Ukatili dhidi ya wanawake: Je, sheria inaweza kuutokomeza?

Miatta Gray points to a poster

Chanzo cha picha, MIATTA GRAY

    • Author, Tabitha Mwai
    • Nafasi, BBC News

“Dada yangu mdogo alivuja damu hadi kufa baada ya sote wawili kukeketwa,” anasema Miatta Gray.

Akiwa na umri wa miaka 11, mwanamke huyo wa Kiliberia alipelekwa vijini pamoja na dadake mdogo kukeketwa, jambo ambalo ni la kawaida nchini humo.

“Nilipopata fahamu, hakuna mtu aliyeniambia alipo dada yangu. Siku chache baadaye, binamu yangu aliniambia kwamba alikuwa amefariki,” anasema.

Miatta amelazimika kufanyiwa upasuaji mara mbili kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na ukeketaji.

Mwaka mmoja baada ya hilo kutokea, Miatta alidhulumiwa kingono na mtu wa karibu wa familia.

"Ilikuwa ya kikatili sana, nilikuwa mgonjwa sana na hakuna mtu aliniyesikiliza," anasema.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa chini ya asilimia 40 ya wanawake wanaofanyiwa ukatili huomba msaada. Hali hii inafanywa kuwa mbaya zaidi na ukosefu wa usawa wa kijinsia na kukubalika kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake katika nchi nyingi.

Pia uanaweza kusoma:

Kwa Miatta, ilionekana kana kwamba hakuna mtu aliyemwamini na kwamba alikuwa akilaumiwa kwa kile kilichotokea.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hakuwa na msiri, kwa kuwa amefiwa na dada yake na kwa sababu alikuwa ametenganishwa na mama yake.

“Mimi ni manusura wa ulanguzi wa watoto. Nilichukuliwa na mama yangu nikiwa na mwaka mmoja,” asema.

Miatta aliunganishwa tena na mama yake akiwa na umri wa miaka 14. Mama yake hakujua kwamba binti yake alikuwa amesafirishwa, na alikuwa akimtafuta kwa muda wote huo. Ilikuwa ni bahati ya kukutana tena huku mamake akipigana kumzuia Miatta asiozwe akiwa mtoto.

"Ni kwa sababu tu mama yangu alipinga ndoa ya utotoni ndio nilifanikiwa kutoroka," asema Miatta.

Akiwa mtu mzima, Miatta alijihusisha na uhusiano mbaya ambao uliathiri vibaya afya yake ya akili.

"Nimejaribu kujiua mara nyingi kwa sababu ya kiwewe," asema, akiongeza kwamba wakati huo, alihisi mpweke duniani.

Miatta anasema mamake alikuwa mwamba wake na alipofariki, Miatta aliamua kumuangazia binti yake mwenyewe. Mawazo ya nini kingeweza kumpata binti yake bila ulinzi wake yalimpa nguvu ya kuendelea kupambana.

Mwanamke ameketi kitandani akiwa ameshika kitambaa

Chanzo cha picha, Getty Images

Umoja wa Mataifa unafafanua unyanyasaji dhidi ya wanawake kama kitendo chochote cha unyanyasaji wa kijinsia ambacho kinasababisha, au kinaweza kusababisha madhara ya kimwili, kingono, au kiakili au mateso kwa wanawake.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mwanamke mmoja kati ya watatu duniani kote hufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono, hasa unaofanywa na mwenzi wa karibu. Zaidi ya wanawake milioni 640 walio na umri wa miaka 15 na zaidi wamefanyiwa ukatili wa karibu na wenza.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ubakaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake umetangazwa kuwa janga la kitaifa na serikali za Liberia, Puerto Rico, Nigeria, Afrika Kusini na Sierra Leone.

"Kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake ni vita vinavyohitaji kujitolea," anasema Miatta.

Kama mwathirika wa aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia, sasa anaendesha Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) nchini Liberia linalojitolea kupambana na unyanyasaji dhidi ya wanawake. Ameazimia kuwasaidia wengine wanaokabiliwa na matatizo sawa na yeye.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa angalau nchi 162 zina sheria dhidi ya unyanyasaji wa nyumbani na 147 zina sheria dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia mahali pa kazi. Walakini, hii sio kila wakati husababisha kutekelezwa au kupunguza shida.

Changamoto za kisheria

Mwanamke ameshikilia bango linalosomeka 'wanawake wanajitahidi' wakati wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake 2022 nchini Indonesia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Angalau wanawake watatu wanakumbana na unyanyasaji wa kingono nchini Indonesia kila baada ya saa mbili, kulingana na takwimu za serikali

Indonesia ni nchi moja ambayo hivi karibuni imebuni sheria mpya.

Kulingana na takwimu za hivi punde za serikali ya Indonesia, karibu wanawake watatu hukabiliwa na ukatili wa kijinsia nchini humo kila baada ya saa mbili.

Mnamo Aprili 2022, bunge lilipitisha sheria ya Uhalifu wa Unyanyasaji wa Kijinsia ambayo ilipanua ufafanuzi wa ubakaji kujumuisha ubakaji wa ndoa na kuanzisha mbinu inayowalenga waathiriwa kushughulikia kesi.

"Ubakaji katika ndoa mara nyingi hauripotiwi na hata inaporipotiwa, polisi huona kama suala la kibinafsi la familia," anasema Theresia Iswarini kamishna wa Komnas Perempuan, Tume ya Kitaifa ya Ukatili Dhidi ya Wanawake ambayo ilianzishwa kusaidia waathiriwa kupata huduma na kujiandikisha. uhalifu.

Kulingana na Theresia, visa vingi vya dhuluma dhidi ya wanawake nchini Indonesia ni unyanyasaji wa nyumbani dhidi ya wake na mabinti.

"Ni changamoto kwa waathirika kutoa taarifa kutokana na utamaduni wa mfumo dume na msisitizo wa haki urejeshaji. Hata hivyo, sheria inaamuru kesi zote za unyanyasaji wa majumbani ziripotiwe,” anasema.

"Sheria ya jinai ya unyanyasaji wa kijinsia ina kifungu kinacholinda waathiriwa na inawapa fidia."

"Waathiriwa sasa wana haki ya kusahauliwa na wanaweza kuomba mahakama kufuta picha au video zao za ngono mtandaoni," anasema.

Ingawa Theresia anasema kuwa sheria mpya inaunga mkono wanawake, anabainisha kuwa sheria nyingine ambayo inaharamisha ngono nje ya ndoa na kuadhibu matendo machafu, ambayo katika baadhi ya matukio ni pamoja na kumbusu, inaweza kutumika kuwalenga waathirika.

Kulingana na Theresia ni asilimia 30 pekee ya kesi zinazoripotiwa kwa polisi huhukumiwa mahakamani jambo ambalo linaonyesha bado kuna vizuizi vya kupata haki.

Utafiti wa Komnas Perempuan unaonyesha kuwa ugumu wa kupata huduma jumuishi katika ngazi ya wilaya na jiji ni kikwazo cha kupata haki. Suala jingine ni kwamba vifaa vya serikali pia vimejikita katika kisiwa kikuu cha Indonesia, Java, na si kuenea kote nchini ambako nyumba salama na huduma za usaidizi ni ndogo. Waathiriwa bado wanapaswa kulipia vipimo vya DNA.

Utafiti pia unasema kuwa watekelezaji sheria na watoa huduma mara nyingi huwalaumu waathiriwa na hawasikilizi hadithi zao.

"Ili kusaidia waathirika serikali za mitaa zinahitaji kutoa huduma jumuishi na marekebisho ya sera za kibaguzi," anasema Theresia.

Kamishna huyo anaamini kuwa kuna haja ya kuwa na mbinu kamili zaidi ya kushughulikia suala hilo.

"Hatua za kuzuia ni pamoja na utekelezaji wa sheria, kupunguza umaskini, kukabiliana na rushwa, kuzuia migogoro na kukabiliana na dharura inayozingatia jinsia," anasema.

Mageuzi ya Liberia

Miatta Gray akitembea pamoja na wanawake wengine

Chanzo cha picha, MIATTA GRAY

Nchini Libeŕia, baada ya miaka 14 ya vita, nchi hiyo imeanzisha idadi ya sheŕia na afua za kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Sheria ya Ubakaji ya mwaka 2005 inaamuru adhabu ya miaka 10 au kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia ukubwa wa kosa.

Mnamo 2008, mahakama maalum ya uhalifu ilianzishwa ili kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kijinsia.

Mnamo 2019, Sheria ya Unyanyasaji wa Majumbani ambayo inalenga kuwalinda waathiriwa na walionusurika ilipitishwa.

"Kwa miaka michache, kulikuwa na uchunguzi wa haraka na mashtaka. Mambo yamebadilika katika miaka sita iliyopita,” anasema Miatta, ambaye anaendelea kuboresha maisha ya wanawake.

imetafsiriwa na Ambia Hirsi