Je unajua madhara ya njia za mkato katika kutafuta kupunguza unene wa mwili wako?

Kunenepa sana

Chanzo cha picha, Thinkstock

    • Author, Lulu A. Sanga
    • Nafasi, BBC Swahili

'Pungua kidogo, he! umenenepa sana, punguza kula, utapasuka', ni baadhi ya kauli zinazo tajwa na baadhi ya watu wanapo ona mtu ameongezeka mwili au ame nenepa kama wengi wanavyopenda kutafsiri.

Kauli hizo hizo huwafanya watu wenye mwili mkubwa kutapa tapa katika kutafuta namna inayoweza kuwasaidia kupunguza mwili. Baadhi wanafahamu njia salama lakini wengi hutamani njia za mkato ambazo pia ni za haraka kama vile kutumia dawa.

Kwa sasa kupitia mitandao ya kijamii kumeshamiri matangazo ya dawa mbalimbali za kupunguza mwili, na idadi kubwa ya watu huonyesha kutamani kuzitumia kwa kuuliza maswali na kujiunga na makundi mbali mbali ili kufanikiwa.

Dawa hizo za kupunguza unene hupatikana kulingana na uwezo wa mtumiaji. Kawaida huanzia bei ya shilingi elfu Tano mpaka laki tano. Katika kundi hilo kuna ambazo zina tangazwa kuwa zimethibitishwa na mkemia mkuu na baadhi zenyewe huandikwa jina la dawa na kazi zake tu.

Wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo huzinadi sana kupitia mitandao, vipeperushi na hata kwenye matangazo mitaani.

Dawa hizo zina sifa mbali mbali ambayo kwa maelezo yake humvutia mtumiaji. Mojawapo ya sifa hizo ni kuwa zina punguza unene, hufanya mwili kuwa mwepesi, zinaondoa sehemu mbaya mwilini, kuondoa sumu mwilini, kupunguza kitambi, kujenga afya na kuepuka magonjwa sugu kama vile kiharusi, kisukari na magonjwa ya moyo.

Mtumiaji na muuzaji wa dawa za kupunguza unene

Chanzo cha picha, Dativa Mosha

Maelezo ya picha, Dativa Mosha yeye ni mtumiaji na muuzaji wa dawa za kupunguza mwili anasema inategemea dawa ambayo mtu anatumia, zipo zilisho thibitishwa na mamlaka husika

BBC imewatafuta baadhi ya watumiaji wa dawa hizo ili kupata ufafanuzi kama dawa wanazo tumia zimethibitishwa na je wamepata matokeo?

"Mie natumia hiyo dawa nimenunua elfu ishirini wanasema ni dawa ya asili kwa ivo nikinywa usiku asubuhi na harisha na matokeo na yaona, sema ndo lazima ufanye diet," anasema Leina.

Hata hivyo wapo ambao wametumia dawa mbali mbali lakini zote wanasema zina mashariti.

"Mie mwenzangu nimetumia dawa za kila aina kwa kweli, nimetumia makampuni yote ya dawa unayo yajua hapa tz, mpaka zile za buku tano sema ndo kuharisha mpango mzima. Na zinanikera kwasababu lazima nifanye diet na mazoezi ndo nione matokeo," Mama Abuu anaiambia BBC

Dativa Mosha yeye ni mtumiaji na muuzaji wa bidhaa za edmark ambaye pia alifanikiwa kupunguza mwili wake.

"Kila kampuni inatengeneza bidhaa na watu binafsi saivi wameongezeka kuandaa dawa za kupunguza mwili na ni kwasababu wameona watu wanashida hiyo.Matokeo ya dawa yanategemea na bidhaa anayo tumia mtu, wengine wanatumia miti shamba wengine mizizi wengine tiba lishe au vyakula virutubisho. Lakini watumiaji mtu yupo tayari kubadilisha mfumo wake wa ulaji? Kama unatumia na unaendelea kula kama kawaida upatikanaji wa matokeo unakuwa ni mdogo au unakosa kabisa," anasema Dativa Mosha

Daktari Fredrik Mashili kutoka chuo kikuu cha sayansi na Tiba Muhimbili anatathmini kwa undani juu ya matumizi ya dawa za kupunguza mwili.

Athari za matumizi ya dawa za kupunguza mwili

Daktari Mashili anasema watu wengi wanapenda njia za mkato kwa kiasi kikubwa na wanapenda kupata matokeo ya haraka, hivyo huchagua dawa za kupunguza unene na kukwepa njia salama ya kufanya mazoezi na kubadili mfumo wa chakula.

Anasema, zipo dawa za kupunguza unene zimefanyiwa tafiti na zinakubalika kisayansi, lakini zinafanya kazi kwa njia tofauti na huenda si dawa zinazoweza kutumiwa na kila mtu. Hivyo ni vizuri kufahamu madhara yanayoendana na dawa hizo.

"Baadhi wanatumia dawa za kupunguza uzito bila kupata ushauri wa wataalamu, pia sina uhakika sana ila dawa nyingi za kupunguza uzito nchini kwetu hazija pata vibali, nyingi ni dawa za mtaani ambapo kiukweli zingine si dawa za uhakika au zinatumia njia ambazo si sahihi, anasema dokta Mashili.

Anaongeza kua baadhi hudhani wamepungua kumbe wana sinyaa.

unene

Chanzo cha picha, SPL

"Kuna dawa nimeona watu wengi wanatumia, wanachanganya kwenye maji alafu inamfanya mtu anaharisha sana kwa maana ya kwamba anapoteza maji mengi. Na ukipoteza maji maana yake ni kwamba utasinyaa, si kwamba umepungua bali ume sinyaa. Mtu atajiona kweli amepungua mwili kumbe si kweli bali amepunguza maji mwilini njia ambayo ni hatari. Hakuna kitu muhimu kwenye mwili wa binadamu kama maji," Dokta Mashili anaiambia BBC.

Anasisitiza kuwa zipo dawa mitaani ambazo hazina uthibitisho wowote wa ki sayansi watu wanazitumia, na wanao wapa kuzitumia si wote wanautaalamu wa namna hizo dawa zinafanya kazi. Anaongeza kuwa hakuna dawa za kupunguza uzito zilizo thibitishwa na kutumika hospitalini ama zikatolewa na daktari anayetoa mwongozo sahihi.

"Hakuna njia ya mkato katika maisha, watu wanao ziuza hizo dawa nadhani wanakuwa kibiashara zaidi. Hakuna dawa pekeake ambayo imethibitika ya kupunguza uzito mtu akakupa bila mashariti yoyote kwenye chakula au kufanya mazoezi na ikafanya kazi, kisayansi hakuna hiyo dawa. Tuwe makini sana," dokta mashili anaiambia BBC.

Hata hivyo anatoa ushauri kwa watu ku hoji kwa undani juu ya dawa hizo, kwani hakuna dawa inayotengenezwa kwa siri. Inapo anza tu kutumika lazima iwekwe wazi hivyo kunakuwa na machapisho ya kisayansi yanayo elezea dawa inavyo fanya kazi, inavyo tumika na madhara yake.