Ayatollah Khamanei: Kiongozi mkuu wa Iran anavyokumbwa na manung'uniko ya upinzani kuhusu uongozi

Muda wa kusoma: Dakika 7

Baada ya kukaa karibu wiki mbili katika chumba cha siri mahali pasipojulikana nchini Iran wakati wa vita vya nchi yake na Israel, kiongozi mkuu wa kidini, Ayatollah Ali Khamenei, 86, amejitokeza na kusisitiza kuwa iran ilishinda katika vita vyake vya hivi karibuni na Marekani.

Anaaminika kuwa alikuwa amezuiliwa kwa hofu ya kuuawa na Israel. Hata maafisa wakuu wa serikali inaonekana hawakuwa na mawasiliano naye.

Alishauriwa kuwa mwangalifu, licha ya usitishaji dhaifu wa mapigano ambao Rais wa Marekani Donald Trump na Amiri wa Qatar walisimamia. Ingawa inasemekana kwamba Rais Trump aliiambia Israel isimuue kiongozi mkuu wa Iran, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huenda angepuuza.

Wakati - au iwapo - ataibuka kutoka mafichoni, ataona mandhari ya kifo na uharibifu. Bila shaka bado ataonekana kwenye TV ya serikali akidai ushindi katika mzozo huo. Atapanga kurejesha hadhi yake. Lakini atakabiliwa na ukweli mpya - na enzi mpya.

Vita vimeiacha nchi ikiwa dhaifu sana na yeye kuwa mtu aliyedhoofika.

Pia unaweza kusoma

Manung'uniko ya upinzani

Wakati wa vita, Israel ilichukua udhibiti wa anga ya Iran haraka, na kushambulia miundombinu yake ya kijeshi. Makamanda wakuu na Walinzi wa Mapinduzi ya jeshi waliuawa haraka.

Kiwango cha uharibifu wa jeshi bado hakiko wazi na kinabishaniwa, lakini mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi na vituo vya walinzi wa mapinduzi yanaashiria uharibifu mkubwa wa nguvu za kijeshi za Iran. Jeshi lilikuwa limetumia rasilimali nyingi za taifa kwa muda mrefu.

Vituo vinavyojulikana vya nyuklia vya Iran ambavyo viliiwekea nchi hiyo karibu miongo miwili ya vikwazo vya Marekani na kimataifa, vinavyokadiriwa kugharimu mamia ya mabilioni ya dola, sasa vimeharibiwa kutokana na mashambulizi ya anga, ingawa kiwango kamili cha hilii imekuwa vigumu kutathminiwa. Ilikuwa ya nini, wengi wanauliza.

Idadi kubwa ya raia wa Iran kwa umoja wao itamshikilia Ayatollah Khamenei, ambaye alikua kiongozi kwa mara ya kwanza mwaka 1989, kuwajibika kwa kuiweka Iran kwenye mkondo wa mgongano na Israel na Marekani ambao hatimaye ulileta uharibifu mkubwa kwa nchi yake na watu wake.

Watamlaumu kwa kufuata lengo la kiitikadi la kuangamiza Israeli - jambo ambalo Wairani wengi hawaungi mkono. Watamlaumu kwa kile wanachokiona kama upumbavu - imani yake kwamba kupata hadhi ya nyuklia kungeufanya utawala wake kutoshindwa.

Vikwazo vimedhoofisha uchumi wa Iran, na kupunguza uwezo wake wa kuuza mafuta nje hadi kuwa kivuli kwa ubinafsi wake .

"Ni vigumu kukadiria ni muda gani utawala wa Iran unaweza kudumu chini ya matatizo makubwa kama haya, lakini hii inaonekana kama mwanzo wa mwisho," anasema Profesa Lina Khatib, mwanazuoni mgeni katika Chuo Kikuu cha Harvard.

"Ali Khamenei huenda akawa 'Kiongozi Mkuu' wa mwisho wa Jamhuri ya Kiislamu kwa maana kamili ya neno hili."

Kumekuwa na manung'uniko ya upinzani kuhusu uongozi. Katika kilele cha vita hivyo, shirika moja la habari la Iran liliripoti kwamba baadhi ya viongozi wakuu wa zamani wa utawala wamekuwa wakiwataka wasomi wa kidini walio kimya zaidi wa nchi hiyo walioko katika mji mtakatifu wa Qom, ambao wamejitenga na Ayatollah, kuingilia kati na kuleta mabadiliko katika uongozi.

"Kutakuwa na hesabu," kulingana na Profesa Ali Ansari, mkurugenzi mwanzilishi wa Taasisi ya Mafunzo ya Iran katika Chuo Kikuu cha St Andrews.

"Ni wazi kabisa kwamba kuna kutoelewana kukubwa ndani ya uongozi, na pia kuna ukosefu mkubwa wa furaha miongoni mwa watu wa kawaida."

'Hasira na mfadhaika vitaota mizizi'

Katika muda wa wiki mbili zilizopita, Wairani wengi walipambana na hisia zinazokinzana za hitaji la kuilinda nchi yao dhidi ya chuki yao kubwa dhidi ya serikali.

Walipigania nchi, si kwa kujitokeza kutetea utawala, bali kuangaliana wao kwa wao. Kumekuwa na ripoti za mshikamano na ukaribu mkubwa.

Watu katika miji na vijiji nje ya maeneo ya mijini walifungua milango yao kwa wale ambao walikimbia mabomu katika miji yao, wauzaji wa maduka walitoza bidhaa za kimsingi, majirani waligonga milango ya kila mmoja kuuliza ikiwa walihitaji chochote.

Lakini watu wengi pia walikuwa wanafahamu kwamba Israel pengine ilikuwa inatafuta mabadiliko ya utawala nchini Iran.

Mabadiliko ya utawala ndio ambayo Wairani wengi wanatamani. Wanaweza kuchora mstari kwenye mabadiliko ya serikali yaliyobuniwa na kuidhinishwa na mataifa ya kigeni.

Katika takriban miaka 40 ya utawala wake, Ayatollah Khamenei, mmoja wa watawala wa muda mrefu zaidi duniani, amemaliza upinzani wowote nchini humo. Viongozi wa kisiasa wa upinzani wako jela au wametoroka nchini. Nje ya nchi, takwimu za upinzani hazijaweza kuunda msimamo unaounganisha upinzani dhidi ya utawala.

Wameshindwa katika uanzishaji wa aina yoyote ya shirika linaloweza kuchukua madaraka ndani ya nchi iwapo fursa itatokea.

Na wakati wa wiki mbili za vita, wakati kuanguka kwa serikali kungeweza kuwa jambo linalowezekana, ikiwa vita viliendelea, wengi waliamini kwamba hali inayowezekana ya siku iliyofuata haikuwa kutwaliwa na upinzani, lakini kuingia kwa nchi katika machafuko na uasi.

"Haiwezekani kwamba utawala wa Iran utaangushwa kupitia upinzani wa ndani. Utawala unasalia kuwa na nguvu nyumbani na utaongeza ukandamizaji wa nyumbani dhidi ya upinzani," anasema Prof Khatib.

Raia wa Iran sasa wanahofia kubanwa zaidi na serikali. Takriban watu sita wamenyongwa katika muda wa wiki mbili zilizopita tangu kuanza kwa vita na Israel kwa tuhuma za kuifanyia ujasusi Israel. Maafisa wanasema wamewakamata takriban watu 700 kwa madai hayo.

Mwanamke mmoja wa Iran aliiambia BBC Kiajemi kile anachohofia zaidi ya kifo na uharibifu wa vita ni utawala ambao umejeruhiwa na kufedheheshwa na sasa unageuza hasira yake dhidi ya watu wake.

"Ikiwa serikali haitaweza kusambaza bidhaa na huduma za kimsingi, basi kutakuwa na kuongezeka kwa hasira na kufadhaika," anasema Prof Ansari.

"Ninaona kama mchakato wa hatua. Sioni kama kitu ambacho, kwa maana ya wengi, kitakita mizizi hadi muda mrefu baada ya kumalizika kwa shambulio la mabomu."

Watu wachache nchini Iran wanafikiri kwamba usitishaji vita ulioandaliwa Jumatatu utadumu - na wengi wanaamini kuwa Israel bado haijakamilika kwa vile ina ubora kamili angani kuliko Iran.

Hifadhi za makombora ya balistiki ya Iran

Jambo moja ambalo linaonekana kuepukana na uharibifu huo ni maghala ya makombora ya balistiki ya Iran ambayo Israel ilipata vigumu kuyapata yakiwa yamewekwa kwenye vichuguu chini ya milima kote nchini.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel, Eyal Zamir, alisema Israel ilianzisha mashambulizi yake dhidi ya Iran ikijua kwamba "Iran ilikuwa na makombora 2,500 ya ardhi hadi angani". Makombora ambayo Iran ilirusha yalisababisha vifo na uharibifu mkubwa Israeli.

Israel itakuwa na wasiwasi kuhusu makombora 1,500 ambayo bado yako mikononi mwa Iran.

Pia kuna wasiwasi mkubwa katika miji ya Tel Aviv, Washington na miji mikuu mingine ya Magharibi na kikanda kwamba Iran bado inaweza kuharakisha kutengeneza bomu la nyuklia, jambo ambalo imeendelea kukanusha kujaribu kufanya.

Ingawa vituo vya nyuklia vya Iran vimepata pigo, na vikafanywa kuwa visivyofaa wakati wa milipuko ya mabomu ya Israel na Marekani, Iran ilisema imehamisha hazina yake ya Uranium iliyorutubishwa hadi mahali salama pa siri.

Hifadhi hiyo ya 60% ya Uranium, ikiwa itarutubishwa hadi 90%, ambayo ni hatua rahisi, inatosha kwa takriban mabomu tisa, kulingana na wataalam.

Muda mfupi kabla ya vita kuanza, Iran ilitangaza kwamba ilikuwa imejenga kituo kingine kipya cha siri kwa ajili ya kurutubisha ambacho kilipaswa kutangazwa hivi karibuni.

Bunge la Iran limepiga kura ya kupunguza vikali ushirikiano wake na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA.

Hili bado linahitaji kibali, lakini kama litapita Iran itakuwa imesalia hatua moja kuondoka kwenye Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia, NPT - huku watu wenye msimamo mkali wanaomuunga mkono kiongozi mkuu wakishinikiza kutengenezwa kwa silaha za nyuklia.

Ayatollah Khamenei sasa anaweza kuwa na imani kwamba utawala wake umesalia, tu. Lakini akiwa na umri wa miaka 86 na asiye na afya njema, anajua pia kwamba siku zake mwenyewe zinaweza kuhesabiwa, na anaweza kutaka kuhakikisha uendelevu wa utawala na mpito wa mamlaka kwa utaratibu - kwa mhubiri mwingine mkuu au hata baraza la uongozi.

Vyovyote vile itakavyokuwa, makamanda wakuu waliosalia na Walinzi wa Mapinduzi ambao wamekuwa watiifu kwa kiongozi mkuu wanaweza kutaka kuchukua madaraka nyuma ya pazia.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla