Israeli inasubiri na kujiandaa kujibu: Kwa nini Nasrallah alitishia mji wa Haifa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel inajiandaa, kijeshi na kiraia, kukabiliana na uwezekano wa mashambulizi ya Iran au Hezbollah ya Lebanon, au yote mawili ya kulipiza kisasi cha mauaji ya kamanda wa kijeshi wa chama hicho, Fouad Shukr, na kile ambacho mamlaka ya Israeli pia inashutumiwa - mauaji ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati za Hamas, Ismail Haniyeh, katika mji mkuu wa Iran, Tehran.
Israeli ilipeleka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga, iliongeza kiwango cha tahadhari cha vikosi vyake kwa kiwango cha juu, na manispaa za jiji zilipokea maagizo ya kuwapa wakazi habari na maagizo kuhusu maeneo ya ulinzi wa umma na maeneo ya usambazaji wa maji katika hali ya dharura.
Katika mji wa Haifa, kwa mfano, eneo la kuegesha magari katika moja ya hospitali maarufu liliandaliwa kuwa hospitali ya dharura iliyotengwa kwa ajili ya visa vya dharura, ili kutoa huduma ndani ya magari ya wagonjwa kwa ajili ya majeruhi, ikiwa jiji litashambuliwa.
Hii ni sehemu ya maandalizi ya Manispaa ya Haifa kutokana na uwezekano wa mashambulio ambayo Israeli haijui, na haijaamua yatakuwaje, na iwapo mashambulio ya kulipiza kisasi na namna watakavyokabiliana nayo yanayotarajiwa yataongeza uwezekano wa kuongezeka kwa ghasia za mapigano zaidi au la.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Haifa haiko tayari kwa mapambano"
Kauli hii inarudiwa mara kwa mara na wakazi wengi wa mji huo, ambao ni nyumbani kwa takriban Waisraeli 300,000, asilimia 12 kati yao wakiwa ni Waarabu wa Israeli.
Miongoni mwa wakaazi hao ni Yoav Haifa, ambaye anaamini kwamba serikali ya Israel na jeshi litauweka mji wa Haifa katika mzunguko wa kulenga na kuwa kitovu cha mapambano, kwa sababu ya kile anachoelezea kama "mauaji yao ya hivi karibuni."
"Kulengwa kwa viwanda vya kemikali kwenye eneo hilo kunaweza kuwa hatari kwa mamia ya maelfu ya wakazi," Yoav alituambia wakati tulipomuuliza ni nini wakazi wa jiji hilo wanachohofia zaidi.
Anasema kuwa nyumba nyingi za Haifa hazina makazi au maeneo salama, na kwamba mitaa haina maeneo ya ulinzi.
Kwa kweli, majengo mengi huko Haifa, ni ya zamani, hayana maeneo kama hayo yanayoweza kutumiwa kama ngome ya mapigano.
Katika miaka ya 1990, baada ya kuzuka kwa vita vya pili vya Ghuba mwaka 1991, sheria ya Israeli ilieleza kwamba wakandarasi wa ujenzi lazima wahakikishe ujenzi wa hifadhi ya watu katika kila nyumba ya makazi.
Lakini idadi kubwa ya nyumba za mji huo, ikiwa ni pamoja na zile zinazokaliwa na Waarabu wa Israeli, hazina maeneo yoyote ya kujikinga kabisa, kama zilivyojengwa kabla ya sheria hii kutungwa.
Wizara ya Ulinzi wa Mazingira ya Israel inasema kuwa Haifa ina maghala mengi na viwanda vya kemikali hatari, jambo ambalo linaleta wasiwasi mkubwa kwa wakazi.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Maeneo ya kuegesha magari suluhisho la ukosefu wa makazi"
Msemaji wa manispaa ya Haifa Gil Miller ameiambia BBC kuwa manispaa hiyo inafahamu kuwa baadhi ya wakazi hawana makazi ya hifadhi katika nyumba zao, hali ambayo imewafanya kuchagua maeneo ya kuegesha magari kuzunguka mji huo, ambayo ni ghorofa kadhaa chini ya ardhi, kama sehemu za ulinzi.
Msemaji huyo aliongeza kuwa maeneo hayo yanaweza kuchukua maelfu ya watu, baada ya manispaa kuandaa zaidi ya makazi 100 yaliyo na jenereta za umeme ili kukabiliana na kukatika kwa umeme.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mahali salama ni zaidi ya nusu saa kutoka kwangu."
Mkazi wa Haifa Halim Haddad amekasirishwa na maandalizi ya manispaa hiyo kwa ajili ya uwezekano wa shambulio. Anasema eneo ambalo manispaa imemuandalia ili achukue hifadhi endapo kutatokea mashambulizi ni zaidi ya nusu saa kutoka nyumbani kwake, na hivyo kumfanya ashindwe kwenda huko.
Katika mahojiano na BBC, Haddad aliongeza kwamba vitongoji vya zamani vya Waarabu havina utayari wa vita na kwamba kuna kile anachokielezea kama "ubaguzi wa rangi" unaotokea katika mji huo, katika suala hili, kati ya wakazi wa Kiarabu na Wayahudi.
Lakini mamlaka ya Israeli kwa kawaida hukanusha tuhuma hizo, na kusema kuwa raia wote wa Israeli wanatendewa sawa, bila ubaguzi wa aina yoyote.

Chanzo cha picha, Ibrahim Kamal Hamad/Anadolu via Getty Images
Kwa nini Katibu Mkuu wa Hezbollah aliitishia Haifa?
Haifa ni moja ya miji mikubwa nchini Israeli, na ina maeneo mengi ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na vituo muhimu vya kijeshi, maeneo yenye viwanda vya kemikali, na bandari kuu ya jiji.
Katibu Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah amesema kuwa Haifa huenda ni miongoni mwa maeneo yatakayolengwa na chama hicho katika kujibu mauaji ya kamanda wa jeshi la Israel Fouad Shukr, ambaye aliuawa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa waangalizi, Haifa inaweza kuwa ndani ya msururu wa mapigano, kutokana na umuhimu wake wa kimkakati na kiuchumi, eneo lake karibu na mpaka wa Lebanon, na pia kwa sababu Hezbollah ilitangaza kuwa ina picha za kina za maeneo kadhaa ya kimkakati huko, kupitia kile ilichosema ni kuingizwa kwa ndege yake ya reconnaissance katika anga lake mapema.

Chanzo cha picha, Ibrahim Kamal Hamad/Anadolu via Getty Images
Israel inakabiliana vipi na vitisho vya Iran na Hezbollah
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika siku za mwanzo baada ya mauaji ya Shukr na Haniyeh, Israeli iliridhika kuwa katika hali ya kusubiri na kutarajia. Baada ya hapo, maafisa waliamua kupitisha sera ya vitisho, kupitia taarifa za mara kwa mara za viongozi waandamizi wa kisiasa na kijeshi, ambapo walisema kuwa shambulio lolote dhidi ya Israeli litakabiliwa kwa majibu makali.
Wakati hali ya wasiwasi na hofu miongoni mwa Waisraeli ikiendelea, msemaji wa jeshi la Israeli alijitokeza angalau mara tatu kutuliza maoni ya umma, akisema kwamba hakuna mabadiliko katika maagizo ya awali yaliyotolewa nyumbani.
Mazingira ya utata, matarajio, na labda maandalizi ya kukabiliana na kisasi yanatawala eneo la Israeli, kutokubaliana kati ya Waisraeli, kati ya wale wanaotoa wito wa kupanuliwa kwa mapambano ya kijeshi na Iran na Hezbollah, na wale wanaoamini kwamba Israeli, kijeshi, haiko tayari kwa vita kama hivyo.
Aidha, hivi karibuni kumekuwa na wito wa kuanzisha " shambulizi la kijeshi mapema," ambao, kwa mujibu wa duru za vyombo vya habari vya Israeli, umekataliwa na huduma za usalama, ambazo zinaamini kuwa hii sio miongoni mwa njia hali bora za kukabiliana na vitisho vya sasa kutoka Iran na Hezbollah.
Katika siku chache zilizopita, Waisraeli wengi wamekuwa wakielekea madukani kuhifadhi chakula cha msingi, ambacho kitahitajika haraka ikiwa kutakuwa watajipata katika mapigano huku jeshi likitoa maagizo ya kuwahimiza watu kununua betri na vifaa vya huduma ya kwanza, ikitarajia mapigano.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, wachambuzi wa masuala ya kijasusi wanayaonaje maendeleo haya?
Maeneo ya mpakani kati ya Lebanon na Israel hayajakuwa kimya katika kipindi hiki cha matarajio.
Israel imeongeza mashambulizi yake ya anga kusini mwa Lebanon na kuendelea kulenga makundi ya Hezbollah, wakati chama hicho kikilenga maeneo ya Galilaya ya Juu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani, na kufikia miji kama vile Acre na Nahariya, ambayo ilielezewa kama maendeleo ya ubora, katika mazingira ya kuongezeka kwa mapigano kati ya pande hizo mbili, dhidi ya hali ya nyuma ya vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7.
Katika muktadha wa makabiliano ya hivi karibuni, Hezbollah ilitangaza kuwa ililenga kambi za kijeshi za Israeli, wakati Israeli ilipotangaza kuwa Waisraeli kadhaa, ikiwa ni pamoja na wanajeshi, walijeruhiwa kutokana na mashambulizi haya, na pia kutokana na kile kilichoelezwa kama "kombora la kuzuia" lililolipuka kwa makosa karibu na raia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa wa zamani wa ujasusi wa Israel, Avi Melamed, anasema kuwa moja ya masuala muhimu anayoyazingatia katika hatua hii yanahusiana na matokeo yanayotarajiwa ya shambulio lolote ambalo Israel inaweza kukumbana nalo Iran au Hezbollah.
"Kwa maneno rahisi, ikiwa Israeli italengwa kwa namna inayofanana na shambulio lililotekelezwa na Iran mwezi Aprili mwaka uliopita, na matokeo yake ni yale yale, basi natarajia mambo yataishia hapo," alisema, kwa kuzingatia kwamba hali hii inaweza kusababisha vita.
Lakini aliiambia BBC kwamba jibu lolote ambalo linaweza kusababisha, hata kwa makosa, mauaji ya Waisraeli au kulenga miundombinu nchini Israeli, bila shaka litamaanisha kuzuka kwa vita, akibainisha kuwa ukosefu wa maelekezo ya wazi kutoka kwa jeshi kwa la Israeli, wakati huu kuhusu jinsi ya kukabiliana na shambulio lolote.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












