Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ifahamu sumu ya chura iliyotumika kumuua kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny
Kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny aliuawa kwa kutumia sumu ya ''Dart Frog'' inayopatikana katika chura wanaopatikana Amerika Kusini, Uingereza na maeneo mengine ya Ulaya.
Sumu aina ya epibatidine ilipatikana katika sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mwili wa Navalny ambayo ilichangia kufariki kwake katika gereza moja nchini Urusi miaka miwili iliyopita, ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza ilisema.
Washirika wake walisema Urusi pekee ndio ina 'uwezo, motisha na nafasi' ya kutumia sumu hiyo.
Ikulu ya Kremlin imetupilia mbali uchunguzi huo na kuutaja kama 'kampeni ya kueneza habari' kulingana na shirika la habari la Tass News.
Sumu hiyo ni nini?
Epibatidine ni sumu inayopatikana kwenye chura aina ya ''dart frog'' kulingana na mtaalam wa sumu Jill Johnson.
''Inanguvu mara mia mbili zaidi kushinda Morphine'', aliiambia BBC Idhaa ya Urusi.
Epibatidine hupatikana wa kwa aina ya chura za 'dart frogs' na pia inaweza kuzalishwa kwenye maabara.
Chura hao wakiwa wamezuiliwa hawawezi kutoa sumu hiyo, na aidha sumu hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Urusi, washirika wa Ulaya walisema katika taarifa yao.
Speshi za Anthony's poison arrow frog na Phantasmal poison frog, ni aina za vyura ambazo hutoa sumu hiyo kupitia ngozi yao.
Ingawa epibatidine imechunguzwa na kupatikana kuwa inaweza kupunguza maumivu na uvimbe wa mapafu, huwa haitumiki katika matibabu kutokana na sumu iliyonayo.
Sumu ya chura 'dart frog' inafanyaaje kazi?
Sumu hii ina nguvu na huathiri mfumo wa neva, kulingana na Johnson.
Husisimua vipokei vya neva, na ikiwa itatumika sahihi, husababisha misuli kutetemeka, kupooza,kifafa, mipigo ya moyo kupungua, matatizo ya kupumua na baadaye kifo cha ghafla.
Alastair Hay, Professa wa sumu na mazingira katika Chuo Kikuu cha Leeds, anasema athari zake ni kushindwa kupumua na ''yeyote anayepewa sumu hiyo hufa kwa kukosa hewa''.
Sumu hiyo kupatikana kwa mwili wa mtu ''kunaashiria kuwa alipewa kimakusudi,'' aliongezea.
Upatikanaji wa sumu hii
Sumu ya Epibatidine haipatikani kwa urahisi, na hupatikana katika eneo moja la kijiografia duniani na kwa kiwango kidogo sana, anaelezea Johnson.
Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza, sumu iliyotumika ilikuwa ya Anthony's poison arrow frog, speshi ambayo inapatikana tu katika mataifa ya Ecuador na Peru.
Vyura hao huzalisha kemikali hiyo kwa kula vyakula sahihi zinazozalisha alkaloids ambazo hufanya sumu ya epibatidine kujikusanya kwenye ngozi.
Iwapo lishe ya vyura hao itabadilika, sumu hiyo ya epibatidine huisha.
"Kupata chura wa porini katika sehemu hiyo, inayokula chakula stahili ya kutengeneza alkaloids, ni vigumu, si rahisi'',alisema Johnson
"Hii ni njia ya kipekee ya kumpa mtu sumu. Kisa kingine cha sumu ya epibatidine ninayo ijua ilikuwa ya maabara na haikuwa na mauti'
Urusi imesema nini?
Maabara za Ulaya zimedhibitisha kuwa Navalny alifariki kutokana na sumu hiyo ya kipekee, washirika hao walisema .
Moscow awali ilikuwa imesema Navalny alifariki kutokana na sababu za kiasili , ila mke wake Yulia Navalnaya, alikuwa akipinga hoja hiyo na kusema mumewe 'aliuawa' kwa kupewa sumu.
Ubalozi wa Urusi mjini London ulikanusha madai kuwa Moscow ilihusika na kifo cha Navalny.
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Maria Zakharova, kupitia shirika la habari la kitaifa nchini Urusi la Tass News alisema "maneno yote yanayosemwa na taarifa zinazotolewa na kampeni ya habari ya kuwazubaisha watu kutoka kwa matatizo yanayoikumba mataifa ya magharibi"
Wakati wa kifo chake, Navalny alikuwa amefungwa jela kwa miaka mitatu.
Kulingana na Urusi, kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 47, alitembea kwa muda mfupi na kusema hahisi salama kisha akazirai na hakuamka tena.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi