Hospitali ya chini ya ardhi ya Israel inayojiandaa kwa mashambulizi

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Jenny Hill
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Haifa, Israel
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ndani kabisa ya mji wa kaskazini mwa Israeli wa Haifa, kuna hospitali kubwa ya chini ya ardhi.
Mamia ya vitanda vimepangwa ndani ya kuta zake za zege.
Kuna vyumba vya upasuaji, wadi ya wajawazito, na vifaa vya matibabu vilivyowekwa kwenye kona
Lakini bado hakuna wagonjwa .
Kituo cha Matibabu cha Rambam kilichimba shimo hili baada ya vita vya Israel-Hezbollah vya 2006.
Kwa kawaida ni maegesho ya orofa nyingi lakini inaweza kubadilishwa kuwa hospitali kwa chini ya siku tatu.
Imekuwa katika hali ya utayari tangu muda mfupi baada ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 na operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza.
Kituo hicho kina zaidi ya vitanda 2,000. Katika tukio la shambulio kubwa kwa Israeli, itachukua wagonjwa waliopo kutoka kwa kituo cha matibabu cha ardhini na hospitali zingine za karibu. Na kuna nafasi pia ya kutibu majeruhi .
Huku tishio la vita vya eneo zima likikaribia kufuatia kuuawa kwa kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismael Haniyeh na kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukr wiki iliyopita, madaktari hapa wanasema wako tayari kwa shambulio kuu dhidi ya Haifa.
"Ni Lini, lini, ni lini itafanyika? Hakuna anayejua. Tunalizungumzia sana," anasema Dk Avi Weissman, mkurugenzi wa matibabu wa kituo hicho.
Anaongeza kuwa watu wana wasiwasi. Yeye na wafanyakazi wake wanatumai tu kwamba ongezeko lolote la vurugu halitadumu kwa muda mrefu.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Karibu na hospitali kuna mtazamo mzuri juu ya jiji na bandari yake inayostawi.
Kutoka baharini, meli za mafuta zinapita kwenye maji.
Lakini ukaribu wa Haifa na Lebanon - na roketi za Hezbollah - unaiacha katika hatari.
Ukiangalia njia za safari za meli na unaweza kuona mpaka.
Watu wanaoishi hapa wamezoea kufanya mazoezi ya dharura kila baada ya miezi michache. Watoto wa shule hupitia mara kwa mara nini cha kufanya katika tukio la shambulio likifanyika.
Wenzi wa ndoa wachanga tuliokutana nao katikati mwa jiji walieleza kuishi na tisho hilo.
"Ni kama bomu la muda," anasema mwanamke huyo. "Dakika yoyote sasa king'ora kinaweza kulia. Je, nitakufa? Nitapata muda wa kwenda kwa familia yangu?"
Wengine hawajali sana. Katika duka lake jipya la kahawa lililofunguliwa, Luai alimimina cappuccino na kusema kuwa amezoea hali hiyo.
"Watu wanaogopa. Siogopi," alisema.
Lakini katika Ukumbi wa Jiji la Haifa, meya anakiri kukosa usingizi usiku. Yono Yahav yuko katika miaka yake ya themanini na uzito wa uwajibikaji umejaa macho yake.Pia alisimamia jiji wakati wa vita vya 2006.
"Nina huzuni sana juu ya hali hii," alisema. "Kuna uma Mashariki ya Kati. Viongozi wanahusika tu na uharibifu, kuua, kupigana badala ya kujenga."
Haifa ni kile kinachoitwa "mji mchanganyiko"; mahali ambapo idadi kubwa ya Waarabu wa Israeli wanaishi pamoja na Wayahudi wa Israeli. Bw Yahav anasema ni jamii yenye amani, ambayo inafanya mzozo uliopo kuwa mchungu zaidi.
Amani, anasisitiza, bado inawezekana.
Na diplomasia ya kimataifa inaendelea hata kama madaktari wa Haifa wanatayarisha hospitali yao ya ngome hii.
Bado kuna matumaini, labda, hawatawahi kuitumia.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












