimamo; ama hata kuwepo hali ya kupinga hoja kwa sababu ya msimamo. Kuhusishwa hakutokani na chama lakini kwa ngazi za chama hata kama vyama hivyo havina mipangilio kama hiyo.

Hata hivyo, kuwashutumu wabunge wa Kenya kijumla, labda, haifai. Labda, itabidi tuchunguze mfumo wa jinsi wawakilishi hawa huchaguliwa.

Hii ni kwa sababu itakuwa ajabu kutarajia hali nzuri kutoka kwa taratibu ambazo wengi wanakubaliana zina hitilafu na huvurugwa wakati mwingine kuhakikisha kuwa wale wasiofaa ndio hufaulu.

Tukumbuke pia kuwa wananchi hupata aina ya viongozi ambao huwachagua.

Lililo dhahiri hata hivyo ni kuwa Wakenya wanahitaji wabunge watakaojali maslahi yao zaidi kuliko ya wabunge binafsi.

Mchakato ambao utafaulisha kuchaguliwa kwa wawaniaji kwenye michujo ya vyama na wenye sifa nzuri na watakaofanya kazi nzuri kwa ajili ya wote ndio njia mojawapo ya kulitatua hili.

Wakenya wengi wanatarajia kuwa badala ya kushughulikia mambo yasiyo na umuhimu kwa taifa, wabunge wangekuwa wanajadili maswala kama deni la kitaifa na maendeleo kwa jumla, suala sugu la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini Kenya, kupanuka kwa mwanya kati ya matajiri ma maskini, sekta ya kilimo ambayo inaendelea kudidimia, na matatizo mengine mengi yanayoikodolea macho nchi ya Kenya.