Makozmen: Watu wenye tabia ya kipekee ya kuchungulia wapendanao usiku wa manane Mombasa Kenya

- Author, John Nene
- Nafasi, BBC News, Mombasa
Kwa miaka mingi sasa tabia ya watu wazima na vijana kuchungulia wapendanao wanapojiburudisha usiku imeshamiri pwani ya Kenya kiasi kwamba kwa wengine ni jambo la kawaida watu hawa - wajulikanao kwa jina la utani kama Makozmeni - kuendelea na tabia hii duni ambayo imekua ni kero kubwa kwa waliofunga ndoa mji wa Mombasa hasa mitaa ya Majengo na Kisauni.
Makozmeni ni watu ambao wana tabia ya kipekee ya kuchungulia wapendanao usiku wa manane.
Ni tabia iliyoenea sana pwani ya Kenya na hata Dar es Salaam nchini Tanzania na Zanzibar ambako watu hao wa kuchungulia hupatikana.
Kulingana na Kozmeni huyu ambaye nimezungumza naye kwa muda na hatimaye akaacha, wao huchungulia kuanzia saa nane kwenda juu.
Je, huwa wanafanya utafiti kujua ni wapi watachungulia?
``Kwa kawaida mimi nachungulia hapa Majengo, nina nyumba zangu nne ambazo najua sitakosa sinema kila siku. Huwa kwanza mchana nazunguka nikiangalia wako kwenye hali gani..Si wajua hapa Mombasa wengine hawaendi kazini lakini utapata mtu yuko sawa. Nikiona wako nje wanacheka wamefurahi basi najua usiku sitakosa filamu nzuri''
``Nimekua nachungulia tangu mwaka wa 1998. Ni uraibu mbaya lakini nimeshindwa kabisa kuacha tabia hiyo. Basi huwa kwanza nala miraa halafu naanza kazi kama saa tisa maanake kwa ujuzi wangu wa hizo ndizo time watu huanza mambo hayo. Hapa Majengo watu wengi hawafungi madirisha kwa sababu ya joto la Mombasa. Kuna wale huzima stima na wengine hawazimi lakini wamefunga pazia. Huwa natumia waya za baiskeli, zaitwa spoki. Naitumia kuvuta pazia kando kisha naburudika.''
Kuna Kozmeni mwingine naye kuchungulia maeneo ya Kisauni. Huyo hubeba kiti chake na dawa ya mbu.
``Natumia kiti mimi kuchungulia kwa sabababu madirisha yako juu kwa hivyo inabidi nipande stool ndiyo nijionee ngoma,'' anasema.
``Mbali na kiti nina dawa ya mbu inayonisaidia usiku kutoshambuliwa na mbu. Huu ni uraibu ningetaka niuache lakini nashindwa. Tena nina mke lakini usiku natoka kwenda kukozi.''
Tabia ya Makozmeni imekua ni kero kubwa kwa wakaazi wa Mombasa lakini kulingana na wadokezi wangu huko, polisi hawajaelezwa vizuri kuhusu tabia hii.
Mama Pili anasema:``Hawa wanastahili kukamatwa, si vizuri kuchungulia mtu akifanya tendo la ndoa kwa sababu hayo ni mambo yake binafsi hangetaka mtu ayaone lakini hawa Makozmeni ndiyo raha yao hiyo. Twawajua lakini twaogopa kuwasema. Sisi twawachukulia kama wahalifu hapa Majengo.''
Adhabu wanayopata wakipatikana
Wanapopatikana hupigwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama. Miongoni mwao huacha tabia hiyo na wengine wanaendelea.
Mohammed Paka Mkali anasema kuna siku alilazimika kummwagilia mafuta ya diesel Kozmeni mmoja mtaa wa Majengo.
``Huyo nilimkomesha kabisa. Sote twamjua kwa tabia zake hizo na ni mtu ameoa. Siku hiyo mke wangu nikamwambia leo nitamkomesha. Basi tukajipanga mke wangu akawa kitandani nami nikajibana kwa dirisha tumezima taa, nikasikia ndio huyo yuaja. Alipojaribu kukaribia dirisha letu nilimwagia diesel ikamchafua mwili wote kuanzia kichwa hadi chini akakimbia kwake na aibu yote hiyo. Ndugu zake walinipongeza sana kwa kumkomesha. Mke wake naye pia akafurahia jinsi nilimtendea maanake naye alikua amechoka na tabia za mumewe. Kutoka siku hiyo kwangu hajaonekana tena. Sijui kama anachungulia nyumba zingine.''
Kozmeni mwingine naye sehemu ya kaunti ya Tana River naelezwa alimwagiwa pilipili machoni kisha akapigwa sana huku akilia kama mtoto, na mkewe akaitwa aone jinsi mumewe anavyolia baada ya kupatikana akichungulia.
Huyo wa Majengo pia hatimaye alipatikana kama anavyotueleza: Mazee sitasahau siku hiyo. Nilipigwa kama mbwa na watu zaidi ya kumi walionipata nikichungulia. Nilichapwa zaidi mbavu na sehemu zingine mwilini. Kutoka siku hiyo niliamua kuacha kuchungulia kabisa. Sasa nimeoa na nina watoto wawili wa kiume. Kazi nafanya ya Tuk Tuk . Hata nimeanza kuzungumza na Makozmen wengine waache tabia hiyo.''
Atafanya nini akijipata naye anachunguliwa usiku na Kozmeni yeye akiwa amepitia hapo?
``Lo! wajaribu, mimi siwezi kukubali mtu anichungulie. Nitampiga vilivyo.''
Utampiga vipi na wewe mwenye ilikua ni kazi yako hiyo, namuuliza.
``Najua nimefanya hivyo miaka mingi lakini sitampa mtu nafasi hiyo ya kunichungulia. Ikifika usiku kwanza mimi hutoka nje niangalie hali ikoje kwa sababu najua time zao za kuanza kuchungulia. Nikisha hakikisha hamna mtu narudi ndani kuendelea na shughuli.''
Daktari wa maradhi ya akili Frank Njenda anasema huu ni uraibu kama ule wa pombe na mihadarati na kwamba makozmen ni watu wanaohitaji usaidizi mkubwa na hata polisi hawafai kuwakamata.
``Huu ni uraibu unajulikana kote duniani lakini wakitaka kuacha wanashindwa. Wengine huanza kwa sababu wameona marafiki zao wanachungulia, na wengine wanajitosheleza wakiona watu wa ndoa kwa hilo tendo.
Lakini wakili Muciimi Mbaka anasema wanastahili wakamatwe kwa sababu tabia hiyo ni kinyume cha sheria.
``Kwa sheria za Kenya kuna kifungu cha watu kama hawa, na mtu akipatikana na hatia hiyo anafungwa miaka mitatu,'' kwa mujibu wa Muciimi..












