Yakuza: Ni ipi asili ya genge la kimafia la Japani?

z

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Yakuza, taasisi kongwe zaidi ya uhalifu duniani, hutumia kanuni za heshima, mila, tamaduni na alama zinazoifanya kuwa ya kipekee ikilinganishwa na mitandao mingine ya uhalifu kama vile makundi ya Amerika Kusini au mafia wa Italia na Urusi.

Yakuza inaundwa na vyama vya wafanyakazi 25 au "familia," ikiwa ni pamoja na familia tatu kuu. Mamia ya vikundi vidogo vidogo hufuata amri za uongozi mkuu.

Iliundwa zaidi ya karne nne zilizopita huko Japan na mabwana wakubwa na maaskari za zamani. Yakuza waliishi enzi yao ya dhahabu kati ya miaka ya 1960 na 1980, wakati idadi yao ilipokuwa zaidi ya wanachama 180,000.

Kupungua kwake kasi ni kutokana na maendeleo ya sasa, na kubinywa kisheria, na kufanya idadi ya wanachama kupungua hadi 10,000.

Mambo manne ili kuelewa taasisi hii ya uhalifu ambayo inajitahidi kuishi bila kupoteza asili yake katika karne ya 21.

Jina na asili

as

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Picha ya 1895 ya mwanachama wa Yakuza.

Neno Yakuza linatokana na nambari 8, 9 na 3, zinazotamkwa kwa Kijapani ya, ku, sa).

Yakuza iliibuka katika karne ya 17 miongoni mwa vikundi vya jamii ya Kijapani kama vile bakuto (wacheza kamari na wasafiri), tekiya (wachuuzi) na askari wa zamani wasio na kazi (sumarai).

Tekiya na bakuto walichukua mila kadhaa za samurai, ikijumuisha kanuni kali za heshima na ibada za uaminifu, na hayo yakawa muhimu katika tamaduni na muundo wa Yakuza.

Maadili na mila zao

SD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Kundi la Yakuza huko Tokyo 1960.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yakuza ina mfumo mgumu wa maadili na itikadi. Maadili haya yalianzishwa karne nyingi katika jamii ya Wajapani, yakipenya tabaka zake zote, kutoka vitongoji na Tokyo mji mkuu wa Japani, na kwenye biashara halali hadi zisizojulikana.

"Yakuza wanashikilia kanuni za heshima za uanaume. Ni wazo la 'kuishi na kufa kama mwanaume,” anasema mwanasosholojia Noboru Hirosue, mwandishi wa vitabu kadhaa kuhusu mafia wa Japani.

Wanachama wa taasisi hiyo “wanaamini ni lazima wajiweke wakfu, kimwili na kiakili, na wanaona ni jambo la heshima kuonyesha msimamo usioyumba, hata kufikia hatua ya kutoa kafara uhai wao inapohitajika,” anasema Hirosue.

Kiini cha itikadi ya Yakuza ni kanuni ya heshima itokanayo na dhana ya giri (wajibu) na ninjo (ubinadamu).

Giri ni deni la heshima ambalo mwanachama anadaiwa na mkuu wake, hiyo ni sehemu muhimu ya kuimarisha uaminifu ndani ya shirika.

Wkati ninjo ni huruma kwa wengine ambayo hutumika kama kipingamizi cha ukali wa giri katika muundo wa mafia.

Zote mbili zimeegemezwa kwenye roho ya kujitolea, ambayo inawaongoza wanachama wake kuweka masilahi ya kikundi juu ya yale ya kibinafsi.

Mfano wa hili ni tambiko la yubitsume, ambapo mwanachama hukata kipande cha kidole chake (kwa kawaida kidole kidogo). Kama kitendo cha toba au kuomba msamaha kwa Oyabun (mkuu) wake kwa kosa lake mwenyewe au la mtu aliye chini ya jukumu lake.

C

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wanachama wengi wa zamani wa Yakuza waliweka vidole vya bandia ili kuunganishwa tena na jamii ya Wajapani, kwani kidole kilichokatwa hubeba unyanyapaa mkubwa.

"Ijapokuwa kupoteza kidole kwa sababu ya kosa kunaweza kuwa chanzo cha aibu, lakini vilevile kutoa kidole kama malipo ya kosa inachukuliwa kuwa jambo la heshima," anaelezea Hirosue.

Tamaduni hii, hata hivyo, inazidi kupungua na siku hizi wanachama kwa kawaida hulipa faini za kifedha ili kukomboa makosa yao.

"Vikundi vya Yakuza vimeundwa katika uhusiano wa kifamilia ambapo wakubwa wanaitwa aniki, kaka za bosi huitwa oniisan au wajomba, na mke wa bosi anaitwa anesan au dada mkubwa," anaeleza Hirosue.

Mashirika haya hayana itikadi rasmi ya kisiasa. Lakini Martina Baradel, mtafiti kuhusu uhalifu wa Japan kutoka Chuo Kikuu cha Oxford anasema:

"Itikadi ya Japan kwanza, mila za samurai, heshima na utukufu wa falme za zamani – hizi hujitokeza zaidi katika siasa za mrengo wa kulia, kwahivyo kuna uhusiano wa kiitikadi."

Baradel anaongeza, Yakuza mara kwa mara hushirikiana na vyama vya siasa vya kihafidhina, ingawa kwa kawaida vyama hivyo hukataa uhusiano wowote na mafia ili kudumisha sura yao safi.

Uhalali wa kisheria na shughuli zao

AS

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wanachama wa Yamaguchi-gumi, mojawapo ya familia kuu ya Yakuza, wakihudhuria mazishi ya Oyabun wao 2002.

Tofauti na mashirika ya uhalifu katika sehemu nyingine za dunia, Yakuza haijawahi kuwa kinyume cha sheria, ingawa inakabiliwa na sheria zinazozidi kuweka vikwazo na zinatatiza shughuli zake.

"Mafia wa Italia ni wa siri kabisa, huku Yakuza wapo dhahiri," anasema Hirosue.

Taasisi hii ya uhalifu inanufaika na haki ya ushirika huria – iliopo katika Katiba ya Japan katika kifungu chake cha 21.

"Ilimradi hazitishii usalama wa taifa, maadili ya umma au utaratibu - haziko chini ya marufuku ya serikali," msomi huyo anaeleza.

Hadi mwisho wa karne ya 20, makao makuu mengi ya Yakuza yalikuwa na mabango mlangoni, yalisajiliwa katika taarifa mbalimbali, na wanachama wao walitoa kadi za biashara kwenye mikutano kana kwamba walikuwa wafanyakazi wa kampuni fulani.

Lakini hali haiko tena hivyo. Katika miongo mitatu iliyopita serikali ya Japan imeimarisha sheria ili kudhoofisha ufadhili wa vikundi vya wahalifu, kuwatenga, kuzuia shughuli zao na kupunguza ushawishi wao kwa jamii.

Ingawa bado uwepo wa Yakuza ni halali, lakini wanachama wake daima wako chini ya uchunguzi wa siri wa mamlaka.

"Mtu anapofanya uhalifu na kufunguliwa mashtaka, ikiwa ni mwanachama wa Yakuza, anapokea hukumu ndefu kuliko mtu mwingine kwa uhalifu huo," anaelezea Martina Baradel.

Yakuza hujihusisha na nini hasa?

SD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Ingawa Yakuza ni halali, polisi wa Japani hufuatilia wanachama wake.

Huko zamani mtandao huo uliendesha biashara katika kamari, kujipatia pesa kwa vitisho, malipo ya ulinzi, ukusanyaji wa madeni, mikopo haramu, mashirika ya ukahaba na ulanguzi wa dawa za kulevya, miongoni mwa mengine.

Hirosue anaelezea kuwa wanachama pia walijhusisha na biashara halali kama vile mali isiyohamishika, ujenzi, usafirishaji au biashara ya hisa.

Hata hivyo, kuimarishwa kwa sheria dhidi ya uhalifu wa kupangwa, hasa sheria mbili za 1992 na 2010 na kutoa adhabu kubwa, zimebadilisha mwenendo wa mafia wa Kijapan.

"Taratibu wamekuwa hawaonekani na wala hawajuulikani, wakijihusisha na uhalifu kama vile udanganyifu, wizi na ujambazi. Kwa maneno mengine, mbinu ambazo Yakuza wanapata mapato yao zimetoka kuwa vitisho hadi kuwa udanganyifu," anasema Baradel.

Anaongeza "katika siku za hivi karibuni wameshirikiana na vikundi vinavyojulikana kama hangure kufanya shughuli kama vile udanganyifu, wizi, ujambazi, biashara ya dawa za kulevya na biashara haramu ya binadamu."

Sheria za kupinga Yakuza zimeweza kuharibu taasisi, lakini wakati huo huo hufanya iwe vigumu kwa wanachama wanaoamua kuondoka katika kundi hilo kuunganishwa katika jamii.

Kifungu kinachojulikana kama "kifungu cha miaka 5," ambacho kinakataza kampuni na watu binafsi kufanya malipo kwa wanachama wa Yakuza, hufanya iwe vigumu kwa wale ambao wameacha taasisi hiyo karibuni kufungua akaunti za benki, kukodisha nyumba au hata mkataba wa huduma ya mawasiliano ya simu ya mkononi.

"Kwa sababu hiyo, wanakuwa watu wa pembezoni wenye chuki na jamii," anasema Hirosue.

Michoro ya mwili, alama na silaha

DF

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Ni mara chache Yakuza huonyesha tattoo zao hadharani, na mojawapo ya matukio haya ni tamasha la Sanja Matsuri katika kitongoji cha zamani cha Asakusa huko Tokyo.

Sanaa ya kuchora tatuu, inayojulikana kama irezumi, ni mojawapo ya alama zinazotambulika za Yakuza.

"Katika tamaduni za Kijapan, tatuu zilihusishwa na kazi hatari kama wachimbaji wa makaa ya mawe na wavuvi. Sababu ilikuwa, katika ajali ambazo uso hautambuliki, wanaweza kumtambua mwathirika kwa mchoro,” anasema Hirosue.

Lakini, kadiri karne zilivyopita, zikawa ni alama za kipekee za uhalifu uliopangwa.

Michoro ya samaki, dragoni, mashujaa wa sumaria, maua na michoro mingine ya jadi ya Kijapani – yana maana za kipekee kuhusu mafanikio au hadithi ya maisha, pamoja na kujitolea kwao kwa kundi la uhalifu.

"Hapo awali michero ilikuwa na maana ya kutangaza kiapo cha kutorudi katika jamii na kuishi kama Yakuza maisha yote baada ya kujiunga," mtaalamu huyo anasema.

Tatuu hazipendelewi nchini Japan, zinahusishwa na uhalifu, na watu waliojichora tatuu wamepigwa marufuku katika maeneo mengi ya umma, kuanzia sauna na mabwawa ya kuogelea hadi fukwe.

S

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Joka na mapigano ni michoro maarufu katika tatuu za Yakuza.

Mbali na tatuu, Yakuza hutumia alama, bendera, na vipengele vingingine kujitambulisha kama wanachama na kuonyesha uaminifu wao.

Michoro hii ni pamoja na mambo ya asili na imani za Kijapani zenye maana maalumu ndani ya utamaduni wa Yaakuza kama vile uaminifu, nguvu, au uwezo wa kushinda dhiki.

Kipengele kingine kinachotofautisha mafia wa Kijapani na wale wa nchi nyingine ni kwamba hawatumii sana silaha za moto na wanafanya vurugu kidogo ikilinganishwa, na wale wa Amerika ya Kusini.

"Ni mara chache sana wanatumia bunduki kutokana na adhabu kali wanazopata, na wanapotumia silaha, hutumia silaha za visu au panga," anasema Hirosue.

“Wanapotaka kutumia nguvu za kimwili, kama vile vitisho, wanaweza kutaja tu jina la kikundi chao ili kuwa na mamlaka,” anasema mtaalamu huyo.

Hata hivyo, anabainisha, Yakuza wanapoamua hasa kufanya vurugu, matokeo yanaweza kuwa vifo na majeruhi.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah