Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Kwa nini kuishambulia Iran ni hatari zaidi kuliko kumkamata Maduro?' - New York Times
Katika mapitio yetu ya magazeti, tunawasilisha maoni yanayojadili ongezeko la mvutano kati ya Marekani na Iran, ikiwa ni pamoja na uchambuzi unaozingatia kuilenga Tehran kuwa hatari kubwa kwa Trump kuliko kumkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, makala inayohoji uzito wa Washington kutumbukia kwenye vita na Iran, na hatimaye makala inayoangazia hatua kali za China za kupunguza shughuli za kijasusi za Marekani na Ulaya ndani ya himaya yake.
Tunaanza ziara yetu na gazeti la Marekani la "The New York Times" na maoni yaliyoandikwa na Abdul Latif Daher na Samuel Granados yenye kichwa "Kwa nini Kuilenga Iran ni Hatari Kuliko Kumkamata Maduro?"
Waandishi hao wawili wanaanza kwa kudokeza kwamba uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran, pamoja na mtandao wake mpana wa vikosi vya washirika katika eneo hilo, huenda ukaisukuma Marekani katika mzozo wa muda mrefu.
Waandishi hao wanasema kwamba wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipotangaza Januari iliyopita kwamba "meli" ya Marekani ilikuwa ikielekea Iran, alilinganisha na mtindo wa nguvu uliotumika wakati wa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela ambayo yalisababisha kukamatwa kwa Maduro na mkewe.
Hivi sasa, kulingana na waandishi hao, wakati Trump anazingatia chaguzi nyingi kuelekea Tehran, pamoja na mashambulizi madogo, wataalam wanaonya kwamba shambulio lolote dhidi ya Iran litakuwa gumu zaidi kuliko operesheni ya Venezuela na linaweza kusababisha Marekani kujiingiza katika mzozo wa muda mrefu, kwa sababu Iran ina uwezo mkubwa wa kijeshi, pamoja na mtandao wa vikosi washirika katika eneo ambalo linaweza kusaidia upinzani endelevu kwa muda.
Waandishi hao wanahoji kuwa, tofauti na ilivyotokea Venezuela, Trump anaonekana kufikiria uwezekano wa kufanya operesheni pana zaidi ya kijeshi, bila kueleza wazi malengo yanayotarajiwa ni yapi, lakini ametangaza nia yake ya kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia, huku akiona kwamba mabadiliko ya utawala ni "jambo bora zaidi linaloweza kutokea."
Wakati anga ya Venezuela ilikuwa haina mifumo ya ulinzi kabla ya shambulio la Marekani, Iran inamiliki mojawapo ya maghala makubwa na tofauti ya makombora katika Mashariki ya Kati, kulingana na wataalam wa kikanda.
Silaha hizi zinajumuisha ndege zisizo na rubani na mifumo ya kuzuia meli, lakini ukubwa halisi wa hifadhi yake ya makombora bado haujulikani baada ya mzozo wa siku 12 na Israeli mnamo Juni.
Waandishi hao walimnukuu Sanam Vakil, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Chatham House, ambaye alibainisha kuwa mkakati wa Tehran "unategemea kuongezeka kwa kasi kwa mzozo na kukosekana kwa utulivu katika eneo kubwa la kanda hiyo, ili gharama na athari zienee."
Mataifa ya Ghuba, ambayo yana kambi za Marekani, pia yana wasiwasi kuhusu shambulio lolote la kijeshi la Marekani ambalo linaweza kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran kwenye ardhi yao.
Mnamo mwezi Januari, Saudi Arabia na UAE, washirika wa Washington, walitangaza kukataa kwao kuruhusu matumizi ya anga yao kwa mashambulizi.
Hatahivyo kulingana na wataalam, msimamo huu unaweza kutosheleza kuwalinda kutokana na majibu yoyote ya Iran.
Waandishi hao wanaamini kwamba ingawa washirika wengi wa Iran katika kanda hiyo wamekabiliwa na mapigo ambayo yamewadhoofisha sana, wanaweza kulipiza kisasi kwa kulenga vikosi vya Marekani na washirika wao, hatua ambayo inaweza kusababisha mzozo kuenea katika pande nyingi mbali na nje ya mipaka ya Iran.
Waandishi hao wanaeleza kuwa Marekani ilifanya uvamizi uliotekelezwa vyema nchini Venezuela ambao ulisababisha kukamatwa kwa Maduro katika muda wa saa mbili tu.
Hata hivyo, kuupindua utawala wa Iran si suala la kumuondoa tu Kiongozi Muadhamu, kwa kuzingatia kwamba nguvu halisi ya Tehran ina itikadi iliyothibiti vyema, inayoungwa mkono na mikondo mikali ya kisiasa, na kuimarishwa na muundo tata wa kimabavu ambao umekita mizizi kwa takriban nusu karne.
Pia, eneo la Tehran takriban maili 400 kutoka Ghuba hufanya iwe vigumu zaidi kwa majeshi ya Marekani kuwafikia moja kwa moja na kuwaweka kizuizini viongozi wa Iran, ikilinganishwa na operesheni ya Venezuela, ambayo ni takriban maili 10 tu kutoka Bahari ya Caribbean, kulingana na wataalamu.
Waandishi hao wanahitimisha makala yao kwa kubainisha kwamba Iran hapo awali ilitishia kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ungevuruga mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, na pia inaweza kusababisha kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta
Je, Trump atapigana na Iran?
Bado tunaangazia ongezeko la mzozo kati ya Marekani-Iran na maoni yaliyoandikwa na George Grells katika gazeti la Uingereza "The Sunday Times" yenye kichwa "Je, Marekani itapigana vita na Iran?", na mwandishi anaanza kwa kuashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili, wakati ambapo Trump anajadili ni vituo vipi vya anga ambavyo Marekani inaweza kutegemea katika hali ya aina hii ya mgogoro, na kuamua kuhusu muhula wake kama rais.
Mwandishi huyo anasema kuwa shehena ya ndege ya USS Gerald R. Ford, chombo kikubwa zaidi cha kubeba ndege duniani, inatarajiwa kuwasili Ghuba siku zijazo ili kuungana na shehena ya USS Abraham Lincoln.
Anaongeza kuwa Trump alisema siku ya Ijumaa, akijibu swali kuhusu iwapo Marekani inaweza kufanya mashambulizi madogo dhidi ya Iran: "Nadhani naweza kusema kwamba ninaitazama." Saa kadhaa baadaye, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran "inapaswa kujadiliana makubaliano ya haki."
Mwandishi huyo anadokeza kuwa Marekani imetuma ndege nane za kivita aina ya Arleigh Burke-class katika eneo la Mashariki ya Kati, na kwamba takriban ndege 120 za Marekani zimevuka bahari ya Atlantiki katika siku za hivi karibuni.
Ndege za kivita, ndege za angani za kuongeza mafuta, na ndege za upelelezi zote zimeonekana zikielekea eneo hilo, na inaaminika kuwa angalau nyambizi moja ya kiwango cha Ohio, iliyo na makombora ya masafa marefu, imewekwa kwa njia ambayo inaruhusu kuilenga Iran.
Mwandishi huyo anaamini kuwa licha ya uwezo wa kijeshi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Trump anafahamu hatari ya kuingilia kijeshi nchini Iran.
Pia kuna imani inayoongezeka kwamba utawala wa Iran, baada ya hivi karibuni kuonyesha ugumu mkubwa wa eneo lake la ndani ili kuhakikisha uhai wake, unaweza kujibu mara hii bila kizuizi, kwa kulenga ujumbe wa kidiplomasia wa Marekani, kwa kutumia washirika wake nchini Iraq, kufunga mkondo wa bahari wa Hormuz, au kushambulia vituo vya Marekani huko Jordan, Bahrain, na Qatar.
Mwandishi George Grells anahitimisha makala yake kwa kuashiria kwamba licha ya kuongezeka kwa jeshi la Marekani katika eneo hili, huenda isitoshe kuanzisha uvamizi kamili, na haijabainika iwapo Trump yuko tayari kupeleka wanajeshi wa nchi kavu ili kumpindua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Khamenei.
Pia kuna uwezekano kwamba jibu lolote la Iran katika tukio la vita litajumuisha mashambulizi yanayolenga Israel.