Kunusurika mashambulizi ya viboko na mamba katika ziwa la Kenya

tt

Chanzo cha picha, BBC/HASSAN LALI

Joseph Atuma alikuwa mvuvi katika Ziwa Baringo tangu alipokuwa na umri wa miaka 12 na, licha ya kukutana na viboko na mamba mmoja au wawili, hakuna aliyewahi kumshambulia hadi jioni moja ya Septemba 2018, wakati kiboko alipopasua mtumbwi wake, akaushika mguu wake wa kushoto na kuurarulia mbali

"Alikuwa akijificha kwenye kichaka, karibu na ufuo, mahali ambapo sikutarajia kiboko. Na ilinishangaza sana," anasema Atuma mwenye umri wa miaka 42.

"Aling’ata mtumbwi wa mbao hadi meno yake yakanifikia mguuni mwangu. Nyama kidogo sana ilibaki kwenye mfupa wangu, kati ya goti na mguu," anasema, huku akionyesha makovu aliyosalia nayo.

Ziwa Baringo, nchini Kenya, ni moja ya maziwa makubwa ya maji baridi nchini. Kutoka kwenye barabara kuu katika mji mdogo wa Marigat, jua zuri linaangaza miale yake juu ya maji linapochomoza, na kufanya ziwa hilo kumetameta.

Wavuvi tayari wametoka nje, boti zao zikiwa kwenye maji matulivu ya kumetameta. Bw Atuma anasema ndio mwanzo anarejea kutoka kuvua samaki ziwani, miaka mitano baada ya shambulio la viboko.

"Huu ni mkate wangu wa kila siku. Nimejaribu kazi zingine za kawaida hapa na pale, lakini siwezi kuendeleza familia yangu," baba wa watoto wanne anasema.

Anasema kwamba viwango vya maji vimeongezeka kwa miaka mingi, na sasa anasimamisha mashua yake juu ya kile ambacho kilikuwa msingi wa kanisa la mtaa. Kwa sasa limefunikwa na maji ya ziwa - kama vile nyumba, shule, hospitali, barabara za lami na hata ofisi za idara ya uvuvi ya Kenya.

Lakini huwezi kuthibitisha majengo haya yalikuwepo. Zote zimesombwa na ziwa, na jamii zimesukumwa nje, na kuwalazimisha kuishi mbali zaidi.

Maelezo ya video, Tazama: Mamba wa ziwa Baringo wanavyowahangaisha wakazi

Wanamazingira wanasema kiwango vya maji katika ziwa hilo kimeongezeka maradufu katika muongo uliopita kwa sababu ya mvua kubwa inayohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Lakini watu bado wanaendeleza shughuli zao kwa sababu ziwa ndio tegemeo lao la maisha. Makumi ya wanawake huteremka kuchota maji kwa mitungi mikubwa ya manjano kupeleka nyumbani. Wengine wanafua nguo zao ufukweni; na wengine wengi wanasafisha samaki wanaoletwa na wavuvi.

Viboko wakubwa na wanyama wanaowinda wanyama hatari, mamba wa mto Nile, wako ndani ya maji hayo.

Wakazi wanasema kutokana na ziwa hilo kuwa kubwa, idadi ya mamba imeongezeka na maji sasa yamejawa na wanyama wanaowinda wanyama wengine. Wanasema pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya viboko, ambao hulisha karibu na ufuo na sasa wanafika karibu na makazi ya watu.

Hii imeongeza hatari kwa maisha ya watu, na watoto wameburutwa ndani ya ziwa na mamba, wasionekane tena.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Winnie Keben, mama wa watoto sita, alibahatika kunusurika baada ya kushambuliwa na mamba. Sasa anatumia mguu wa bandia uliounganishwa kwenye nyonga yake ya kushoto.

“Nilikuwa nimemaliza kuchota maji ziwani na nilipokuwa nikiosha naosha miguu nilimuona mamba, niliruka na kupiga kelele, nilijaribu kutoroka lakini alinivamia na kunishika mguu akinivuta majini,” anasema.

“Nilipiga kelele na kuinua mkono wangu ili watu wanione, mume wangu alikuwa karibu, aliponiona tu alikimbia kuniokoa.

"Ikiwa imeshika mguu wangu, sote wawili tulijaribu kupambana nayo. Hatimaye iliachana na mguu wangu na kuuma paja langu, likavunjika.

Mtu aliyekuwa karibu alinyanyua panga na kuniokoa kutoka kwa mamba lakini mguu wangu ulitafunwa."

Alilazwa hospitalini kwa muda wa miezi sita, na aliporuhusiwa, alikuta nyumba yake na ardhi ilikuwa imesombwa na maji. Sasa anaishi kilomita kadhaa kutoka ziwa na hajawahi kurudi karibu na maji yake.

“Mambo mengi yamekuwa yakibadilika polepole, zamani hatukuwa na mafuriko, mvua za masika zilitabirika, tungelima na kupata chakula chetu, siku hizi mvua ikinyesha tunapata hasara na uharibifu.

"Nina hofu kwamba nikikaribia maji, naweza kushambuliwa tena, na pia ninaogopa kwamba ziwa linaweza kunipata hata hapa kwa sababu linaendelea kusonga," Bi Keben anaongeza.

tt
Maelezo ya picha, Jengo ndani ya ziwa

Kwa niaba ya jamii, wakazi 66 wameishtaki serikali wakiishtumu kwa kushindwa kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kesi nyingine sawai na hiyo iliwasilishwa mahakamani mwaka jana lakini haijaamuliwa.

Hatua ya hivi punde ya lrgal inalingana na serikali na Umoja wa Afrika (AU) kuandaa kwa pamoja mkutano wa kwanza kabisa wa hali ya hewa barani Afrika katika mji mkuu, Nairobi, na Rais William Ruto akiwasili kwa gari la kutumia umeme.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Afŕika inachangia asilimia 2-3 tu ya hewa chafu ya kaboni duniani lakini bara hilo limeathiriwa zaidi na ongezeko la joto duniani.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Ruto alisema bara hilo litahitaji matrilioni ya dola katika "fursa za uwekezaji wa kijani" ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.

"Lazima tuwekeze katika ukuaji wa kijani, sio tu umuhimu wa hali ya hewa bali pia chemchemi ya fursa za kiuchumi za mabilioni ya dola ambazo Afrika na ulimwengu unatazamiwa kuzitumia," Bw Ruto aliambia wajumbe.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeahidi kuipatia Afrika dola bilioni 4.5 katika uwekezaji wa nishati safi, juu ya wawekezaji kutoka nchi hiyo wanaokubali kununua $450m za mikopo ya kaboni kupitiaMpango wa Masoko ya Kaboni Afrika (Africa Carbon Markets Initiative).

Serikali ya Uingereza imeahidi kuwekeza dola bilioni 61 (£49m) katika miradi mipya ili kusaidia bara hilo kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ni pamoja na dola milioni 43 kwa miradi mipya katika nchi 15 kusaidia wanawake, jumuiya zilizo katika hatari, na zaidi ya wakulima 400,000 kujenga uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya hali ya hewa, inasema.

Wakazi ambao wamewasilisha kesi mahakamani wanadai kuwa serikali ya Kenya mpaka sasa imeshindwa kukabiliana na janga la hali ya hewa, na wanateseka kutokana na umaskini na magonjwa kwa sababu ya kuongezeka kwa ukubwa wa ziwa hilo.

Ramani

Wanadai fidia ya kifedha kwa ajili yao na familia zingine ambazo zimepoteza ardhi ya mababu zao, mashamba na mifugo, na wamekabiliwa na magonjwa yanayotokana na maji kama vile malaria na kipindupindu.

"Vyombo vinavyohusika na kuweka sera husika za mabadiliko ya hali ya hewa ili kuhakikisha haki ya mazingira safi na yenye afya vilishindwa, vilikataa na au vilipuuza kufanya hivyo," kulingana na karatasi za mahakama zilizowasilishwa kwa niaba yao na kituo cha ushauri wa kisheria, Kituo Cha Sheria.

"Wakati mahakama itakapofanya uamuzi, inaweza kuweka kanuni fulani na inaweza kuwa mfano wa kuvunja njia katika eneo la mabadiliko ya hali ya hewa," anasema Omondi Owino, wakili wa mazingira katika kituo hicho.

Serikali bado haijajibu kesi hiyo.

Kuhusu Bw Atuma, ziwa hilo bado linasalia kuwa chanzo chake cha riziki – lakini anaishi kwa hofu ya mara kwa mara ya mamba na viboko.

"Kiwango cha maji ni kikubwa sana kwa sasa. Wanyama wa ziwa [viboko] wanafika karibu na ufuo. Baadhi yao wanataka kukanyaga ardhini ambako maji ni duni na hii ina maana kwamba wanakaribia watu.

"Inakupa nafasi ndogo ya kufanya ujanja hata unapokaribia kutua. Wakati unapokimbia wanashambulia na hakuna njia ya kutoroka," anasema.