Bomu la pekee duniani linaloweza kuharibu kituo cha nyuklia cha Iran cha Fordo

    • Author, Luis Barrucho na Abdalla Seif Dzungu
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kiwanda cha siri cha Iran cha kurutubisha uranium cha Fordow kimezikwa chini kabisa ya mlima, huku vituo vyake muhimu vikilindwa na tani juu ya tani za miamba.

Israel haijaficha nia yake ya kuharibu mpango wa nyuklia wa Iran, lakini bomu pekee linaloaminika kuwa na nguvu za kutosha kupenya kituo cha Fordow ni bomu la Marekani la "bunker buster" ambalo Waisraeli hawana kufikia sasa.

Siku ya Jumatatu, maafisa kadhaa wa Israel walitangaza kuidhibiti anga ya Iran.

Jeshi la IDF lililinganisha udhibiti wa anga ya Iran na uongozi wake wa anga ya medani zingine za mzozo na maadui wanaoegemea Iran, kama vile Gaza na Lebanon - ambapo Israeli inaendelea kushambulia kwa mabomu ipendavyo.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema siku ya Jumatatu kuwa udhibiti wa Israel wa anga ya Iran ni "ushindi mkubwa ".

Mshauri wa Usalama wa Taifa Tzachi Hanegbi alisema marubani wanaweza kufanya kazi "dhidi ya malengo mengi zaidi" ya Tehran, kutokana na uharibifu wa "mifumo mingi ya ulinzi wa anga ya taifa hilo.

Huku Rais Donald Trump akionekana kubadilisha msimamo kati ya kuitaka Iran ijadiliane na kutishia kulipiza kisasi "katika viwango ambavyo havijawahi kuonekana", mjadala sasa unageukia iwapo Marekani itaingizwa katika mzozo mwingine wa Mashariki ya Kati, bila shaka - jambo ambalo rais amekuwa akisema mara kwa mara kuwa hataki.

Kulingana na gazeti la New York Times, Iwapo Marekani itaamua kuunga mkono Israel moja kwa moja katika mashambulizi yake dhidi ya Iran, chaguo mojawapo kwa Washington litakuwa kutoa mabomu ya "bunker-buster" yanayoaminika kuwa muhimu kuharibu kwa kiasi kikubwa kinu cha kurutubisha mafuta ya nyuklia cha Fordo.

Bomu kama hilo litalazimika kurushwa kutoka kwa ndege ya Marekani, ambayo inaweza kuwa na athari kubwa, ikiwa ni pamoja na kuhatarisha nafasi yoyote ya Iran kushiriki katika mazungumzo yanayotarajiwa ya Trump juu ya mpango wake wa nyuklia.

Lakini je, bomu hili ni hatari kiasi gani na lina uwezo gani?

Pia unaweza kusoma

Lifahamu bomu la Marekani la 'Bunker Bluster'

Miongoni mwa silaha zinazoweza kushambulia maeneo ya chini ya ardhi ya Iran ya nyuklia, moja bado haijatumika - na hipo kwenye mikono ya Israel kwa sasa: GBU-57A/B Massive Ordnance Penetrator, ni bomu kubwa zaidi kwa jina "bunker buster" lisilo la nyuklia ya nyuklia linalomilikiwa na Marekani pekee.

Silaha hii inayoongozwa kwa usahihi, yenye uzito wa kilo 13,600 inaweza kupenya kwenye kiwanda cha kurutubisha mafuta ya nyuklia cha Iran cha Fordo, ambacho kimezikwa ndani kabisa ya mlima.

Lakini ina changamoto gani na je, inaweza kutumika dhidi ya Iran?

Kwa mujibu wa serikali ya Marekani, GBU-57A/B ni "silaha kubwa ya kupenya yenye uwezo wa kushambulia mahandaki na vichuguu vilivyozikwa katika kina kirefu."

Ikiwa na urefu wa mita sita, inaaminika kuwa na uwezo wa kupenya takriban futi 200 (mita 61) chini ya ardhi kabla ya kulipuka. Mabomu mengi kama hayo yanaweza kurushwa kwa mfululizo, kwa ufanisi ili kuchimba zaidi kila yanavyolipuka.

Bomu hilo Iimetengenezwa na kampni ya Boeing, na kwamba halijawahi kutumika katika mapigano lakini imejaribiwa katika ardhi ya makombora ya White Sands, eneo la majaribio la kijeshi la Marekani katika jimbo la New Mexico.

Silaha hiyo ina nguvu zaidi kuliko Massive Ordnance Air Blast (MOAB), bomu lenye uzito wa pauni 21,600 (kilo 9,800) linalojulikana kama "Mama wa Mabomu Yote," ambalo illitumika katika mapigano nchini Afghanistan mnamo 2017.

"Jeshi la Wanahewa la Marekani liliweka juhudi kubwa katika kuunda silaha za ukubwa sawa na MOAB, lakini kwa vilipuzi vilivyomo ndani ya chuma chake ilikuwa vigumu sana.

Matokeo yake yalikuwa ni bomu hilo linaloweza kupenya kina kirefu chini ya ardhi la GBU-57A/B," anasema Paul Rogers, profesa mstaafu wa Mafunzo ya Amani katika Chuo Kikuu cha Bradford nchini Uingereza.

Hivi sasa, ni ndege aina ya US B-2 Spirit pekee - inayojulikana kama mshambuliaji wa siri - inayoweza kubeba bomu hilo. Ndege hii, ambayo mara nyingi hujulikana kama B-2, hutengenezwa na Northrop Grumman na ni mojawapo ya ndege za kivita za hali ya juu zaidi katika safu ya silaha za Jeshi la Anga la Marekani.

Kulingana na mtengenezaji, B-2 inaweza kubeba mzigo wa pauni 40,000 (kilo 18,000). Hata hivyo, Jeshi la Wanahewa la Marekani limesema limefanikiwa kuifanyia majaribio ndege hiyo aina ya B-2 iliyobeba mabomu mawili ya GBU-57A/B - yenye uzito wa karibu pauni 60,000 (kilo 27,200).

Ndege hii nzito ya masafa marefu ina uwezo wa kusafiri umbali wa maili 7,000 (kilomita 11,000) bila kujaza mafuta, na hadi maili 11,500 (kilomita 18,500) ikiwa na ujazo mmoja - kuiwezesha kufikia karibu sehemu yoyote duniani ndani ya masaa, kulingana na Northrop Grumman.

Prof. Rogers anasema kwamba kama MOP ingewahi kutumika dhidi ya adui mwenye ulinzi wa kisasa wa anga, kama Iran, ndege za B-2 zinaweza kushirikiana na ndege nyingine. Kwa mfano ndege ya F-22 ya siri inaweza kutumika kukandamiza ulinzi wa adui, ikifuatiwa na ndege zisizo na rubani kutathmini uharibifu na kubaini ikiwa mashambulio zaidi yalihitajika.

Anakadiria kuwa Marekani ina akiba ndogo ya mabomu haya ya MOP.

"Pengine wana hifadhi ya mabomu 10, au labda mabomu 20 kwa ujumla," anasema.

Je, bomu la 'Bunker Buster' au MOP litatumika dhidi ya kituo cha Fordo Iran?

Fordo ni kituo cha pili cha kurutubisha nyuklia cha Iran, baada ya Natanz, ambacho ndio kituo chake kikuu.

Imejengwa kando ya mlima karibu na mji wa Qom, kama maili 60 (kilomita 95) kusini magharibi mwa Tehran. Ujenzi unaaminika ulianza karibu 2006, na kituo hicho kilianza kufanya kazi mwaka 2009 - mwaka huo huo Tehran ilikubali uwepo wake hadharani.

Mbali na kuzikwa takriban mita 80 (futi 260) chini ya mwamba na udongo, Fordo inaripotiwa kulindwa na mifumo ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani ya Iran na Urusi.

Mnamo mwezi Machi 2023, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) liligundua chembechembe za uranium zilizorutubishwa hadi 83.7% - karibu kiwango cha silaha utengenezaji - kwenye eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa lengo la kuishambulia Iran ni kuondoa mpango wake wa makombora na nyuklia ambao aliutaja kuwa ni tishio lililopo kwa Israel.

Maafisa wamesema kuwa Fordo ni sehemu ya lengo hilo.

"Operesheni hii yote... inabidi ikamilishwe kwa kuondolewa kwa Fordo," Yechiel Leiter, balozi wa Israel nchini Marekani, aliiambia Fox News siku ya Ijumaa.

Lakini Israel haina uwezo wa kupeleka MOP peke yake, na Marekani haitaruhusu matumizi yake bila kuhusika moja kwa moja, anasema Prof. Rogers.

"Kwa hakika hawakuwaruhusu Waisraeli wafanye wao wenyewe. Na Israeli haina silaha zinazoweza kupenya kina hicho ."

Iwapo Marekani itapeleka bomu hili inategemea sana nia yake ya kuongeza ushiriki wake - hasa chini ya uongozi wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Prof. Rogers anaongeza: "Inategemea sana ikiwa Trump atainama kabisa kuwasaidia Waisraeli."

Katika mkutano wa G7 nchini Canada, Trump aliulizwa itachukua nini kwa Washington kujihusisha kijeshi. Akajibu:

"Sitaki kuzungumza juu ya hilo."

Katika mahojiano ya hivi majuzi na ABC News, Balozi Leiter aliulizwa kuhusu uwezekano wa Marekani kuhusika katika shambulio dhidi ya Fordo. Alisema kuwa Israel imeiomba Marekani tu msaada wa kujihami.

"Tuna matukio kadhaa ya dharura ... ambayo yatatuwezesha kukabiliana na Fordo," alisema.

"Sio kila kitu ni suala, unajua, kupanda angani na kulipua mabomu kutoka mbali."

Iran imekuwa ikisema kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani kabisa na kwamba haijawahi kutaka kutengeneza silaha za nyuklia.

Lakini wiki iliyopita bodi ya magavana wa mataifa 35 ya IAEA ilitangaza rasmi Iran ilikiuka wajibu wake wa kutoeneza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20.

"Silaha hii ina nafasi nzuri zaidi ya kuharibu uwezo wa nyuklia wa Iran chini ya ardhi kuliko silaha nyingine yoyote iliyopo kwa sasa. Lakini kama inaweza kufanya hivyo - ni nani anayejua?"

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla