Madai ya uwongo ya 'vifo vilivyopangwa' yanaongezeka katika vita vya Israel-Gaza

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Olga Robinson & Shayan Sardarizadeh
- Nafasi, BBC Verify
Mama na babu wa mtoto wa Kipalestina Muhammad Hani al-Zahar mwenye umri wa miezi mitano – walikuwa wamebeba maiti ya mtoto huyo wakiwa mbele ya hospitali huko Gaza, siku ya kwanza ya mwezi Disemba.
Lakini picha za familia hiyo iliyojawa na huzuni kwa kumpoteza mtoto wao ziliposambaa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walidai Muhammad ni mwanasesere na si mtoto halisi.
Madai hayo yalichapishwa katika makala ya Jerusalem Post, gazeti lenye ushawishi mkubwa la Israel. Lilichapisha picha ya maiti ya Muhammad na kusema imethibitisha kuwa ni mwanasesere.
Baada ya kukosolewa, gazeti hilo liliondoa makala hiyo katika mitandao yake, na kisha kuandika kupitia mtandao wa X (Twitter), kwamba ripoti hiyo "ilitokana na chanzo kisichoaminika."

Chanzo cha picha, ABC NEWS
Wiki chache kabla ya hapo, video ya ndugu watatu wa Kiisraeli - Rotem Mathias1 (6) na dada zake wawili, Shakked na Shir, ilisambaa mitandaoni. Rotem alishuhudia wazazi wake wakiuawa na wapiganaji wenye silaha wa Hamas tarehe 7 Oktoba, walipokuwa katika nyumba yao huko Kibbutz karibu na mpaka na Gaza.
Video hiyo ilijumuisha mchanganyiko wa video za mahojiano ya ndugu hao na runinga za Marekani, ABC na CNN siku chache baada ya shambulio la Oktoba 7.
Madai ya uongo yalisambaa kuwa ndugu hao walikuwa "waigizaji" waliokuwa wakidanganya kuhusu vifo vya wazazi wao huku wakijizuia kucheka mbele ya kamera.
Pallywood na Kuitetea Hamas

Hiyo ni mifano miwili tu - ikionyesha mgawanyiko wa kijamii juu ya vita vya Israel na Gaza na watu kukanusha ukatili na mateso ya raia wanayopitia katika mzozo huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mojawapo ya kauli zinazotumiwa kukataa au kudogosha mateso ya huko Gaza ni "Pallywood,’’ yaani mchanganyiko wa "Palestina" na "Hollywood."
Wale wanaotumia kauli hiyo huchapisha mara kwa mara katika mitandao video wanazodai ni za uwongo au zilizoigizwa za Wpalestina wakijifanya waathiriwa.
Uchunguzi wa BBC umebaini katika mtandao wa kijamii wa X pekee, neno "Pallywood" limepata idadi kubwa ya wanaolitumia katika kipindi cha miaka kumi.
Wakati wa mapigano ya hapo awali ya Israel na Palestina ya mwaka 2014, 2018 na 2021 neno "Pallywood" lilitajwa katia ya mara 9,500 hadi 13,000 ndani ya mwezi mmoja katika mtandao wa X.
Baada ya shambulio la Oktoba 7 la Hamas, idadi ya waliolitumia imefika 220,000 hadi mwezi Novemba.
BBC imegundua kuwa miongoni mwa waliolitumia neno "Pallywood" kwenye mitandao ya kijamii ya X, Facebook na Instagram katika miezi iliyopita, ni maafisa wa Israel, watu mashuhuri na wanablogu maarufu kutoka Israel na Marekani.
Machapisho yao hupata maoni ya mamilioni ya watu kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa upande mwingine, wale wanaunga mkono Wapalestina huchapisha madai ya uongo ya kukanusha ukatili uliofanywa na Hamas tarehe 7 Oktoba nchini Israel.
Baadhi ya wafuasi hao hutoa madai ya uongo kwamba Hamas haikuua raia siku hiyo, au kiwango cha vifo vya raia kimetiwa chumvi sana. Wengine wanaenda mbali zaidi, wakidai wengi wa waathiriwa waliuawa na Jeshi la Ulinzi la Israeli, sio Hamas.
Wataalamu wanasemaje?
Wataalamu wa upatanishi wana wasiwasi kwamba taarifa potofu ambazo zinakanusha mateso ya upande mwingine zinaweza kudhoofisha utu, na zinaweza kuathiri mustakbali wa baadaye wakati wa kurekebisha uhusiano kati ya jamii zilizoathirika.
"Hatari kubwa zaidi, nadhani, ni kupotea kwa uaminifu na huruma," anasema Harriet Vickers, kiongozi wa shirika la Tim Parry and Johnathan Ball Foundation For Peace. Shirika la hisani linalosaidia wahanga wa migogoro, vurugu za kisiasa na vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kuwa taarifa za uwongo na matamshi ya kudhalilisha utu pia yanaweza kuwa na athari kubwa zaidi ya kuendeleza uchungu ambao waathiriwa wamepitia."
Taarifa za uwongo kuhusu au kukanusha ukatili si mapya kwa wale wanaosoma kuhusu habari ghushi.
Dhana ya "wahusika wa mgogoro" - yaani watu wanaojifanya au kulipwa ili kuigiza janga fulani au maafa - imekuwa maarufu miongoni mwa waendelezaji wa nadharia hiyo kwa miaka mingi.
Ilitumiwa vibaya kudai kwamba wazazi wa watoto waliouwawa katika shambulio la shule ya Sandy Hook nchini Marekani walikuwa kwa namna Fulani wakitengeneza misiba yao binafsi.
Katika miaka michache iliyopita madai sawa na hayo yalichapishwa kuhusu mauaji ya raia wa Ukraine huko Bucha na waathiriwa wa vita nchini Syria.
Lakini wingi wa matamshi ya udhalilishaji yaliyochapishwa wakati wa vita ya Israel na Hamas - yamewashangaza hata wale wanaofuatilia maudhui ya aina hiyo kila siku.
Eliot Higgins, mwanzilishi wa tovuti ya uchunguzi ya Bellingcat ambayo inafuatilia vita vya Syria na Ukraine, anasema wingi wa taarifa za uongo katika vita vya sasa vya Israel na Gaza ‘inatisha.’
"Watu wengi wana maoni makali sana kuhusu pande zote mbili za mzozo huu, kuna watu huchapisha taarifa kwa sababu zinawahusu kihisia. Hawajali kama ni kweli au la."
Uongo Zaidi na Zaidi

Chanzo cha picha, MAHMOUD RAMZI
Mwezi Novemba, video inayoonyesha vipodozi na damu bandia vikipakwa kwenye uso wa mwigizaji mtoto ilichapishwa kwenye X na Ofir Gendelman, msemaji wa Waziri Mkuu wa Israel katika ulimwengu wa Kiarabu.
"Jioneeni wenyewe jinsi wanavyotengeneza majeraha bandia wakiwa mbele ya kamera," Gendelman aliandika kwenye chapisho lililotazamwa mara mamilioni kabla ya kufutwa.
Video hiyo, kwa hakika, ilikuwa ni ya maandalizi kutoka katika filamu ya Lebanon ya sekunde 45 iliyotengenezwa kwa ajili ya kuwaenzi watu wa Gaza na ilichapishwa mtandaoni mwezi Oktoba.
Mwongozaji wa filamu hiyo Mahmoud Ramzi, ambaye aliandika kwenye Instagram kukanusha madai ya uwongo yaliyotolewa kuhusu filamu yake, aliiambia BBC, ''habari hiyo potofu imeshindwa, kinyume chake imesaidia filamu yake kufikia hadhira kubwa zaidi.''
BBC ilimtafuta Gendelman kutoa maoni yake lakini hajajibu.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
James Longman, mwandishi wa ABC ambaye alimhoji Rotem na dada zake, anasema.
“Alikuwa akitokwa na machozi, dada yake anatokwa na machozi, babu yao aliyekuwa nasi, mpigapicha wetu, wafanya kazi wa hospitali, wauguzi, madaktari na mimi tulikuwa tunatokwa na machozi, wote tumekaa pale tunasikiliza anachosema," aliiambia BBC.
Longman anasema alishtuka alipoona madai ya uwongo kuhusu ndugu hao yakisambazwa mtandaoni na kumfanya aandike kwenye X ili kuyapinga. Ujumbe wake ulienezwa sana, na kusababisha moja ya ujumbe wa uongo kuhusu ndugu hao kufutwa na mtu aliyeuchapisha.
End of Pia Unaweza Kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












