Jinsi ya kugundua taarifa za uongo
Rashid Abdallah

Mitandao ya kijamii ni miongoni mwa maendeleo ya karne hii. Ingawa haina maana kila kitu ni kizuri katika mitandao hiyo, kuna orodha ya mambo ambayo hayapaswi kuwepo lakini yanakuwepo kwa sababu udhibiti ni mgumu kutokana na wingi wa watumiaji.
Ukiachilia mbali mazungumzo ya chuki na ubaguzi, ambayo hutamalaki katika mitandao. Pia, ni kiwanda kikuu kinachozalisha habari za uongo kila siku. Watu hujitungia taarifa kutoka vyumbani mwao – kwa lengo la kuchafua wengine, maslahi binafsi ama kupotosha tu.
Panapohusika taarifa za uongo, kuna mambo mawili huendana; intaneti (wavuti) na taarifa zenyewe za uongo. Hawa ni watoto mapacha. Kwa sababu intaneti inatoa jukwaa kwa kila mmoja kuchapisha anachotaka, maadamu ana simu na data ya kuunganisha.
Makala haya yana lengo la kukueleza mbinu ambazo utaweza kuzitumia, kugundua taarifa za uongo hasa zile zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii na tovuti mbali mbali.
Tazama vyombo vingine
Ulimwengu wa sasa umejaa vyombo vya habari, vile vya kimataifa na vya ndani. Taarifa ambayo ni muhimu haiwezi kuwa ipo katika tovuti au akaunti ya chombo kimoja pekee. Ikiwa taarifa huioni katika vyombo vingine hiyo ni dalili kwamba ni uongo.
Duniani kuna mashirika makubwa ya habari, yanayoaminika mfano;= Associated Press (AP), Agence France Presse (AFP), Anadolu Agency, Reuters na mfano wa hayo. Pia, vyombo vya habari vya ndani vinavyoaminika, ndio maeneo ya kuyatumia kuhakiki taarifa ikiwa imechapishwa huko.

Akaunti rasmi au bandia
Mbinu nyingine kujua taarifa ya uongo au ya kweli, ni kuangalia ikiwa taarifa hiyo imechapishwa katika akaunti rasmi inayojulikana. Ikiwa utakuta habari ipo katika akaunti ambayo sio rasmi wala maarufu miongoni mwa akaunti za kupasha habari, hiyo ni taa nyekundu.
Taarifa ya uongo mara nyingi huchapishwa katika akaunti za kughushi. Hapo ni kusema, ili kujua taarifa za uongo inabidi uwe na ujuzi wa kujua akaunti za uongo ama ghushi.
Chanzo cha taarifa
Ikiwa ni habari ambayo inatangaza juu ya kifo cha mtu fulani maarufu. Ni muhimu kuzingatia nani katoa hiyo taarifa. Je, mwandishi wa taarifa ametaja chanzo cha taarifa yake kaipata wapi?
Kuna taarifa nyingi zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii na zinabaki kuwa taarifa hewa haijulikani nani kasema. Ikiwa msanii maarufu kutoka Tanzania amefariki, tegemea chanzo cha kifo chake kimethibitishwa na familia, meneja wake ama daktari wa hospitali alikopokelewa au Polisi.

Alama za uandishi
Kwa sababu mara nyingi taarifa za uongo huandikwa na watu ambao hawana taaluma ya uandishi hasa wa habari, mbinu nyingine ya kujua ni kuangalia uandishi wa hiyo taarifa kwa kuzingatia matumizi ya alama za uandishi.
Nikisema alama za uandishi nakusudia, kituo kikubwa, kituo kidogo, mabano, funga semi na fundua semi, nukta mbili, alama ya kuuliza na mfano wa hizo, ambazo wakati mwingine hukosea namna ya kuzitumia.
Zingatia picha
Wachapishaji wa taarifa za uongo wana tabia ya kuunganisha picha ili kushika hisia za mtazamaji. Mfano, unaweza kukuta picha ya mtu maarufu akionekana anatoka machozi. Ukitazama kwa makini utagundua machozi yale sio yake, yamewekwa kwa programu za picha.
Habari hizo pia hutumia picha zenye kuleta msisimko, mfano picha inaoyesha ajali. Ingawa ajali hiyo inaweza isiwe unahusiana na taarifa aliyo ichapisha, bali huwekwa ili kumvuta mtu ashughulike na taarifa hiyo. Pia, ubora wa picha huwa mdogo.

Kichwa cha kuteka hisia
Katika mtandao mfano wa YouTube utakutana na video nyingi zinaambana na vichwa vya habari vinavyolenga kukamata hisia za mtu, ili kumfanya abonyeze na kufungua video hiyo. Kisha utakuta video haiendani na taarifa iliyolezwa katika kichwa cha habari.
Mbinu hii hutumika hata katika filamu zinazowekwa katika mtandao huo. Unaweza kusoma kichwa chenye kueleza fulani fulani maarufu ya mwingizaji anayeheshimika, ila ukifungua kuna filamu nyingine waigizaji wake hawana majina makubwa.
Uliza wajuzi
Mbinu nyingine ni kuuliza wajuzi wa mambo. Kuna watu ni wataalamu wa mitandao ya kijamii, waandishi wa habari wanaotambulika ama wataalamu wa kujua taarifa za kweli na uongo.
Ikiwa mbinu zote hizo zimeshindwa kufanya kazi, unaweza kuuliza yule ambaye unamwamini.
Intaneti imekuja na faida nyingi, ila kuenea kwa taarifa za uongo ni changamoto iliyokuja nayo.
Uandishi habari wa kiraia, mara nyingi huingia kwenye mkumbo huu kwa sababu taarifa huandikwa na mtu mmoja, haipitiwi na mtu mwingine na huchapishwa. Ni hatari kusoma taarifa za uongo na kuziamini.












