Homa ya Nyani: Kwa nini Mpox inaenea kwa kasi Afrika Mashariki na Kati?

    • Author, Makuochi Okafor & Chigozie Ohaka
    • Nafasi, BBC News
    • Akiripoti kutoka, Lagos, Nigeria
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imekumbwa na ongezeko la wagonjwa wa homa ya nyani ama Mpox. Hilo limepelekea hatua za dharura za afya kwa umma kuchukuliwa.

Uganda pia imethibitisha kesi mbili mpya za Mpox, kama ilivyo kwa Kenya, Rwanda na Burundi katika ripoti kuhusu milipuko wa homa hiyo Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa ripoti ya Africa CDC, idadi ya kesi zimeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana, na idadi ya vifo imeongezeka vilevile.

Umoja wa Afrika umeidhinisha dola milioni 10.4 kutoka katika fedha zilizopo za Covid kusaidia Afrika CDC, katika kukabiliana na mlipuko wa Mpox katika bara zima.

Kesi nyingi na vifo viko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mwaka huu pekee, kumekuwa na visa zaidi ya 8000 vilivyoripotiwa na zaidi ya vifo 300.

Dk Fiona Braka, Meneja wa Dharura wa Shirika la Afya Duniani nchini Congo Brazzaville, anasema "kesi zimeripotiwa katika nchi 11 za eneo hilo tangu mwanzoni mwa 2024."

"Tunaona kesi nyingi zaidi nchini DRC, ambayo inachukua asilimia 96 ya kesi zote ambazo zimeripotiwa katika eneo hili," anasema.

Visa viwili vya ugonjwa huo unaoambukiza viliripotiwa hivi karibuni nchini Rwanda na Jamhuri ya Afrika ya Kati, (CAR), siku chache tu baada ya Burundi kutangaza uthibitisho wa kesi.

Hivi karibuni, nchi jirani ya Kenya pia imeripoti kisa kilichogunduliwa kwa msafiri aliyekuwa akitoka Uganda kwenda Rwanda kupitia kivuko cha mpaka kusini mwa nchi hiyo.

Hali hii imezua wasiwasi kuhusu kuenea kwa aina mpya na mbaya ya ugonjwa huo.

Afrika Kusini pia ilirekodi visa vya virusi hivyo, na vifo vitatu, lakini vipimo vya awali vinaonyesha maambukizi hayo yamesababishwa na aina isiyo hatari sana ya virusi hivyo.

Wataalamu wa afya wanasema virusi hivyo vinabadilisha tabia yake, vinajitokeza miongoni mwa makundi mapya, kama vile wafanyabiashara ya ngono.

Ugonjwa huu huenea kwa njia ya mawasiliano ya kimwili na ya ngono na unaweza usigundulike kwa kutazama kwani baadhi ya watu hawaonyeshi dalili.

Pia unaweza kusoma

Mpox ni nini?

Ugonjwa wa Mpoksi, hapo awali ulijuulikana kama monkeypox, ni ugonjwa unaosababishwa na virusi. Dalili zake ni homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, na upele unaosambaa kutoka kwenye uso hadi sehemu nyingine za mwili.

Mpox huenea kupitia mgusano wa mtu na mtu na imethibitishwa kupitia vipimo vya maabara juu ya mgusano wa vidonda vya ngozi.

Kuna aina mbili kuu za virusi vya Mpox (MPVX): MPVX Clade IIb na MPXV Clade I.

Mlipuko wa kimataifa wa mwaka 2022 ulisababishwa na aina ya MPXV Clade IIb, lakini wanasayansi wanasema aina hiyo inayoenea nchini DRC sasa ni tofauti ya aina ya MPXV Clade I ambayo ni kali zaidi na hatari sana.

Changamoto za kukabiliana nao

Visa vya Mpox vipo zaidi katika eneo la mashariki mwa DRC, hasa katika jiji la uchimbaji madini la Kivu Kusini-Kamituga – eneo la mpakani lenye utitiri wa wafanyabiashara, mafundi, wachimba madini, na wafanyabiashara wengine.

Dk Steeven Bilemo Kitwanda, ambaye amekuwa akifanya kazi katika kituo maalumu cha matibabu cha Mpox huko Kamituga, anasema ana wasiwasi na mienendo ya watu katika mkoa huo.

"Ni ngono zembe ndio inayosababisha ugonjwa huo kuenea na watu wanaokuja hapa [Kamituga], hawadhibitiwi. Wanaondoka kwenda Goma, Gisenyi nchini Rwanda, Bujumbura na kwengineko," anasema.

Kamituga ni kitovu cha kibiashara na maisha yaliyochangamka ya usiku, kumejaa baa na wafanyabiashara ya ngono.

Kulingana na Dk Kitwanda, kesi za kwanza zilirekodiwa miongoni mwa wachimba migodi, na kusababisha baadhi ya wanajamii kuamini kuwa ugonjwa huo ni laana ya Mungu kwa sababu ya Uasherati.

Miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, Mpox huonekana kuwa ni ugonjwa wa watu wasio na adabu au wahuni na unaochukuliwa kuwa ni ugonjwa wa aibu.

Dk Kitwanda anasema unyanyapaa huu unazuia watu kutafuta usaidizi wa matibabu na umeongeza usiri kuhusu maambukizo, jambo ambalo hufanya ufuatiliaji wa watu kuwa mgumu.

Hilo huvifanya virusi kuenea bila utambuzi, haswa kati ya wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao na wafanyabiashara ya ngono.

Anasema kuna haja ya kufanyika ufuatiliaji maalumu kwani mara nyingi watu huficha utambulisho wa wapenzi wao. Watu wengi walioathirika na ugonjwa huo pia wana VVU, jambo ambalo linaweza kufanya maambukizi kuwa mabaya zaidi.

Nje ya vituo vya mijini, viongozi wanajitahidi kufuatilia virusi hivyo katika maeneo ya vijijini huku kukiwa na migogoro inayoendelea.

Nini kifanyike?

Hatua za kimsingi za afya ya umma zichukuliwe kama vile mawasiliano, upimaji, matibabu, ufuatiliaji wa watu wanaokutana nao, na ushirikishwaji wa jamii – yote hayo ni muhimu ili kupambana na Mpox.

Leandre Murhula Masirika, mŕatibu wa utafiti wa Mpox nchini DRC, anasema mipaka isiyo na uangalizi ni moja ya changamoto kuu katika kukabiliana na ugonjwa huo.

"Hakuna udhibiti kwenye mipaka. Kamituga ina mipaka miwili na watu hutoka hapa kwenda Rwanda na Burundi," anasema.

Virusi hukaa takribani siku nne hadi 20 kuonekana na wakati mwingine vidonda vinaonekana tu kwenye sehemu ya siri. Masirika anasema, hilo hufanya kuwa vigumu kugundua ugonjwa, hivyo kupima mpakani ni muhimu.

Mratibu wa utafiti anasema kuwe na mawasiliano na makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa na unyanyapaa, ili kuzuia kuenea.

Hali nchini DRC sasa iko katika kiwango cha maambukizi ya jamii, huku akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wakiwa hatarini zaidi.

"Virusi hivi vimeibuka katika familia zenye watoto, mama zao, na hata wajawazito, jambo ambalo limesababisha utoaji wa mimba kuongezeka," anasema Masirika.

Nchini DRC, watoto wengi, wakiwemo wachanga, wameambukizwa. Pia kumekuwa na visa vichache vya wanawake wajawazito kuharibu mimba. Wagonjwa wengine wameteseka kwa muda mrefu na maambukizi ya macho, ngozi, na sehemu zao za siri.

Wito wa haraka wa chanjo

Virusi hivyo vinapoenea, wataalamu wa afya duniani wanatoa wito wa kampeni ya chanjo. Wakati DRC na Afrika Kusini zimeanza mchakato wa kuomba chanjo, bado hakuna chanjo iliyofika.

Marekani na Japan zimeahidi kutoa chanjo, lakini bado hazijapelekwa.

"Chanjo haipo, na watu wanakufa," anasema Masirika, mtafiti wa Mpox.

Mapema mwaka huu, DRC ilitangaza mipango ya kutumia aina mbili za chanjo ya Mpox. Mamlaka ya Kitaifa ya Udhibiti imeanza kukagua chanjo hizi, lakini bado hazijatolewa kwa matumizi.

Dr Braka wa WHO anasema shirika lake linazidisha juhudi katika nchi mbalimbali ili kuimarisha ufuatiliaji na kuboresha mifumo ya upashanaji habari.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriw ana Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah