Kinachojulikana kuhusu kifo cha Alexei Navalny, mwanasiasa wa Urusi ambaye alimpinga Putin

Toleo rasmi linasema kwamba Ijumaa wiki hii Alexei Navalny alifanya matembezi mafupi katika gereza Siberia ambapo alifungwa, alisema alijisikia vibaya, kisha akaanguka na hakupata tena fahamu.

Mpinzani huyo mkuiu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi alikuwa na umri wa miaka 47.

Hali yake ilikuwa mbaya zaidi kwa muda wa miaka mitatu aliyokaa gerezani, ambapo alilalamika kwamba alinyimwa matibabu na alifungwa karibu siku 300 katika kifungo cha upweke.

Wakati wa kukamatwa kwake mnamo Januari 2021, alikuwa alikaa miezi kabla ya kupona kutokana na shambulio la neva.

Bado, alionekana kuwa na ari na afya njema katika video ya mahakama iliyorekodiwa siku moja kabla ya kifo chake.

Maoni ya kimataifa hayaonekani kukubaliana na maelezo ya Urusi kuhusu kile kilichomtokea katika IK-3 , au "Polar Wolf" , mojawapo ya jmagereza ya kaskazini na yenye ulinzi mkali zaidi ya Urusi.

Mnamo mwezi Disemba alikuwa amehamishiwa kwenye gereza hili maarufu la Aktiki, maelfu ya kilomita kaskazini-mashariki mwa Moscow.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné alisema Navalny "alilipia maisha yake" kwa "upinzani wake dhidi ya ukandamizaji wa Urusi" , akiongeza kuwa kifo chake kilikuwa ukumbusho wa "uhalisia wa utawala wa Vladimir Putin".

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema nchini Urusi "roho huru huhukumiwa kifo ," wakati mwenzake wa Marekani , Joe Biden , alisema kuwa "Putin ndiye anayehusika na kifo cha Navalny . "

Mamake yake Navalny, Lyudmila, anasema katika chapisho la Facebook lililonukuliwa na gazeti la Novaya Gazeta kwamba mwanawe alikuwa "hai, mwenye afya na mwenye furaha" alipomwona mara ya mwisho mnamo Februari 12.

"Kwa kweli hatuwezi kumwamini Putin na serikali yake," Yulia, mke wake alisema.

Vyombo vya habari vya Urusi vinasema nini kuhusu kuanguka kwake

Shirika la habari la Urusi Interfax liliripoti kwamba madaktari walitumia nusu saa kujaribu kumzindua.

Kulingana na wakuu wa magereza, madaktari walikuwa wakimhudumia ndani ya dakika mbili na gari la wagonjwa lilipatikana ndani ya dakika sita.

Shirika la utangazaji la serikali RT, lililopigwa marufuku katika nchi nyingi za Magharibi, liliibua uwezekano kwamba aliufariki kutokana na kuganda kwa damu.

Msemaji wa Putin, Dmitry Peskov, alisema "madaktari lazima watatue hili kwa njia fulani."

Wazo lolote kwamba Kremlin inahusika na kifo cha Alexei Navalny "halikubaliki kabisa ," Peskov alisema, kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Urusi Tass.

Msemaji huyo alisema mwitikio wa viongozi wa nchi za Magharibi kwa kifo cha Navalny ulikuwa "wa kutisha."

Peskov pia alisema Ijumaa kwamba huduma ya magereza ya Urusi ilikuwa ikifanya "uchunguzi wote" juu ya kifo cha Navalny, lakini hawakuwa na habari zaidi juu yake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova alisema kwenye Telegram kwamba matokeo ya uchunguzi wa mwili kuhusu chanzo cha kifo cha Navalny bado hayajapatikana.

Spika wa Bunge la Urusi, Viacheslav Volodin, alizilaumu nchi za Magharibi kwa kifo cha mkosoaji huyo wa Kremlin.

"Wote, majina yao yanajulikana sana, kuanzia Katibu Mkuu wa NATO na viongozi wa Marekani hadi (Olaf) Scholz, (Rishi) Sunak na (Volodymyr) Zelensky wana hatia ya kifo cha Navalny," mwanasiasa huyo alisema katika kituo chake cha Telegram. .

Walau hadi saa 10 jioni kwa saa za ndani (17:00 GMT) hakuna uchunguzi wa maiti ulikuwa umefanywa.

Mashambulizi ya awali dhidi ya Navalny

Iwe ni kuzorota polepole, janga la ghafla au tukio moja lililomuua, Navalny alijua kwamba walitaka afe.

Mnamo Desemba 2020, alishutumu maajenti wa Huduma ya Usalama ya Shirikisho (FSB) kwa kumtia sumu.

Aliugua sana na kuanguka kwenye ndege iliyokuwa ikiruka kutoka Tomsk, Siberia, na kulazimisha ndege kutua kwa dharura huko Omsk wakati wafanyakazi wakitafuta msaada wa matibabu.

Maabara za Ulaya baadaye zitathibitisha kwamba Novichok , wakala wa neva uliotengenezwa na Urusi ambao pia ulitumiwa kuwatia sumu Sergei na Yulia Skripal huko Salisbury, Uingereza, ulipatikana katika mwili wake.

Katika simu isiyo ya kawaida, ambayo Navalny alirekodi, alimdanganya wakala wa FSB akiri kwamba silaha hiyo ya kemikali ilikuwa imewekwa kwenye nguo yake ya ndani katika hoteli ya Tomsk.

Ajenti Konstantin Kudryavtsev alisema kwamba ikiwa ndege hiyo isingetua kwa dharura, angekufa.

Baada ya matibabu nchini Ujerumani, Navalny alirudi Urusi mnamo Januari 2021 na alikamatwa papo hapo.

Hali mbaya gerezani

Afya yake ilizidi kuwa mbaya gerezani.

Katika miezi iliyofuatia kufungwa kwa Navalny, akishutumiwa kwa "itikadi kali" na "ufisadi", washirika wake na mawakili walitoa tahadhari kadhaa kwamba afya yake inazidi kuwa mbaya , kwamba alikuwa mgonjwa sana au kwamba haijulikani aliko.

Alilalamika kuhusu maumivu makali ya mgongo, homa na miguu yake kufa ganzi.

Alizungumzia kuhusu kukosa usingizi kutokana na walinzi kumulika mienge machoni mwaka na bado hakua amepata nafuu baada ya athari mbaya za shambulio la sumu ya Novichok.

Katika kuonekana kwake hadharani mara ya mwisho Januari 10, Navalny alitania kwamba alikuwa bado hajapokea barua yoyote ya Krismasi kwa sababu alikuwa "mbali kabisa."

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan, siku ya Ijumaa alielezea kifo cha Navalny kama "msiba mbaya" na mfano wa hivi punde wa "historia ndefu na chafu ya serikali ya Urusi ya kuwadhuru wapinzani wake."

"Hii inazua maswali ya kweli na dhahiri kuhusu kile kilichotokea hapa," aliendelea.

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema "imeshtushwa" na kifo hicho na kuongeza kuwa kinapaswa kuchunguzwa na chombo huru.

"Iwapo mtu atakufa katika kizuizi cha serikali," taarifa ya Umoja wa Mataifa inaongeza, "dhana ni kwamba serikali inawajibika."

"Jukumu hili linaweza kukanushwa tu kupitia uchunguzi usio na upendeleo, wa kina na wa uwazi unaofanywa na chombo huru," chombo hicho kilisema.

Kifo cha Navalny kinawanyima wapinzani wa Putin njia mbadala inayotambulika kimataifa, na labda ni onyo kubwa zaidi kwa wale wanaojaribu kuipinga Kremlin.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi