Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Alexei Navalny: Kwanini kumfunga Navalny kutampa taabu Rais Putin?
Wakati misururu mirefu ya polisi wa kudhibiti ghasia ikishika doria katikati mwa Moscow usiku wa Jumanne, ujumbe ulikuwa wazi: maandamano yote ya kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Alexei Navalny yangevunjwa.
Kwa saa chache zilizofuata, wale ambao walithubutu kuijaribu mamlaka walifukuzwa barabarani.
Picha za moja kwa moja za kukamatwa na polisi wanaotumia fimbo zao hivi karibuni zilianza kusambaa mitandaoni.
Matukio hayo yalikuja saa chache baada ya jaji kuamuru kwamba mkosoaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin atatumia miaka miwili ijayo akiwa gerezani.
Mbinu kali na matokeo yaliyo kinyume na matarajio
"Nadhani ni mwanzo tu wa shida kwa serikali, kwa sababu Navalny hakuwa tu nguvu ya kisiasa lakini pia maadili, ambayo inamfanya awe kivutio zaidi kwa wale ambao hawakuwa wafuasi wake hapo awali," anasema Andrei Kolesnikov, wa Carnegie Moscow.
"Sio tu upinzani wa kisiasa, lakini asasi za kiraia ndizo zinazokerwa na ukatili, tabia ya polisi na mahakama."
Kremlin kwa muda mrefu imekuwa ikimuelezea Navalny kama "wakala" wa Magharibi anayedhamiria kudhoofisha Urusi, huku ikisisitiza kuwa korti iko huru kabisa na kwamba waandamanaji wenye hasira ni "wahuni."
Msemaji wa Rais Putin alisifu vikosi vya usalama kwa kuwa "imara''
Lakini wengine hapa wanaonya kuwa mbinu ngumu zinaweza kuwa kinyume na matarajio.
"Ukandamizaji dhidi ya Alexei Navalny, ambao unashangaza kwa ukatili wake ... pia ni ujinga wa kushangaza," Filipp Styorkin aliandikia tovuti huru ya VTimes.
Anashikilia kuwa adhabu ya kifungo cha Navalny kitasababisha maandamano zaidi, sio kuwazuia. Hii sio namna bora kwa Kremlin katika nyakati za uchumi zisizo na uhakika.
Wengi katika maandamano ya barabarani wanasema waliingia mitaani kwa mara ya kwanza, sio kwa sababu ya Alexei Navalny lakini kwa sababu ya namna mbaya walivyomtendea.
Jumanne usiku baada ya kusikilizwa mahakamani, madereva katikati ya Moscow walipiga honi kwa mshikamano na wale wanaoandamana, wakiwa bado na woga sana kusimama na kujiunga nao.
Hiyo ni pamoja na ghadhabu kutokana na ufisadi wa kiwango cha juu ambao uchunguzi wa Navalny umebainisha, ambayo inakera haswa kwani Warusi wanaona maisha yao yanazidi kuwa magumu.
Gereza pengine si njia ya kumnyamazisha Navalny
Haijafahamika bado wimbi hili la maandamano litadumu kwa muda gani.
Wanaweza kupungua kwa kile kinachoweza kuwa hatua inayofuata ya mvutano: uchaguzi wa bunge mnamo msimu wa joto, wakati Navalny alikuwa na mipango ya "kukisambaratisha" chama kinachounga mkono Kremlin United Russia kwenye uchaguzi.
Timu yake sasa itajaribu kutekeleza mpango huo bila yeye.
"Itakuwa ngumu," mshirika wa Navalny Lyubov Sobol alikiri wiki iliyopita alipoulizwa ni vipi timu hiyo ingeweza kukabiliana ikiwa kiongozi wake atapelekwa gerezani.
"Alexei ni msukumo wetu. Lakini tutafanya kazi kwa shauku zaidi ikiwa itatokea, ikichochewa na hasira yetu."
Wanakabiliwa na mashtaka ya jinai, na labda kifungo cha gerezani, kwa kuwataka watu waandamane wakati wa janga la corona.
Navalny ni wazi atakuwa na wakati mgumu kukusanya wafuasi wake na kuongoza timu yake akiwa gerezani, hasa ikiwa mamlaka itaendelea na mashtaka dhidi yake.
Lakini mtu ambaye alinusurika shambulio la sumu kisha akarudi kuwakabili wale aliowalaumu ana uwezekano wa kunyamazishwa kabisa.
Simu za mkononi zimepigwa marufuku katika kambi za gereza za Urusi, lakini hupatikana kama kawaida, na Navalny ataweza kupiga simu zilizoidhinishwa mara kwa mara na kupokea wageni.
Wiki iliyopita, akiwa kizuizini kabla ya kesi, aliweza kutuma ujumbe kwenye Instagram kutoka gerezani akiwataka Warusi waondoe hofu yao na wafanye maandamano.