Yahya Sinwar: Je, tunajua nini kuhusu nyumba iliyoshuhudia wakati wa mwisho wa maisha ya kiongozi wa Hamas?

Mbele ya Hospitali ya Emirati kwenye Mtaa wa Ibn Sina katika kitongoji cha Sultan, magharibi mwa mji wa Rafah, kuna nyumba kijijini ya familia ya Mpalestina.
Hawakuwahi kufikiria kwamba nyumba yao, ambayo walilazimika kuihama ingegeuka kuwa eneo la operesheni ya kijeshi kati ya jeshi la Israeli na kiongozi wa harakati ya Hamas, Yahya Sinwar, na hatimaye kuuawa hapo kwa Sinwar katika makabiliano jeshi.
Ashraf Abu Taha, mmiliki wa nyumba na mkuu wa familia iliyoishi ndani ya nyumba hiyo , alikiambia kipindi cha redio cha Gaza Today : "Nimeishi katika nyumba hii kwa miaka 15 na familia yangu. Hatujawahi kuwa wakimbizi na kulazimika kutoka huko, hata wakati wa vita vya awali. Kitu pekee kilichonilazimisha kuondoka ni mbinu ya utoaji wa amri ya kuhama za jeshi la Israeli na uhamishaji wa majirani zangu wote huko Rafah."

Abu Taha aliongeza kuwa anafanya kazi katika klabu ya huduma za utawala ya Rafah na "Sina uhusiano wowote wa kisiasa."
"Kujenga nyumba hii kulinigharimu shekeli 200,000 (karibu dola 53,800 za Marekani), ambazo nilizihifadhi kwa miaka mingi wakati nikifanya kazi yangu ili niweze kuinunua.
Mwanangu na ndugu zangu pia walinisaidia kulipa, na kisha nikaiweka samani za nyumba kikamilifu. Sikuwahi kufikiria kwamba nyumba hii siku moja ingegeuka kuwa uwanja wa vita kati ya Sinwar na jeshi la Israeli," anasema Abu Taha.

Kuhusiana na jinsi alivyopokea taarifa za kilichotokea kwenye nyumba yake ambayo imekuwa gumzo duniani kote, anasema: “Sina uhusiano wowote na mitandao ya kisasa ya kijamii, lakini binti yangu aliona picha na klipu za video zilizochapishwa haraka akanionyesha na kuniuliza: Je, hii si nyumba yetu?”
Aliongeza kuwa: "Nilishangaa nilipoiona, sikuamini. Lakini kaka yangu alinipigia simu na kuniambia kuwa ni nyumba yangu, nilikuwa na uhakika wa kile ambacho macho yangu yanaona. Nilipinga mara ya kwanza, " nilipokea habari kama mshtuko ambao siwezi kuuelezea hadi sasa."
Abu Taha alithibitisha kuwa nyumba yake ilikuwa shwari wakati alipohamishwa tarehe sita mwezi wa Mei na hakuwahi kushambuliwa kwa bomu, na katika kipindi chote hicho hakuweza kupata taarifa zozote kuhusiana na hilo kwa sababu eneo ilipo nyumba yake lilikuwa limeainishwa kama "eneo hatari la operesheni za kijeshi."
Picha zilizosambazwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii kufuatia tangazo rasmi la Israel la kuuawa kwa Sinwar ni jambo la kwanza ambalo Mpalestina huyo aliyekimbia makazi yake alilifahamu kuhusu nyumba yake tangu alipoondoka, jambo ambalo lilizidisha hisia zake za mshtuko, kama alivyoeleza.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuhusu sofa la kupendeza lililoonekana kwenye kipande cha video kilichochapishwa na Avichai Adraee, msemaji wa jeshi la Israeli kwa Kiarabu, ambapo Sinwar alikuwa ameketi katika dakika zake za mwisho, kulingana na jeshi la Israeli, Abu Taha anasema: "Ni sofa lile lile nililokuwa nimekalia huku nikikusanya baadhi ya vifaa nilivyochukua kwenye safari yangu ya kutoka.” [kwenye makazi yangu].
Aliongeza: "Sofa hii ni kipande cha seti ya viti ambayo mama yangu alinipatia, kwa hiyo ina maana ya kipekee kwangu. Ni sofa hiyo hiyo aliyokalia ambayo wanafamilia wangu wamekuwa wakikusanyika kila wakati kwa kipindi cha miaka 15."
Siku ya Alhamisi, Oktoba 17, jeshi la Israel lilitangaza kuuawa kwa kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, katika operesheni iliyofanyika kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya jeshi la Israel na shirika la usalama wa ndani (Shin Bet Kwa upande wake). Hamas ilitoa taarifa siku ya Ijumaa ikimuomboleza kiongozi wake, Yahya Sinwar, katika makabiliano hayo ya jijeshi huko Gaza.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












