Tayari kumeripotiwa kuonekana kwa silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi ndani ya Urusi, tangu Ukraine ilipoanzisha mashambulizi yake mapya mapema mwezi huu.
Muhtasari
Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza, kuwaachilia mateka yaanza tena Doha
MPOX yasababisha vifo vya watu zaidi ya 500 mwaka huu DRC
Shutuma zalifanya jiji la Eldoret kuondoa sanamu za 'wanariadha' wa Kenya
Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachofahamu kufikia sasa
Ni silaha gani za Magharibi zimetolewa kwa Ukraine hadi sasa?
Mwanamke mwenye uraia wa Marekani na Urusi afungwa miaka 12 jela kwa kosa la uhaini
Zaidi ya watu 40,000 waliuawa huko Gaza, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas yasema
Baba yake nyota wa Barcelona Lamine Yamal achomwa kisu
Silaha za nchi za magharibi zaonekana Urusi
Kikosi cha anga cha Ukraine chasema kilidungua ndege 29 za Urusi usiku kucha
Ukraine iko 'huru kutumia' silaha za Uingereza Urusi
Korea Kaskazini kufunguliwa tena kwa utalii baada ya miaka mitano
India: Wanawake waandamana usiku kulalamikia mauaji ya daktari tarajali
Rais wa zamani wa Argentina ashutumiwa kwa kumdhalilisha mpenzi wake
Hamas haitajiunga na mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza
Columbia: Rais wa chuo kikuu ajiuzulu baada ya maandamano kuhusu Gaza
WHO yatangaza mlipuko wa Mpox kuwa dharura ya kiafya duniani
Ukraine yaendelea kusonga mbele ndani ya eneo la Urusi
Moja kwa moja
Asha Juma
Habari za hivi punde, Mgonjwa wa kwanza wa Mpox apatikana Sweden
Wakala wa afya ya umma nchini Sweden imerekodi kile inachosema kuwa ni kisa cha kwanza cha aina mpya ya ugonjwa wa mpox nje ya bara la Afrika.
Mtu huyo aliambukizwa alipokuwa akikaa katika eneo la Afrika ambako kwa sasa kuna mlipuko mkubwa wa mpox Clade I, shirika hilo lilisema.
Habari hizo zinakuja saa chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kwamba mlipuko wa ugonjwa wa mpox katika baadhi ya maeneo ya Afrika sasa ni dharura ya afya ya umma ambayo inatia wasiwasi kimataifa.
Takribani watu 450 walikufa wakati wa mlipuko wa awali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza, kuwaachilia mateka yaanza tena Doha
Chanzo cha picha, EPA
Mazungumzo kuhusu kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka katika Ukanda wa Gaza yameanza tena nchini Qatar, huku idadi ya Wapalestina walioripotiwa kuuawa katika vita kati ya Israel na Hamas ikizidi 40,000.
Makubaliano yanaonekana kama chachu ya kusitisha mzozo wa miezi 10 unaoendelea hadi katika vita vya kikanda vinavyohusisha Iran, lakini matarajio ya mafanikio ni madogo.
Hamas imesema haitashiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja huko Doha kwa sasa, ingawa wapatanishi wanatarajiwa kupeleka ujumbe kwa maafisa wa kundi hilo lenye silaha walioko huko.
Imetoa wito wa kubuniwa kwa msingi wa pendekezo lililotolewa na rais wa Marekani na kumshutumu waziri mkuu wa Israel kwa kuongeza masharti mapya, jambo ambalo amelikanusha.
Wapatanishi kutoka Marekani, Qatar na Misri wanakabiliwa na mambo kadhaa yanayoweza kukwama, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa ardhi kwenye mpaka wa Gaza na Misri na kurejea kwa raia wa Palestina waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Gaza.
Mazungumzo hayo yalisitishwa tangu kiongozi wa kisiasa wa Hamas na mpatanishi mkuu, Ismail Haniyeh, alipouawa mjini Tehran mwishoni mwa Julai.
Iran imeapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel, ambayo haijathibitisha wala kukanusha kuhusika na hivyo kuzua hofu ya kuongezeka kwa mzozo zaidi.
MPOX yasababisha vifo vya watu zaidi ya 500 mwaka huu DRC,
Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema Homa ya Nyani MPOX imesababisha vifo vya watu mia tano arobaini na wanane mwaka huu,huku mikoa yote nchini humo ikiripotii visa vya ugonjwa huo.
Waziri wa afya w DRC Samuel Roger Kamba amesema nchi hiyo imerekodi visa takribani 15,600 na zaidi ya vifo mia tano tangu kuanza kwa mwaka huu.
DRC ina majimbo ishirini na sita na idadi jumla ya watu milioni mia moja.
Bwana Kamba amesema Majimbo yaliyoathirika vibaya na MPOX ni Kivu Kusini, Kivu Kaskazini,Tshopo,Equateur,North Ubangi,Tshuapa,Mongala na Sankuru.
Hapo jana,shirika la afya duniani WHO lilitagaza kuwa MPOX ni dharura ya afya ya umma duniani kutokana na kuongezeka kwa visa vya homa hiyo ya nyani DRC na katika mataifa jirani na nchi hiyo.
Uamuzi huo wa WHO ulikuja siku moja baada ya shirika la kudhibiti magonjwa Afrika CDC kutangaza pia MPOX ni dharura ya afya ya umma barani Afrika.
Shutuma zalifanya jiji la Eldoret kuondoa sanamu za 'wanariadha' wa Kenya
Chanzo cha picha, Cyrus Sholim
Maelezo ya picha, Mamlaka haijasema sanamu hizo zinapaswa kuwakilisha akina nani
Mamlaka katika mji wa Eldoret nchini Kenya imeondoa sanamu za wanariadha watatu baada ya kukejeliwa na kuelezewa kuwa ni "aibu" na "mzaha".
Sanamu hizo zilizinduliwa kabla ya sherehe za Alhamisi kulipa hadhi jiji la Eldoret.
Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo na Wakenya mtandaoni walisema sanamu hizo hazifanani na wanariadha wanaodaiwa kuwawakilisha.
Eldoret inajulikana kama "Sehemu ya mabingwa", kama ilivyo katikati mwa Bonde la Ufa, ambapo wanariadha wengi wa Kenya wanaoshinda ulimwengu wanatoka.
Sanamu hizo ziliondolewa usiku kucha kabla ya Rais William Ruto kuuteua rasmi mji wa Eldoret kuwa jiji. Jiji hilo wiki hii lilizindua kazi zake za sanaa, zikiwemo sanamu tatu za wanariadha .
Sanamu hizo zililenga kuwakilisha urithi wa michezo na kilimo katika eneo hilo na ziliwekwa katika barabara tofauti za mji huo.
Lakini mara moja zilikosolewa na wengi, na badala yake kuwa vitu vya dhihaka badala ya vitu vilivyowekwa kwa Wakenya kujivunia.
Mkenya mmoja ambaye alisambaza picha ya sanamu ya mwanariadha wa kike anayeshukiwa kumwakilisha mwanariadha aliyeshikilia rekodi ya dunia ya mita 1,500, Faith Kipyegon, alisema kazi hizo zinawakilisha "usawa wetu wa umoja kama nchi".
"Ni aibu kuiita sanamu ya Faith Kipyegon," Mkenya mwingine kwenye X alisema.
Mtumiaji mwingine wa X alisambaza sanamu inayodaiwa kuwa ya gwiji wa mbio za
marathon Eliud Kipchoge akiiita "mzaha", akisema "yeyote
aliyefanya hivi hataiona mbingu".
Ripota
wa eneo hilo aliambia BBC kwamba maafisa wa kaunti waliondoa sanamu hizo tatu
usiku wa kuamkia leo, wawili wakiwakilisha wanariadha wa kike na mmoja wa
mwanamume, na kuwapeleka kusikojulikana.
Mamlaka
haijaonyesha wanamwakilisha nani lakini watumiaji wa mitandao ya kijamii
wametaja moja kama sanamu ya Kipyegon na nyingine ya Kipchoge.
Lakini
taswira yao ya wanariadha hao imeelezwa kuwa "isiyo na aibu", na "chini ya kiwango".
Wakenya
mtandaoni wamekuwa wakiunga mkono kuondolewa kwa sanamu hizo. Haikuwa wazi kama
zingebadilishwa, na lini.
Kabla
ya hafla ya kutangaza Eldoret kuwa jiji la tano la Kenya, Rais Ruto
aliwakaribisha wanariadha walioshinda medali katika Michezo ya Olimpiki ya
2024.
Kila
mmoja wao alituzwa pesa kwa mujibu wa mpango wa serikali uliokusudiwa
kuwahamasisha wanariadha kwa utendaji mzuri.
Kenya
ilikuwa nchi iliyoorodheshwa ya juu zaidi barani Afrika katika Michezo ya
Olimpiki ya Paris, ikishika nafasi ya 17 kwenye jedwali la medali ikiwa na
dhahabu nne na jumla ya medali 11.
Kipyegon
alishinda taji la mita 1,500 katika rekodi mpya ya Olimpiki ya dakika 3 na
sekunde 51.29, akiwa mwanamke wa kwanza
kushinda dhahabu tatu mfululizo katika mashindano hayo.
Pia alishinda
medali ya fedha katika mbio za mita 5,000.
Hata
hivyo, bingwa wa mbio za marathon Kipchoge hakumaliza mbio zake baada ya jeraha la mgongo kumlazimu kujiondoa.
Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachofahamu kufikia sasa
Chanzo cha picha, Reuters
Asubuhi ya leo tumekuwa tukikuletea matukio katika vita vya Ukraine kufuatia uthibitisho kutoka kwa Wizara ya Ulinzi kwamba Ukraine inaweza kutumia silaha za Uingereza katika ardhi ya Urusi - isipokuwa makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow.
Serikali ilisema hii haiwakilishi mabadiliko ya sera.
Tangu wakati huo chanzo cha habari cha Uingereza kimeithibitishia BBC kwamba mizinga ya Challenger 2 imetumika wakati wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Uingereza ilikuwa imeipa Ukraine mizinga 14 ya aina hiyo mwaka jana.Wakati huo huo, jeshi la wanahewa la Ukraine lilisema liliangusha ndege 29 za Urusi usiku kucha - na kuongeza kuwa mtu mmoja aliuawa na 13 kujeruhiwa.
Kulingana na shirika la habari la serikali TASS hali ya dharura imetangazwa katika eneo la mpakani la Belgorod.
Moscow imesema inawarudisha nyuma wanajeshi wa Ukraine, huku wizara ya ulinzi ya Urusi ikidai imelikomboa eneo la makaazi ya Krupets mjini Kursk.
Ni silaha gani za Magharibi zimetolewa kwa Ukraine hadi sasa?
Chanzo cha picha, PA Media
Kama ambavyo tumekuwa tukiripoti, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza
imethibitisha kwamba Ukraine inaweza kutumia silaha za Uingereza katika ardhi
ya Urusi.
Ingawa hatujui hasa ikiwa au ni silaha gani zinaweza kutumiwa na
vikosi vya Ukraine kusonga mbele, aina mbalimbali zimetolewa na nchi za
Magharibi kufikia sasa.
Miongoni mwa hayo ni makombora ya kifaru ya Javelin na Nlaw
yaliyotolewa na Marekani na Uingereza.
Marekani na Norway pia zimetoa Nasams (Mfumo wa Juu wa
Kombora la Anga) kwa ajili ya ulinzi wa anga.
Mnamo Julai tuliangalia kwa undani silaha zilizotolewa kwa
Ukraine wakati huo.
Mwanamke mwenye uraia wa Marekani na Urusi afungwa miaka 12 jela kwa kosa la uhaini
Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Mahakama ya Urusi imemhukumu mchezaji mahiri wa balerina, Ksenia Karelina kifungo cha miaka 12 jela kwa kosa la uhaini kwa kutoa $51 (£39) kwa shirika la misaada linaloisaidia Ukraine.
Karelina, ambaye ana uraia wa Marekani na Urusi, alikutwa na hatia wiki iliyopita baada ya kesi iliyosikilizwa bila kuwepo watu.
Alikuwa akiishi Los Angeles na akawa raia wa Marekani mwaka wa 2021.
Alikamatwa wakati wa ziara ya kifamilia Januari mwaka jana Yekaterinburg, yapata kilomita 1,600 (maili 1,000) mashariki mwa Moscow.
Waendesha mashtaka walikuwa wameomba kifungo cha miaka 15 jela. Mahakama ya Yekaterinburg ilimpata na hatia ya uhaini mkubwa na kumhukumu kifungo cha jela katika jela ya serikali kuu. Karelina alikuwa ameshutumiwa na idara ya usalama ya FSB ya Urusi kwa kuchangisha pesa kwa ajili ya shirika la Ukraine linalotoa silaha kwa wanajeshi wa Ukraine.
Wanaharakati wa haki za binadamu wa Urusi walisema alipokuwa akiishi Marekani alifanya uhamisho mmoja wa fedha wa $51.80 katika siku ya kwanza ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 22 Februari 2022.
FSB inadhaniwa kugundua shughuli hiyo kwenye simu yake.
Wakili wake, Mikhail Mushailov, alisema Karelina alikubali tu kuhamisha pesa hizo na anaamini kuwa fedha hizo zingesaidia waathiriwa wa pande zote mbili.
Aliviambia vyombo vya habari vya Urusi kuwa atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Shirika la hisani, Razom kwa ajili ya Ukraine, lilisema mapema mwaka huu "ilishtushwa" kusikia kuhusu kukamatwa kwa mchezaji mahiri wa ballerina na kukana kukusanya pesa kwa ajili ya silaha. Ilisema ni shirika la misaada lililoanzishwa na Marekani linalolenga misaada ya kibinadamu na maafa.
Tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, mamlaka ya Urusi imedhibiti wapinzani na mashirika ya haki za binadamu yanasema zaidi ya kesi 1,000 za uhalifu zimefunguliwa dhidi ya wapinzani wanaopinga vita.
Zaidi ya watu 40,000 waliuawa huko Gaza, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas yasema
Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya Wapalestina 40,000 wameuawa kutokana na hatua ya kijeshi ya Israel huko Gaza tangu shambulio la Oktoba 7 lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israeli, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema.
Idadi hiyo, 40,005 siku ya Alhamisi ni sawa na karibu 1.7% ya wakazi milioni 2.3 wa eneo hilo.
Kando na vifo, uchambuzi wa picha za satelaiti unaonesha karibu 60% ya majengo huko Gaza yameharibiwa tangu mwanzo wa vita.
Katika miezi michache iliyopita, mji wa kusini wa Rafah umepata uharibifu mkubwa zaidi, picha zinaonesha.
Takwimu za wizara ya afya za idadi ya watu waliouawa hazitofautishi kati ya raia na wapiganaji.
Hatahivyo, uchambuzi wake wa vifo vilivyoripotiwa unasema wengi ni watoto, wanawake au wazee.
Mwezi huu, jeshi la Israel liliiambia BBC kuwa zaidi ya magaidi 15,000 waliuawa wakati wa vita.
Waandishi wa habari wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, wamezuiwa na Israel kuingia Gaza kwa kwa kujitegemea, hivyo hawawezi kuthibitisha takwimu kutoka upande wowote.
Hapo awali, takwimu kutoka Wizara ya Afya ya Gaza (MoH) zilitumika sana nyakati za migogoro na kuonekana kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa.
Ilihesabu tu vifo vilivyosajiliwa katika hospitali na hizi ziliingia katika mfumo mkuu pamoja na majina, nambari za utambulisho na maelezo mengine.
Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka jana Wizara ya Afya haikuweza kufanya kazi ipasavyo na vyumba vya kuhifadhia maiti vilivyofurika, mapigano ndani na karibu na hospitali na muunganisho duni wa intaneti na simu.
Baba yake nyota wa Barcelona Lamine Yamal achomwa kisu
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mounir Nasraoui (kulia) akitazama wakati mtoto wake wa kiume akifunga bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 wa Uhispania dhidi ya England kwenye fainali ya Euro
Baba wa nyota wa soka wa Uhispania Lamine Yamal mwenye umri wa miaka 17 ameripotiwa kuchomwa kisu mara kadhaa kwenye eneo moja la maegesho ya magari.
Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Uhispania, Mounir Nasraoui alishambuliwa katika mji wa pwani wa Mataró, kaskazini mwa Barcelona, Jumatano usiku na kundi la watu aliozungumza nao mapema mchana.
Polisi wa Catalonia wamethibitisha kuwa takriban watu watatu wamekamatwa, shirika la habari la AFP linaripoti.
Bw Nasraoui alipelekwa hospitalini mjini Barcelona akiwa katika hali mbaya lakini sasa anasemekana kuwa yuko sawa.
Shambulio hilo lilifanyika karibu na kitongoji cha Rocafonda ambapo Yamal alikulia.
Mapema siku hiyo, Bw Nasraoui inasemekana aligombana na kundi la watu aliokutana nao alipokuwa akimtembeza mbwa wake, gazeti la Uhispania El Pais liliripoti.
Saa kadhaa baadaye, alifikiwa na kundi lile lile kwenye maegesho ya magari na kuchomwa kisu "mara kadhaa".Sababu ya kuchomwa kisu haijajulikana kwa sasa.Ripoti kwenye tovuti ya michezo ya Relevo ilisema kuwa Bw Nasraoui alitarajiwa kusalia hospitalini kwa siku mbili au tatu chini ya uangalizi.
Lamine Yamal, mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea nchini Uhispania, alishiriki michuano ya Euro 2024 ambapo alitajwa kuwa Mchezaji Chipukizi bora wa Mashindano hayo.
Winga huyo alitoa pasi iliofungwa na Nico Williams likiwa, bao la ufunguzi wakati Uhispania ilipoilaza England 2-1 kwenye fainali iliyochezwa Berlin.
Muda mfupi baada ya Uhispania kunyanyua kombe hilo, mashabiki walijipanga katika mitaa ya Mataró wakimshangilia nyota wao mchanga.
Baada ya kukulia katika mji huo, Yamal alitumia baadhi ya miaka yake ya ujana katika chuo kikuu cha Barcelona cha La Masia.
Silaha za nchi za magharibi zaonekana Urusi
Chanzo cha picha, Getty Images
Tayari kumeripotiwa kuonekana kwa silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi ndani ya Urusi, tangu Ukraine ilipoanzisha mashambulizi yake mapya mapema mwezi huu.
Ni pamoja na magari ya kivita ya Bradley na Stryker yanayotolewa na Marekani pamoja na Marders zinazotolewa na Ujerumani.
Hakujawa na picha zilizooneshwa kufikia sasa za mizinga ya Challenger ya Uingereza au mizinga ya Abrams ya Marekani kwenye eneo la mpaka.
Hata hivyo, wataalamu wa kijeshi wa Magharibi wameangazia mafanikio ya mashambulizi ya Ukraine kwa kutumia askari pamoja na magari ya kivita, mizinga na vifaru pamoja na vita vya kielektroniki na ndege zisizo na rubani, kushambulia.
Hilo lilikuwa jambo ambalo halikuwepo katika shambulio la mwaka jana la Ukraine Kusini na Mashariki mwa nchi hiyo, ambalo lilizuiliwa na ngome za Urusi zilizochimbwa sana na kufanya kuwa vigumu na hatari kutumia silaha.
Moja ya mizinga 14 ya Uingereza iliyopewa Challenger 2 iliharibiwa katika shambulio hilo lililozuiwa. Vifaru vya Uingereza vilivyotolewa vimekuwa vikiendeshwa na Kikosi cha 82 cha Mashambulizi ya Anga cha Ukraine, ambao walipata mafunzo kwa mara ya kwanza nchini Uingereza jinsi ya kutumia Challenger 2.
Imeelezwa kuwa Ukraine imetumia baadhi ya vitengo vyake vilivyofunzwa vyema na vilivyo na vifaa bora kufanya mashambulizi yake kwenye mpaka.
Kikosi cha anga cha Ukraine chasema kilidungua ndege 29 za Urusi usiku kucha
Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la anga la Ukraine linasema kuwa lilidungua ndege zote 29 zisizo na rubani zilizorushwa usiku kucha na Urusi ambayo ililenga maeneo nane ya Ukraine, huku mtu mmoja akiuawa na 13 kujeruhiwa.
Urusi pia ilirusha makombora matatu ya kh-59 wakati wa shambulio hilo, maafisa wa Ukraine walisema katika taarifa, na kuongeza kuwa uharibifu mdogo tu ndio ulioripotiwa.
Magavana wa mikoa ya Kyiv, Poltava na Kirovohrad wanasema hakukuwa na majeruhi au uharibifu wa majengo katika eneo la kati la Cherkasy.
Katika eneo la kusini la Mykolaiv, ndege tano zisizo na rubani zilidunguliwa wakati, ndege nane zisizo na rubani zilidunguliwa huko Kherson. Gavana wa Kherson anasema mashambulizi mbalimbali katika eneo hilo yameua mtu mmoja na kujeruhi 13.
Ukraine iko 'huru kutumia' silaha za Uingereza kwenye ardhi ya Urusi - Wizara ya Ulinzi
Chanzo cha picha, Reuters
Vikosi vya Ukraine vinaweza kutumia silaha za Uingereza
katika ardhi ya Urusi wakati ikijilinda, Wizara ya Ulinzi imethibitisha.
Msemaji wa wizara hiyo amesema Ukraine ina "haki ya
wazi ya kujilinda dhidi ya mashambulizi haramu ya Urusi...hilo haliondoi operesheni
ndani ya Urusi".
"Tunaweka wazi wakati tunawapa kwamba vifaa
vitatumika kulingana na sheria za kimataifa," iliongeza.
Sir Ben Wallace, waziri wa zamani wa ulinzi wa chama cha
Conservative, ameripotiwa kusema hapo awali kwamba silaha zote zinazotolewa na
Uingereza, isipokuwa makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow, zinaweza
kutumika ndani ya Urusi.
Korea Kaskazini kufunguliwa tena kwa utalii baada ya miaka mitano
Chanzo cha picha, Getty Images
Korea Kaskazini itafungua tena jiji moja kwa watalii wa
kigeni mnamo mwezi Desemba baada ya karibu miaka mitano ya kufungwa kwa mipaka
kwa sababu ya janga la Covid-19.
Watu wawili wanaosimamia utalii nchini China wametangaza
kuwa hivi karibuni watalii wataruhusiwa kuzuru mji wa kaskazini mwa milima wa
Samjiyon.
Korea Kaskazini iliyojitenga ilijifungia mwanzoni mwa
janga hili mapema mwaka 2020 na ilianza kulegeza masharti katikati ya mwaka
jana.
Kufungwa kwa mpaka pia kumesitisha uagizaji wa bidhaa
muhimu, na kusababisha uhaba wa chakula ambao ulikuwa mbaya zaidi kwasababu ya vikwazo
vya kimataifa vilivyowekwa kutokana na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
India: Wanawake waandamana usiku kulalamikia mauaji ya daktari tarajali
Chanzo cha picha, Jeet Sengupta
Makumi ya maelfu ya wanawake katika jimbo la West Bengal
waliandamana siku ya Jumatano usiku kupinga ubakaji na mauaji ya daktari tarajali
katika hospitali ya serikali huko Kolkata wiki iliyopita.
Maandamano hayo yalikuwa hitimisho la karibu wiki moja ya
maandamano ya ghasia yaliyochochewa na mauaji ya kikatili ya kijana huyo mwenye
umri wa miaka 31 katika Chuo cha Matibabu cha RG Kar Ijumaa iliyopita.
Baada ya zamu ya kuchosha ya saa 36, alikuwa amepitiwa
na usingizi kwenye chumba cha semina kutokana na ukosefu wa sehemu maalum ya
kupumzikia.
Asubuhi iliyofuata, wenzake waligundua mwili wake ukiwa
nusu uchi kwenye jukwaa, ukiwa na majeraha mabaya. Mfanyakazi wa kujitolea wa
hospitali amekamatwa kuhusiana na uhalifu huo.
Wakiitikia wito kutoka kwenye mitandao ya kijamii,
wanawake kutoka tabaka mbalimbali waliandamana katika jiji la Kolkata na jimbo
lote siku licha ya mvua kunyesha.
Ingawa maandamano kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani,
yalikumbwa na makabiliano kati ya polisi na kikundi kidogo cha watu
wasiojulikana ambao walivamia Hospitali ya RG Kar, eneo kulikotokea mauaji ya
daktari huyo, na kupora idara ya dharura.
Polisi walifyatua vitoa machozi kutawanya umati wa watu waliokuwa
wakisababisha ghasia. Baadhi ya magari ya polisi pia yaliharibika.
Rais wa zamani wa Argentina ashutumiwa kwa kumdhalilisha mpenzi wake
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waendesha mashtaka nchini Argentina wameanzisha uchunguzi
dhidi ya Rais wa zamani Alberto Fernandez, ambaye anatuhumiwa kumsababishia
majeraha mabaya mpenzi wake wa zamani.
Wiki iliyopita, mke wa rais wa zamani Fabiola Yañez, 43,
aliwasilisha malalamiko akimtuhumu kiongozi huyo wa zamani wa miaka 65 kwa
kumpiga wakati wa uhusiano wao, ambao ulifika tamati baada ya kuondoka
madarakani mnamo mwaka 2023.
Katika ushuhuda uliotolewa kutoka Uhispania, alielezea
jinsi alivyodai kuteswa na vitisho vya kisaikolojia na unyanyasaji wa kimwili
alivyopitia, na akamshutumu Bw Fernandez kwa kumlazimisha kutoa mimba.
Bw Fernandez amekanusha tuhuma zote. Hata hivyo, amepigwa
marufuku kuondoka nchini humo wakati uchunguzi ukiendelea.
Siku ya Jumatano, mwendesha mashtaka Ramiro Gonzales
aliwasilisha ombi rasmi mahakamani, akitaka mashtaka yafunguliwe dhidi ya rais
huyo wa zamani.
Uchunguzi huo unafanyika baada ya picha zinazoonekana
kumuonyesha Bi Yáñez akiwa na jicho jeusi na michubuko na kuonyeshwa kwenye
vyombo vya habari vya ndani, na kusababisha hasira nchini Argentina.
Bw Fernandez anakataa shutuma dhidi yake na kusema kuwa
hazina msingi wowote.
Chini ya sheria za Argentina, hakimu atatoa uamuzi wa
mwisho ikiwa kutakuwa na mashtaka yoyote au la.
Bw Fernandez alianza kujihusisha na siasa mwanzoni mwa
miaka ya 1980, katika siku za mwisho za udikteta wa kijeshi na alihudumu kama
rais kati ya 2019-23.
Hamas haitajiunga na mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza - afisa mwandamizi
Chanzo cha picha, EPA
Afisa mwandamizi wa Hamas ameiambia BBC kwamba
haitashiriki katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu usitishaji vita
wa Gaza na mpango wa kuwaachilia mateka ambao utaanza siku ya Alhamisi huko
Doha.
Kundi hilo lilitaka mpango wenye kutoa mwelekeo wa
utekelezaji makubaliano hayo na "halitashiriki mazungumzo kwa ajili ya
mazungumzo tu ili kuificha Israeli kuendeleza vita vyake", afisa huyo
alisema.
Alirejelea kuwa mpango huo unapaswa kuzingatia ule uliopendekezwa na kuainishwa na Rais wa
Marekani Joe Biden mwishoni mwa mwezi Mei na kuishutumu Israeli kwa kuongeza
"masharti mapya".
Waziri mkuu wa Israeli amekanusha kufanya hivyo na kusema
Hamas ndio imekuwa ikidai mabadiliko.
Mazungumzo hayo bado yanatarajiwa kufanyika hata bila ya
Hamas, kwani Marekani, Misri na Qatar ambao ni wapatanishi wanasema wanaweza
kuyatumia kupata mpango utakaotatua masuala yaliyosalia.
Mazungumzo hayo yalikabiliwa na changamoto kadhaa mwezi
uliopita na kusimamishwa tangu kuuawa kwa kiongozi wa kisiasa wa Hamas na
mpatanishi mkuu, Ismail Haniyeh, mjini Tehran.
Marekani inatumai kuwa kukamilisha makubaliano kunaweza
kuizuia Iran kulipiza kisasi cha mauaji dhidi ya Israeli - ambayo
haijathibitisha wala kukanusha kuhusika kwake - na kuepusha mzozo wa kikanda.
Columbia: Rais wa chuo kikuu ajiuzulu baada ya maandamano kuhusu Gaza
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Chuo Kikuu cha Columbia Minouche Shafik
amejiuzulu wadhifa wake huku kukiwa na mjadala wa uhuru wa kujieleza kuhusu
maandamano ya chuo hicho juu ya vita huko Gaza.
Kujiuzulu kwa Bi Shafik kunafanyika mwaka mmoja tu baada
ya kuchukua wadhifa huo katika chuo kikuu cha kibinafsi cha Ivy League huko New
York City, na wiki chache tu kabla ya muhula mpya kuanza.
Bi Shafik sasa ni rais wa tatu wa chuo kikuu cha Ivy
League kujiuzulu kutokana na jinsi alivyoshughulikia maandamano ya vita vya
Gaza.
Mnamo mwezi wa Aprili, Bi Shafik aliidhinisha maafisa wa
Idara ya Polisi ya New York kuvamia chuo hicho, uamuzi wenye utata ambao
ulisababisha kukamatwa kwa wanafunzi wapatao 100 waliokuwa kwenye jengo la chuo
hicho.
Kipindi hicho kiliashiria mara ya kwanza kwa watu wengi
kukamatwa katika chuo kikuu cha Columbia tangu maandamano ya kupinga Vita vya
Vietnam zaidi ya miongo mitano iliyopita.
Hatua hiyo ilichochea maandamano mengine katika vyuo
vingi nchini Marekani na Canada.
Katika barua pepe kwa wanafunzi siku ya Jumatano, Bi
Shafik alisema amepitia "kipindi cha machafuko na imekuwa vigumu kukabili maoni
tofauti katika jamii yetu"
"Imekuwa kipindi cha kufadhaisha - kwa jamii, kwangu
kama rais na kibinafsi – kujikuta mimi mwenyewe, wafanyikazi wenzangu, na
wanafunzi kama vitisho..."
Hasira ya wanafunzi juu ya jinsi Israeli inavyopigana
vita vyake dhidi ya Hamas imeibua maswali makali kwa viongozi wa vyuo vikuu,
ambao tayari wanatatizika na mijadala mikali ya vyuo kuhusu kile kinachotokea
Mashariki ya Kati.
WHO yatangaza mlipuko wa Mpox kuwa dharura ya kiafya duniani
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa
ugonjwa wa mpox katika baadhi ya maeneo ya Afrika kuwa dharura ya kiafya ya
umma.
Ugonjwa unaoambukiza sana - ambao zamani ulijulikana kama
monkeypox - umeua takriban watu 450 wakati wa mlipuko wa awali huko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Sasa umeenea katika maeneo ya Afrika ya kati na
mashariki, na wanasayansi wana wasiwasi kuhusu jinsi aina mpya ya ugonjwa huo
inavyoenea na kiwango chake cha juu cha vifo.
Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema uwezekano
wa ugonjwa huo kuenea zaidi ndani ya Afrika na kwingineko "kunatia
wasiwasi sana".
"Kukabiliana na ugonjwa huu kwa namna iliyoratibiwa ni
muhimu ili kusitisha janga hili na kuokoa maisha," alisema.
Mpox huambukizwa kupitia mguso wa karibu, kama vile
ngono, mguso wa ngozi hadi ngozi na kuzungumza au kupumua karibu na mtu
mwingine.
Husababisha dalili kama za mafua, vidonda vya ngozi na
inaweza kusababisha kifo, na kesi nne kati ya 100 husababisha kifo.
Kuna aina mbili kuu za mpox - Clade 1 na Clade 2.
Dharura ya awali ya afya ya umma, iliyotangazwa mwaka wa
2022, ilisababishwa na Clade 2 ambayo si kali. Hata hivyo, wakati huu ni Clade
1 mbaya zaidi - ambayo imeua hadi 10% ya wale wanaougua katika milipuko ya awali
– idadi hii inaongezeka.
Tangu wakati huo, ugonjwa wa mpox umegunduliwa katika
nchi nyingine za Afrika - ikiwa ni pamoja na Burundi, Jamhuri ya Afrika ya
Kati, Kenya na Rwanda.
Ukraine yaendelea kusonga mbele ndani ya eneo la Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Eneo la mpaka wa magharibi mwa Urusi la Kursk lilikumbwa
na shambulio la kushtukiza wiki iliyopita, na kusababisha mamlaka ya Urusi
kutangaza hali ya hatari katika eneo hilo.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema wanajeshi
wamesonga mbele kilomita 1-2 zaidi ndani ya eneo la Kursk tangu Jumatano
asubuhi, na pia wamewakamata wanajeshi 100 wa Urusi.
Lakini Urusi inadai kuwa imefanikiwa kusitisha hatua za
Ukraine za kusonga mbele zaidi.
Sasa katika wiki yake ya pili, huu ni uvamizi mkubwa
zaidi wa Ukraine ndani ya Urusi tangu Moscow ilipoanzisha uvamizi wake mnamo mwaka
2022.
Kiasi cha eneo la Urusi lililonyakuliwa hakijulikani,
huku nchi zote mbili zikitoa kauli zinazokinzana.
Kamanda wa kitengo cha kikosi maalum cha Chechen Akhmat,
Meja Jenerali Apti Alaudinov aliwaambia watazamaji kwenye Televisheni
inayodhibitiwa na serikali ya Urusi, Channel One, kwamba vikosi vya Urusi viko
karibu "kuwazuia" wanajeshi wa Ukraine kuendelea kusonga mbele.
Lakini katika video moja, mkuu wa jeshi Oleksandr Syrskyi
alisema wanajeshi wa Ukraine sasa wanadhibiti kikamilifu mji wa mpakani wa
Kursk wa Sudzha.
Hata hivyo, BBC haikuweza kuthibitisha dai hili kwa
uhuru, lakini ripoti ya televisheni ya Ukraine iliyorekodiwa kutoka ndani ya
mji ilionyesha wanajeshi wa Ukraine wakiondoa bendera ya Urusi kutoka kwenye shuleni
moja.
Huku kukiwa na madai ya Ukraine kupata mafanikio ya kudhibiti
maeneo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine Heorhiy Tykhy alisema hawana
nia ya "kuchukua" eneo la Urusi. "
Urusi ikikubali kurejesha amani ya haki haraka
iwezekanavyo... ndivyo uvamizi wa vikosi vya ulinzi vya Ukraine nchini Urusi
utakavyofikia tamati," aliwaambia waandishi wa habari.
Katika mkutano wa awali na maafisa wa serikali, Bw
Zelensky alisema atafikiria kuanzisha "ofisi za makamanda wa kijeshi"
katika eneo hilo.