Uchaguzi Kenya 2017: Nusu ya wapiga kura wameshiriki uchaguzi

Mmoja wa wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi Mombasa

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, Mmoja wa wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi Mombasa

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Wafula Chebukati amesema wanakadiria kwamba idadi ya waliojitokeza kupiga kura leo kufikia wakati wa kufungwa kwa vituo saa kumi na moja jioni ni asilimia 48.

Akihutubia wanahabari, mwenyekiti huyo amesema vituo asilimia 87 kati ya vituo vyote vya kupigia kura vilifunguliwa, ambavyo ni vituo 35,564.

Fomu za matokeo kutoka kwa vituo vya kupigia kura 27,124 zimepokelewa.

"Vituo 5,389 ambavyo vimetapakaa kote nchini havikufunguliwa. Baadhi vimo katika kaunti nne ambazo nilitangaza awali kwamba uchaguzi umeahirishwa," amesema.

Bw Chebukati amesema vituo kamili ambavyo uchaguzi umeahirishwa hadi Jumamosi vitatangwa kesho katika gazeti rasmi la serikali.

Baadhi ya watu wameshutumu tarehe mpya ya uchaguzi iliyotangazwa na Bw Chebukati wakisema Jumamosi ni siku ya ibada kwa waumini wa kanisa la Kiadventisti ambao ni wengi katika kaunti ambazo uchaguzi umeahirishwa.

Bw Chebukati hata hivyo amesema tume ilizingatia mambo mengi kabla ya kutangaza tarehe mpya.

"Matokeo ya uchaguzi ni lazima yatangazwe katika siku saba. Lazima tujinyime baadhi ya mambo. Wasiotaka kupiga kura hawatalazimishwa," amesema.

Masanduku ya kupigia kura ya eneo bunge la Kisumu ya Kati ambayo hayakusafirishwa vituoni. Eneo hilo lina vituo 196.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, Masanduku ya kupigia kura ya eneo bunge la Kisumu ya Kati ambayo hayakusafirishwa vituoni. Eneo hilo lina vituo 196.

Tume ya Uchaguzi imekuwa ikipakia fomu za matokeo kutoka kwenye vituo vya kupigia kura mtandaoni.

Kinyume na awali, fomu zinawekwa zilivyo mtandaoni.

Kufikia sasa, fomu za matokeo kutoka vituo 21,033 kati ya 40,883 zimepakiwa.