Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Ni nchi gani zinazoipa Urusi silaha?
- Author, Jeremy Howell
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Urusi inatuma mamilioni ya makombora kwa mwaka kwenye vita vyake nchini Ukraine, pia hufanya mashambulizi ya anga – na inasemekana silaha hizo hutolewa na washirika wa kigeni.
Wakati mataifa ya Magharibi yakijaribu kuhujumu uwezo wa Urusi wa kutengeneza silaha kwa kuiwekea vikwazo, China, Iran na Korea Kaskazini zinadaiwa kuisaidia ili vita viendelee.
Makombora kutoka Iran
Hivi karibuni Iran imeshutumiwa kufanya makubaliano na Urusi ya kuipatia makombora 200 au zaidi ya masafa mafupi. Makombora ya Fath-360, yanaweza kwenda umbali wa maili 75 (120km) na hubeba kilo 150 za vilipuzi.
Idara ya ujasusi ya Marekani inasema makumi ya wanajeshi wa Urusi wamepewa mafunzo nchini Iran juu ya namna ya kutumia makombora hayo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alisema makombora hayo yanaweza kutumiwa dhidi ya Ukraine baadaye msimu huu wa vuli.
Urusi inaweza kuipa Iran teknolojia ya kijeshi kama malipo. Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeiwekea Iran vikwazo vipya kwa kuipatia Urusi makombora hayo.
Ikiwa ni pamoja na kuzuia safari za ndege za Iran Air kwenda Uingereza na Ulaya pamoja na marufuku ya kusafiri na kushikiliwa mali za Wairani wanaodhaniwa kuhusika katika makubaliano hayo.
Iran imekanusha mara kwa mara kusambaza silaha za Fath-360 kwa Urusi.
Droni kutoka Iran
Serikali ya Ukraine na mashirika ya kijasusi ya Magharibi yanasema Iran imekuwa ikiipatia Urusi ndege zisizo na rubani za Shahed-136 tangu msimu wa vuli wa 2022.
Shahed ina kichwa cha kombora kwenye pua yake na imeundwa kuzunguka shabaha hadi ipewe ishara ya kushambulia.
Vikosi vya Urusi mara nyingi hutuma makumi ya droni hizi kujaribu kuuzidi nguvu ulinzi wa anga wa Ukraine. Mara nyingi makundi ya droni hizo hutumiwa ili kuzuia ulinzi wa anga wa Ukraine kunasa makombora, ambayo hupakia vilipuzi zaidi na kufanya uharibifu mkubwa.
Serikali ya Iran inasema iliipatia Urusi "idadi ndogo" ya ndege zisizo na rubani kabla ya vita.
Hata hivyo, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeishutumu Iran kwa kutuma droni mara kwa mara nchini Urusi, na EU imeweka vikwazo kwa watu na makampuni yanayohusika.
Makombora kutoka Korea Kaskazini
Shirika la Ujasusi la Marekani (DIA) la Wizara ya Ulinzi, lilisema katika ripoti ya Mei 2024, Korea Kaskazini imeipatia Urusi makombora milioni tatu.
Makombora ndio silaha kuu inayotumiwa na pande zote mbili katika vita vya Ukraine. Yanazuia magari ya adui na askari wa miguu kutosonga mbele.
Taasisi ya Royal United Services (Rusi) yenye makao yake makuu nchini Uingereza, inasema katika miezi ya hivi karibuni vikosi vya Urusi vimekuwa na makombora 5 kwa 1 dhidi ya Ukraine katika idadi ya makombora yanayoweza kufyatuliwa.
Rusi inasema hiyo ndio sababu kuu ya Urusi kutwaa eneo kubwa mashariki mwa Ukraine tangu msimu wa baridi wa 2023.
Makombora ya Balistiki
Januari 2024, maafisa wa ujasusi wa Ukraine walisema walipata mabaki ya aina mbili za makombora ya masafa mafupi ya balestiki ambayo yalitengenezwa na Korea Kaskazini na yalirushwa Kharkiv katika shambulio kubwa la anga.
Mamlaka ya Ukraine zinasema moja ya kombora hilo ni Hwasong-11, pia linajulikana kama KN-23.
Hili ni kombora la balistiki la masafa mafupi lenye uwezo wa kufika hadi kilomita 400 na 690, linaweza kubeba kichwa cha mlipuko chenye uzito wa hadi kilogramu 500.
Umoja wa Mataifa umeiwekea vikwazo vya kibiashara juu ya makombora ya balistiki nchi ya Korea Kaskazini tangu 2006.
Idara ya ujasusi ya Ukraine inasema Korea Kaskazini imetuma makombora 50 nchini Urusi ya aina hiyo. Na katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Februari 2024, Marekani iliishutumu Urusi kwa kutumia makombora ya Korea Kaskazini katika mashambulizi tisa ya anga dhidi ya Ukraine.
DIA inasema Urusi na Korea Kaskazini zilianza mazungumzo ya uuzaji wa silaha wakati wa msimu wa vuli 2022 na makombora ya kwanza yalitumwa kutoka Korea Kaskazini hadi Urusi wakati wa vuli 2023 kwa majaribio.
Korea Kaskazini imekanusha kutuma silaha kwa Urusi, na Urusi imekana kupokea silaha zozote.
Wanajeshi wa Korea Kaskazini
Maafisa wa ujasusi wa Ukraine wanasema wamewaona wanajeshi wa Korea Kaskazini wakiwa na vikosi vya Urusi nchini humo.
Magazeti ya Ukraine yaliripoti tarehe 3 Oktoba 2024, kuwa maafisa sita wa Korea Kaskazini waliuawa - na wengine watatu kujeruhiwa - katika shambulio la kombora kwenye kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Urusi eneo la mashariki.
Madai ya hapo awali ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kupigana nchini Ukraine yalitolewa mwaka 2023, lakini Rais wa Urusi Vladimir Putin alikanusha kuwa ni "upuuzi mtupu."
Uwepo wa wanajeshi, kufanya mikataba ya silaha na nchi kama Iran na Korea Kaskazini kunaonyesha kwamba Urusi ina washirika, na haijatengwa.
Vifaa vya China
Viongozi wa nchi wanachama wa Nato kwa pamoja wameishutumu China kwa kuwa "mwezeshaji wa Urusi kwa kutoa "msaada mkubwa kwa viwanda vya kutengenezea silaha.”
Wamesema hutoa vifaa kama vile chipu za kompyuta ambazo zina programu za kiraia lakini pia zinaweza kutumika kutengeneza silaha.
Shirika la Carnegie Endowment for International Peace (CEIP) lenye makao yake makuu nchini Marekani, linasema kuwa kila mwezi China imekuwa ikiitumia Urusi bidhaa zenye thamani ya dola milioni 300, ambazo zinaweza kutumika kutengeneza silaha kama vile ndege zisizo na rubani, makombora na vifaru.
Inasema China inaiuzia Urusi 70% ya zana zake zote za mashine, ambazo zinaweza kutumika kutengeneza silaha. CEIP inasema, 2023 Urusi iliagiza 89% ya bidhaa zake zote muhimu katika viwanda vya silha kutoka China.
Kabla ya vita, Ujerumani na Uholanzi ziliuza nyingi ya bidhaa hizo, kabla ya vikwazo na China ilijaza pengo hilo.
China imekanusha kuisaidia Urusi kutengeneza silaha, inasema haigemei upande wowote katika vita vya Ukraine. Na haijatoa vifaa hatari kwa Urusi na imekuwa na tahadhari katika vifaa inavyouza.
Shirika la habari la Reuters linasema Urusi imeanzisha kiwanda nchini China kuzalisha aina mpya ya ndege isiyo na rubani ya masafa marefu iitwayo Garpiya-3.
Serikali ya China imesema haijui lolote kuhusu mradi huo na ina udhibiti mkali wa usafirishaji wa ndege zisizo na rubani nje ya nchi, kulingana na Reuters.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah