Vifo visivyoelezeka vya Wapalestina kwenye magereza ya Israel

Chanzo cha picha, Supplied
Siku chache baada ya Hamas kushambulia Israel na vita kuzuka Gaza, Umm Mohamed katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu alipokea simu kutoka kwa mwanawe katika gereza la Israel.
"Niombee mama," Abdulrahman Mari alisema. "Mambo yanazidi kuwa magumu hapa. Huenda wasiniruhusu niongee na wewe tena".
Ilikuwa mara ya mwisho kusikia sauti yake.
Hali zilizidi kuzorota kwa wafungwa wa Kipalestina nchini Israel baada ya tarehe 7 Oktoba mwaka jana, wakati Hamas ilifanya mashambulizi yake mabaya kwa jamii za Waisraeli karibu na Ukanda wa Gaza, kulingana na Tume ya Masuala ya Wafungwa yenye makao yake huko Palestina.
Wafungwa 13 wa Kipalestina wamekufa tangu wakati huo katika magereza ya Israel, "wengi wao kutokana na kupigwa au kunyimwa matibabu", mkuu wa tume hiyo, Qadoura Fares, aliambia BBC.
Abdulrahman alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kufa.
Seremala huyu katika kijiji cha Qarawat Bani Hassan, alikuwa njiani akirejea nyumbani kutoka kazini huko Ramallah mwezi Februari mwaka jana alipokamatwa kwenye kituo cha ukaguzi. Alipelekwa katika kizuizi cha utawala - ambapo Israeli inaweza kuwaweka watu kwa muda usiojulikana bila kufunguliwa mashtaka - katika gereza la Megido.
Kaka yake Ibrahim alisema mashtaka dhidi yake ni madogo, kama vile kushiriki maandamano na kumiliki silaha, lakini akasema pia anatuhumiwa kuwa mfuasi wa Hamas ingawa hakuna mashtaka maalum kuhusu shughuli zozote ndani ya kundi hilo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ibrahim bado anajaribu kufahamu jinsi kaka yake alikufa. Anapaswa kutegemea ushahidi kutoka kwa wafungwa wenzake wa zamani wa Abdulrahman, pamoja na ripoti kutoka kwa vikao vya mahakama.
Mfungwa mwenzake mmoja wa zamani, ambaye alizungumza na BBC kwa sharti la kutotajwa jina, alisema: "Baada ya Oktoba 7, ilikuwa mateso makubwa. Walitupiga bila sababu, walitutafuta bila sababu. Hata ukimwangalia mtu vibaya. "
Alieleza kuwa alimuona Abdulrahman akipigwa sana mbele yake na wengine.
“Saa 9 alfajiri waliingia ndani ya seli yetu na kuanza kutupiga, mlinzi mmoja alianza kuwatukana wazazi wa Abdulrahman jambo ambalo hakulivumilia na kuanza kupigana.
"Walimpiga vibaya, na kumpeleka kwenye seli nyingine kwa wiki moja. Wakati huo unaweza kumsikia akilia kwa maumivu."
Alisema alikuwa amegundua tu kuhusu kifo cha Abdulrahman baada ya kutoka gerezani wiki moja baadaye.
Huduma ya magereza ya Israel haikujibu moja kwa moja maswali ya BBC kuhusu kifo cha Abdulrahman au yale ya Wapalestina wengine 12 ambao Tume ya Masuala ya Wafungwa inasema wamekufa, wakisema tu: "Hatufahamu madai yaliyoelezwa na tunavyojua si ya kweli."

Chanzo cha picha, Getty Images
Profesa Danny Rosin, daktari kutoka kundi la Madaktari wa Haki za Binadamu, alifanya uchunguzi kwa mwili wa Abdulrahman Mari. Matamshi yake yanathibitisha kile mwenzake Abdulrahman na kaka yake waliiambia BBC.
Ripoti ya Prof Rosin ilitaja kwamba michubuko imeonekana kwenye upande wa kushoto wa kifua cha kushoto Abdulrahman, na kwamba alikuwa amevunjika mbavu kadhaa. Michubuko ya nje pia ilionekana mgongoni, makalio, mkono wa kushoto na paja, na vile vile upande wa kulia wa kichwa na shingo.
Pia ilinukuu ripoti ya ziada ya polisi ambayo ilikuwa imetaja "kuzuia kwa nguvu" kwa Bw Mari siku sita kabla ya kifo chake.
Profesa Rosin alisema katika ripoti hiyo kwamba ingawa hakuna sababu maalum ya kifo iliyopatikana, "mtu anaweza kudhani kuwa vurugu aliyopata ilidhihirishwa na michubuko mingi na kuvunjika kwa mbavu nyingi kulichangia kifo chake".
Pia aliongeza kuwa "mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida" au "mshtuko wa moyo" yanaweza kusababishwa na majeraha haya bila kuacha ushahidi wowote wa kimwili.
Israel kwa sasa inawashikilia zaidi ya wafungwa 9,300 , wengi wao wakiwa Wapalestina kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za Israel la HaMoked, wakiwemo zaidi ya watu 3,600 walioko kizuizini cha utawala.
Takwimu hizi hazijumuishi wafungwa kutoka Ukanda wa Gaza wanaozuiliwa katika vituo tofauti na jeshi la Israel.
Bw Qadoura anasema mabadiliko hayo baada ya Oktoba 7 "yaliathiri hali ya maisha ya wafungwa", akidai kuwa wafungwa wamekuwa wakikabiliwa na njaa na kiu na baadhi ya wale walio na magonjwa sugu walinyimwa dawa. Vipigo vilizidi kuwa vya kawaida na vya kikatili zaidi.
"Nilikutana na mfungwa ambaye alikuwa amepungua kilo 20 katika miezi mitatu iliyopita," alisema.
"Ni kana kwamba vita dhidi ya Gaza pia vilikuwa vita dhidi ya wafungwa wa Kipalestina. Ilikuwa ni aina ya kulipiza kisasi."

Hapo awali BBC ilipata habari kutoka kwa wafungwa wa Kipalestina ambao walielezea kupigwa kwa vijiti,na kunyang'anywa nguo zao, chakula na blanketi wiki moja baada ya Oktoba 7.
Jeshi la magereza la Israel limekanusha unyanyasaji wowote, likisema kuwa "wafungwa wote wanashikiliwa kwa mujibu wa sheria huku wakiheshimu haki zao za kimsingi na chini ya uangalizi wa wafanyakazi wenye taaluma na ujuzi wa magereza".
Ilisema magereza yameingia katika "hali ya dharura" baada ya vita kuzuka na "imeamuliwa kupunguza hali ya maisha ya wafungwa wa usalam". Mifano ilitoa ni pamoja na kuondoa vifaa vya umeme na kukata umeme kwenye seli na kupunguza shughuli za wafungwa katika magereza.
Katika kijiji cha Ukingo wa Magharibi cha Beit Sira, babake Arafat Hamdan alionyesha mahali ambapo maafisa wa polisi wa Israel walikuwa wamepiga teke mlango wa nyumba ya familia yake na kuingia kwa nguvu saa 04:00 tarehe 22 Oktoba wakimtafuta mwanawe.
Polisi waliufunika uso wa mwanawe kwa kitambaa cheusi na kumfunga shingoni kwa kamba.Kilinuka sana, alisema, na Arafat ni wazi alikuwa na wakati mgumu kupumua akiwa amevaa.
"Niliendelea kujaribu kumfariji." Yasser Hamdan aliambia BBC. "Ni sawa. Hawana lolote dhidi yako. Hawana lolote dhidi yetu. Niliendelea kumwambia hivyo huku wakimfunga nje ya nyumba. Kisha wakamchukua."
Siku mbili baadaye simu ilikuja. Arafat alikuwa amepatikana amekufa ndani ya seli yake katika gereza la Ofer katika Ukingo wa Magharibi.
Mamlaka za Israel hazijaeleza jinsi alivyofariki. Arafat alikuwa na kisukari cha Aina ya 1 na angekabiliwa na viwango vya chini vya sukari ya damu mara kwa mara.
Baba yake alisema mmoja wa maafisa wa polisi waliomkamata Arafat alimwambia aje na dawa, lakini haikufahamika kama aliweza.
BBC ilipata ripoti ya Dk Daniel Solomon, daktari wa upasuaji ambaye alikuwepo katika uchunguzi wa maiti ya Arafat Hamdan kwa ombi la Madaktari wa Haki za Kibinadamu.
Dk Solomon alisema kuwa ilifanywa nchini Israeli mnamo Oktoba 31 lakini akaongeza kuwa hali ya mwili, kutokana na kuhifadhiwa kwa muda mrefu, ilifanya iwe vigumu kubaini chanzo cha kifo.
Pia alibaini kukosekana kwa rekodi zozote zinazoonyesha kama dawa ya kisukari ya Arafat ilikuwa imetolewa na kwa kipimo gani.
Ripoti hiyo pia ilitaja hitaji la uchunguzi mwingine zaidi ya uchunguzi wa maiti ili kubaini sababu ya kifo.

Miili ya Arafat wala Abdulrahman bado haijarejeshwa. Familia zao zinataka kupanga uchunguzi wa maiti zao wenyewe, kufanya mazishi, na kusema kwaheri ya mwisho.
"Alikuwa nyama na damu yangu. Kisha akaondoka kwa muda mfupi," Yasser Hamdan alisema. Picha za mtoto wake zilikuwa kila mahali ulipotazama katika nyumba yake.
Umm Mohamed alionyesha picha za Abdulrahman kwenye simu yake, akionyesha moja na kusema: "Mtazame. Alikuwa mchangamfu sana."
Baada ya muda alikuwa kiongozi katika kundi lake la wafungwa, alisema.
"Alikuwa ananipigia simu alipokuwa akiwaandalia kiamsha kinywa wakati wote walikuwa bado wamelala. Yeye ndiye aliyekuwa mchangamfu zaidi. Hangetulia."
Alililia. "Mrudishe kwangu. Ninataka kumuona kwa mara ya mwisho. Mtazamo wa mwisho."












