Mamlaka katika mji wa Eldoret nchini Kenya imeondoa sanamu za wanariadha watatu baada ya kukejeliwa na kuelezewa kuwa ni "aibu" na "mzaha".
Sanamu hizo zilizinduliwa kabla ya sherehe za Alhamisi kulipa hadhi jiji la Eldoret.
Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo na Wakenya mtandaoni walisema sanamu hizo hazifanani na wanariadha wanaodaiwa kuwawakilisha.
Eldoret inajulikana kama "Sehemu ya mabingwa", kama ilivyo katikati mwa Bonde la Ufa, ambapo wanariadha wengi wa Kenya wanaoshinda ulimwengu wanatoka.
Sanamu hizo ziliondolewa usiku kucha kabla ya Rais William Ruto kuuteua rasmi mji wa Eldoret kuwa jiji. Jiji hilo wiki hii lilizindua kazi zake za sanaa, zikiwemo sanamu tatu za wanariadha .
Sanamu hizo zililenga kuwakilisha urithi wa michezo na kilimo katika eneo hilo na ziliwekwa katika barabara tofauti za mji huo.
Lakini mara moja zilikosolewa na wengi, na badala yake kuwa vitu vya dhihaka badala ya vitu vilivyowekwa kwa Wakenya kujivunia.
Mkenya mmoja ambaye alisambaza picha ya sanamu ya mwanariadha wa kike anayeshukiwa kumwakilisha mwanariadha aliyeshikilia rekodi ya dunia ya mita 1,500, Faith Kipyegon, alisema kazi hizo zinawakilisha "usawa wetu wa umoja kama nchi".
"Ni aibu kuiita sanamu ya Faith Kipyegon," Mkenya mwingine kwenye X alisema.
Mtumiaji mwingine wa X alisambaza sanamu inayodaiwa kuwa ya gwiji wa mbio za
marathon Eliud Kipchoge akiiita "mzaha", akisema "yeyote
aliyefanya hivi hataiona mbingu".
Ripota
wa eneo hilo aliambia BBC kwamba maafisa wa kaunti waliondoa sanamu hizo tatu
usiku wa kuamkia leo, wawili wakiwakilisha wanariadha wa kike na mmoja wa
mwanamume, na kuwapeleka kusikojulikana.
Mamlaka
haijaonyesha wanamwakilisha nani lakini watumiaji wa mitandao ya kijamii
wametaja moja kama sanamu ya Kipyegon na nyingine ya Kipchoge.
Lakini
taswira yao ya wanariadha hao imeelezwa kuwa "isiyo na aibu", na "chini ya kiwango".
Wakenya
mtandaoni wamekuwa wakiunga mkono kuondolewa kwa sanamu hizo. Haikuwa wazi kama
zingebadilishwa, na lini.
Kabla
ya hafla ya kutangaza Eldoret kuwa jiji la tano la Kenya, Rais Ruto
aliwakaribisha wanariadha walioshinda medali katika Michezo ya Olimpiki ya
2024.
Kila
mmoja wao alituzwa pesa kwa mujibu wa mpango wa serikali uliokusudiwa
kuwahamasisha wanariadha kwa utendaji mzuri.
Kenya
ilikuwa nchi iliyoorodheshwa ya juu zaidi barani Afrika katika Michezo ya
Olimpiki ya Paris, ikishika nafasi ya 17 kwenye jedwali la medali ikiwa na
dhahabu nne na jumla ya medali 11.
Kipyegon
alishinda taji la mita 1,500 katika rekodi mpya ya Olimpiki ya dakika 3 na
sekunde 51.29, akiwa mwanamke wa kwanza
kushinda dhahabu tatu mfululizo katika mashindano hayo.
Pia alishinda
medali ya fedha katika mbio za mita 5,000.
Hata
hivyo, bingwa wa mbio za marathon Kipchoge hakumaliza mbio zake baada ya jeraha la mgongo kumlazimu kujiondoa.