Mkuu wa jeshi la Kenya afariki dunia katika ajali ya helikopta

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili, Nairobi

TH

Chanzo cha picha, MOD

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya Francis Ogolla amefariki.

Rais William Ruto ametangaza kifo cha Ogolla pamoja na maafisa wengine 9 wa jeshi huku wawili wakinusuruka.

Ogolla alifariki baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maafisa wengine kuanguka Kaben, Marakwet Mashariki siku ya Alhamisi.

Ogolla alichukua nafasi ya kuongoza jeshi mnamo Aprili 28, 2023.

Walioshuhudia walisema kuwa ilishika moto wakati wa kuanguka.

Eneo hilo lilizingirwa mara baada ya ajali hiyo.

Maafisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo kabla ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi kukabiliana na wezi wa mifugo katika eneo hilo.

Helikopta hiyo ya jeshi la Anga la Kenya aina ya Huey ilikuwa imetoka katika shule moja ya msingi ya eneo hilo ilipoanguka na kuwaka moto.

Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi, akichukua hatamu kutoka kwa mtangulizi wake Jenerali Robert Kibochi.

Kibochi alimkabidhi Ogolla kama Mkuu wa majeshi baada ya kufikisha umri wa kustaafu .

Siku tatu za maombolezo

th

Chanzo cha picha, KDF

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Akitangaza kifo cha Jenerali Ogolla rais Ruto amesema kutakuwa na siku tatu za maombolezo kuanzia Ijumaa tarehe 19 Aprili ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwa kipindi hicho .

Amemtaja Jenerali Ogolla kama afisa shupavu aliyefariki akiwa kazini.

Maafisa hao walikuwa wamesafiri hadi eneo la kaskazini mwa Kenya ambalo limekuwa likikumbwa na visa vya wizi wa mifugo.

Walikuwa kwenye shughuli ya kufungua tena baadhi ya shule zilizofungwa kufuatia mashambulizi ya majambazi. Pia walitembelea maafisa wa kijeshi waliotumwa kuleta utulivu katika eneo hilo.

Jenerali Francis Ogolla alikuwa afisa mkuu wa kijeshi wa Kenya na mshauri mkuu wa kijeshi wa Rais na Baraza la Mawaziri.

Aliteuliwa na Rais Ruto Aprili mwaka jana baada ya kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Katika ajali hiyo maafisa wengine wamepoteza maisha ni;

1. Brigedia Swale Saidi,

2. Kanali Duncan Keittany,

3. Luteni Kanali David Sawe,

4. Meja George Benson Magondu,

5. Kapteni Sora Mohamed,

6. Kapteni Hillary Litali,

7. Sajenti Mwandamizi John Kinyua Mureithi,

8. Sajenti Cliphonce Omondi, na

9. Sajenti Rose Nyawira.