Wapalestina wasimulia unyanyasaji katika jela za Israel

f

Chanzo cha picha, Israel Prison Service

Maelezo ya picha, Magereza ya Israel yamefurika wafungwa wa Kipalestina baada ya idadi hiyo kuongezeka hadi takriban 10,000 tangu mashambulizi ya Oktoba.
    • Author, Na Paul Adams
    • Nafasi, BBC Jerusalem
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Tahadhari: Makala hii ina maelezo ambayo huenda ikawaathiri baadhi ya wasomaji.

Shirika kuu la kutetea haki za binadamu nchini Israel linasema hali ndani ya magereza ya Israel wanamoshikiliwa wafungwa wa Kipalestina ni ya mateso.

Ripoti ya shirika la B'tselem yenye kichwa "Karibu Kuzimu", ina ushuhuda kutoka kwa wafungwa 55 wa Kipalestina walioachiliwa hivi karibuni, ambao ushuhuda wao wa wazi unaonyesha kuzorota kwa hali ya magereza tangu kuanza kwa vita vya Gaza miezi 10 iliyopita.

Ni ripoti ya hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa ripoti, ikijumuisha ripoti ya wiki iliyopita ya Umoja wa Mataifa , ambayo inaangazia madai ya kutisha ya unyanyasaji dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

B'tselem inasema ushuhuda ambao watafiti wao wamekusanya ni ya kuaminika kabisa na mashahidi walitoa maelezo yanayofanana.

"Wote walituambia kitu kimoja," anasema Yuli Novak, mkurugenzi mtendaji wa B'tselem.

"Mfumo wa magereza ya Israel kwa ujumla, kuhusu Wapalestina, uligeuka kuwa mtandao wa kambi za mateso."

Unaweza pia kusoma:

'Seli zilizojaa, chafu'

Tangu mashambulizi mabaya ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban Waisraeli1,200 na raia wa kigeni waliuawa, idadi ya wafungwa wa Kipalestina imeongezeka maradufu na kufikia 10,000.

Baadhi ya magereza ya Israel yanaendeshwa na jeshi, huku mengine yanayoendeshwa na huduma za magereza nchini humo yakizidiwa na idadi kubwa ya mahabusu.

Magereza yamefurika, huku wafungwa 12 au zaidi wakati mwingine wakiishi ndani ya seli ambazo zimejengwa kwa ajili ya kuwahifadhi wafungwa wasiozidi ya sita.

Ripoti ya B'tselem inaelezea msongamano wa seli, na uchafu, ambapo baadhi ya wafungwa hulazimika kulala chini, wakati mwingine bila magodoro au blanketi.

Baadhi ya wafungwa walikamatwa baada ya mashambulizi ya Hamas. Wengine walikusanywa huko Gaza wakati uvamizi wa Israeli ulipoanza, au walikamatwa Israeli au Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

Wengi waliachiliwa baadaye bila kufunguliwa mashtaka.

g
Maelezo ya picha, Firas Hassan anasema "maisha yalibadilika kabisa" kwake kama mfungwa katika jela ya Israel baada ya mashambulizi ya Oktoba 7.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Firas Hassan alikuwa tayari gerezani mwezi Oktoba, akishikiliwa chini ya "vizuizi vya kiutawala", hatua ambayo washukiwa - ingawa imetumika kwa wingi kwa Wapalestina - wanaweza kuzuiliwa, zaidi au chini ya muda usiojulikana, bila kufunguliwa mashtaka.

Israel inasema kuwa matumizi yake ya sera ni muhimu, na yanaambatana na sheria za kimataifa.

Firas anasema alishuhudia yake jinsi hali ilivyozidi kuzorota baada ya tarehe 7 Oktoba.

"Maisha yalibadilika kabisa," aliniambia tulipokutana huko Tuqu', kijiji kilichopo katika Ukingo wa Magharibi kusini mwa Bethlehem.

"Ninakiita kile kilichotokea tsunami."

Bw Hassan amekuwa akiingia na kutoka jela tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini, akishtakiwa mara mbili kwa kuwa mwanachama wa Palestina Islamic Jihad, kundi lenye silaha lililotajwa kuwa kundi la kigaidi na Israel na sehemu kubwa ya Magharibi.

Hafichi ushirika wake wa zamani, akisema alikuwa "mtendaji".

Akiwa anafahamu ugumu wa maisha gerezani, alisema hakuna kilichomtayarisha kwa kile kilichotokea wakati maafisa walipoingia katika chumba chake siku mbili baada ya tarehe 7 Oktoba.

"Tulipigwa vibaya na maafisa 20, wanaume waliofunika nyuso zao kwa vitambaa, mbwa na bunduki," alisema.

“Tulifungwa mikono nyuma, macho yetu yakiwa yamefungwa, tukapigwa sana. Damu ilikuwa ikinitoka usoni. Waliendelea kutupiga kwa dakika 50. Niliwaona kupitia chini ya kifuniko cha macho. Walikuwa wakitupiga picha huku wakitupiga.”

Hatimaye Bw Hassan aliachiliwa, bila kufunguliwa mashtaka, mwezi wa Aprili, wakati ambapo alisema alikuwa amepoteza uzito wa kilo 20 wa mwili.

Video iliyorekodiwa siku ya kuachiliwa kwake inaonyesha mtu dhaifu.

"Niliishi miaka 13 gerezani hapo awali," aliwaambia watafiti wa B'tselem baadaye mwezi huo, " lakini sikuwahi kukumbana na jambo kama hilo."

g
Maelezo ya picha, Sari Khourieh, Mwarabu wa Israel, anasema hakukuwa na sheria au amri ndani ya gereza la kaskazini mwa Israel ambako alizuiliwa kwa siku 10.

Lakini sio tu Wapalestina kutoka Gaza na Ukingo wa Magharibi wanaozungumzia unyanyasaji katika magereza ya Israel.

Raia wa Israeli, kama Sari Khourieh, mwanasheria wa Kiarabu kutoka Haifa, anasema imetokea kwake pia.

Bw Khourieh alizuiliwa katika gereza la Megido kaskazini mwa Israel kwa siku 10 mwezi uliopita wa Novemba. Polisi walisema kwamba machapisho yake mawili ya Facebook yametukuza vitendo vya Hamas - shtaka lililotupiliwa mbali haraka.

Lakini uzoefu wake mfupi wa gerezani - wa kwanza - karibu umuue.

“Wamepoteza akili tu,” asema kuhusu matukio aliyoshuhudia huko Megido.

“Hakukuwa na sheria. Hakukuwa na utaratibu ndani.”

Bw Khourieh anasema aliepushwa na unyanyasaji mbaya zaidi. Lakini anasema alishangazwa na jinsi wafungwa wenzake walivyotendewa.

"Walikuwa wakiwapiga vibaya bila sababu," alituambia. "Walikuwa wakipiga kelele, vijana, 'hatukufanya chochote. Si lazima utupige.'”

Alipoongea na mahabusu wengine, harakaharaka akagundua kuwa alichokiona si cha kawaida.

"Hali haikuwa bora zaidi kabla ya Oktoba 7, lakini baadaye kila kitu kilikuwa tofauti." waliniambia.

Wakati wa kipindi kifupi katika eneo la s mahabusu za kutengwa zinazojulikana na wafungwa kama Tora Bora ( kumaanisha mtandao wa mapango wa al-Qaeda nchini Afghanistan), Bw Khourieh anasema alimsikia mfungwa aliyepigwa akiomba msaada wa matibabu katika mahabusu iliyo karibu.

Kulingana na Bw Khourieh, madaktari walijaribu kumzindua, lakini alifariki muda mfupi baadaye.

w
Maelezo ya picha, "Unyanyasaji unaoendelea, unyanyasaji wa kila siku, unyanyasaji wa kimwili na unyanyasaji wakiakili, fedheha, kukosa usingizi, watu wana njaa." anasema Yuli Novak B'tselem mkurugenzi mtendaji

Kulingana na ripoti ya wiki iliyopita ya Umoja wa Mataifa, "matangazo ya IPS (Huduma ya Magereza ya Israel) na mashirika ya wafungwa yanaonyesha kuwa Wapalestina 17 wamekufa wakiwa chini ya ulinzi wa IPS kati ya tarehe 7 Oktoba na 15 Mei".

Wakati huo huo, wakili wa kijeshi wa Israel tarehe 26 Mei alisema kwamba taasisi hiyo inachunguza vifo vya wafungwa 35 wa Gaza waliokuwa chini ya ulinzi wa jeshi.

Miezi kadhaa baada ya kuachiliwa huru kwa Bw Khourieh - tena, bila kufunguliwa mashtaka - wakili bado anajitahidi kuelewa kile alichoshuhudia huko Megido.

"Mimi ni Muisraeli…mimi ni mwanasheria," alituambia. "Nimeona ulimwengu nje ya gereza. Sasa niko ndani. Ninaona ulimwengu mwingine."

Imani yake katika uraia na utawala wa sheria, anasema, imevunjika "Yote ilivunjikabaada ya uzoefu huu."

Tunalaumu mamlaka zinazohusika kwa unyanyasaji mkubwa wa wafungwa wa Kipalestina.

Jeshi lilisema "linakataa madai ya moja kwa moja ya unyanyasaji wa kupangwa wa wafungwa".

"Malalamiko kuhusu utovu wa nidhamu au masharti yasiyoridhisha ya kizuizini," jeshi lilituambia, "yanatumwa kwa vyombo husika katika IDF, na yanashughulikiwa ipasavyo."

Huduma ya magereza ilisema "haikuwa na ufahamu wa madai uliyoelezea, na tunavyojua, hakuna matukio kama hayo yaliyotokea".

f

Chanzo cha picha, Channel 13

Maelezo ya picha, Jeshi la Magereza la Israel linakanusha madai ya unyanyasaji, likisema "hakuna matukio kama hayo yaliyotokea"

Tangu tarehe 7 Oktoba, Israel imekataa kutoa idhini kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ya kuwatembelea wafungwa wa Kipalestina, kulingana na sheria za kimataifa.

Hakuna maelezo yoyote ambayo yametolewa kuhusu kukataliwa kwa idhini hiyo, lakini serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imeeleza mara kwa mara kusikitishwa kwake na kushindwa kwa ICRC kupata ufikiaji wa Israel na mateka wengine wanaozuiliwa Gaza.

Chama cha Haki za Kiraia nchini Israel (ACRI) kimesihutumu serikali kwa "kukiuka sheria za kimataifa".

Wiki iliyopita, ghasia za umma ziliibua kutokana na vitendo wanavyotendewa wafungwa wa Kipalestina , huku waandamanaji wa mrengo wa kulia - ikiwa ni pamoja na wabunge wa Israel - wakijaribu kwa nguvu kuzuia kukamatwa kwa askari wanaotuhumiwa kumnyanyasa kingono mfungwa kutoka Gaza katika kituo cha kijeshi cha Sde Teiman.

Baadhi ya walioandamana walikuwa wafuasi wa waziri wa usalama wa Israel mwenye msimamo mkali, Itamar Ben Gvir, kiongozi mkuu wa huduma ya magereza.

Bw Ben Gvir amejigamba mara kwa mara kuwa chini ya uangalizi wake, hali za wafungwa wa Kipalestina zimezorota sana.

"Ninajivunia kwamba wakati wangu tulibadilisha masharti yote," aliwaambia wabunge wa bunge la Israel, Knesset, wakati wa kikao mwezi Julai.

Kwa B'Tselem, Bw Ben Gvir anabeba jukumu zito kwa unyanyasaji unaoripotiwa sasa.

"Mifumo hii iliwekwa katika mikono ya mrengo wa kulia zaidi, waziri mbaguzi zaidi wa rangi ambaye Israeli imewahi kuwa naye," Yuli Novak alituambia.

Kwake, namna Waisraeli wanavyowatendea wafungwa wa Kipalestina, kufuatia matukio ya kutisha ya Oktoba 7, ni kiashiria hatari cha kuzorota kwa maadili ya taifa.

"Jeraha na wasiwasi hutembea nasi kila siku," anasema.

"Lakini kuruhusu jambo hili kutugeuza kufanya jambo ambalo si la kibinadamu, ambalo halioni watu, nadhani ni jambo la kusikitisha."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi