Somaliland yapitisha sheria dhidi ya wabakaji

Waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono wakishiriki katika somo la uchoraji katika kituo kimoja Mogadishu, Somalia

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono wakishiriki katika somo la uchoraji katika kituo kimoja Mogadishu, Somalia

Bunge katika eneo la Somaliland lililojitangazia uhuru wake limepitisha sheria mpya dhidi ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Kulingana na sheria hiyo atakayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 30 gerezani.

Sheria hiyo pia inapiga marufuku mpango wa kusuluhisha kesi za unyanyasaji wa kingono kupitia njia za kitamaduni.

Spika wa bunge la Somaliland Bashe Mohamed Farah ameambia BBC kwamba visa vya ubakaji vimekuwa vikiongezeka lakini anatumai kwamba sheria hiyo itazuia hilo sasa.

Ubakaji utachukuliwa kama kosa la uhalifu badala ya tatizo la kijamii au kitamaduni.

Njia za kitamaduni, ambazo mara nyingi humfaa mbakaji, pia zimeharamishwa.

Awali, wabakaji wangetakiwa kuwaoa waathiriwa wao, na familia zingeuka mkono hilo kuepuka kubaguliwa na aibu ya kufahamika kwamba mtoto wao alibakwa.

Sheria hiyo mpya imepitishwa baada ya juhudi za miaka mingi za watetezi wa haki za wanawake na watoto.

Faisa Ali Yusuf wa Wakfu wa Ajenda ya Wanawake ameambia BBC kwamba wameisubiri sheria hiyo kwa miaka mingi.

Somaliland inataka pia kuonekana kimataifa kama taifa la kidemokrasia lenye mifumo ya kidemokrasia inayofanya kazi.

Hata hivyo, kutekeleza sheria kama hiyo katika jamii iliyojikita sana katika utamaduni itachukua juhudi zaidi.

Nchini Somalia, hakuna sheria dhidi ya ubakaji.